HUKO mtaani mashabiki wa Simba angalau kwa sasa wanatabasamu kutokana na kiwango cha kuvutia cha timu hiyo, iliyoaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa kwanza nyumbani dhidi ya Stade Malien ya Mali, lakini kuna kocha mmoja ameshtushwa na kazi ya nyota wapya wa timu hiyo.
Simba iliongeza mashine kama saba katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 30 wakiwamo Clatous Chama, mabeki Nickson Kibabage, Ismael Toure, kipa Djibril Kassali na viungo washambuliaji walioanza kuwasha moto, Libasse Gueye, Anicet Oura na Inno Jopsin Loemba kiasi cha kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdelhakh Benchikha kukiri timu hiyo itawashangaza wapinzani wao.
Benchikha aliyeinoa Simba kwa muda mfupi mwaka 2024 kabla ya kurejea kwao Algeria, amekiri klabu hiyo imeshusha vyuma vya maana dirisha dogo, lakini wanahitaji kitu kimoja tu ili kikosi hicho kiimarike zaidi na kuja kuwashangaza wapinzani katika michuano ya ndani kwa msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha amesema ameona timu hiyo imefanya usajili mkubwa na mzuri katika dirisha dogo, japo kuna baadhi hawajacheza kwa muda mrefu ila mchezaji bora anaonekana mapema kama kasi walizoanza nao kina Oura, Gueye na Loemba.
Amesema, kuna wachezaji kama watatu amewaona wana ujuzi wa kutosha na kama kocha ataendelea kuwanoa vyema wanaweza kuisaidia sana Simba katika kipindi hiki ambacho mashabiki wanahitaji kuona timu ikifanya vizuri.
“Kuna kikosi kizuri sana chenye mchanganyiko mzuri wa vijana na wachezaji wenye uzoefu zaidi, hii ni picha kwamba Simba inaendelea kuimarika,” amesema Benchikha na kuongeza;
“Nimeona kuna mawinga wazuri sana Loemba, Anicet Oura na Libasse Gueye wana ujuzi wa kutosha, nguvu na njaa ya mafanikio kama wakiunganishwa vizuri kutakuwa na timu imara sana. Kocha (Barker) apewe muda watu waamini kwenye mabadiliko, ni mpya na wachezaji wengi ni wapya wanahitaji kuzoeana wote vizuri ili kuunda timu sasa itakayokuwa tishio.”
Benchikha amesema, mashabiki, viongozi na wachezaji kwa ujumla wasijione kwamba wana msimu mbaya kwa kutoka kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ila waone ni fursa ya wao kubeba ubingwa wa mashindano yote yaliyosalia.
“Kuna wakati kwenye mpira unaweza kuwa na timu nzuri ukakosa matokeo mazuri. Hii haitokei Simba peke yake lakini baadaye mambo yanarudi kuwa sawa, hiyo ndio soka.
“Simba na watu wake wote waamke kupambania mashindano yaliyobaki, hiki ni kipindi kifupi na kushindwa kimataifa hakushushi heshima yao ila kunawapa nguvu ya kujiapanga mapema na upya.”
Tangu mastaa hao watue Simba katika dirisha dogo wamecheza mechi mbili tu za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa na KMC, huku kati yao Gueye akiongoza kwa kufunga mabao akiwa nayo mawili.
Simba imemaliza mkiani katika Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na pointi 5, nyuma ya vinara Stade Malien, Esperance na Pedro de Luanda.