Matukio ya wizi, uvamizi yatia hofu Mbeya, Polisi yatoa tahadhari

Mbeya. Hofu imetanda kwa wananchi jijini Mbeya kufuatia matukio ya uvamizi, uporaji simu na mikoba yanayofanywa na kundi linalotumia pikipiki, huku umoja wa wasafirishaji ‘Bodaboda’ ukitangaza msimamo ili kukomesha uhalifu huo.

Hata hivyo, Polisi mkoani Mbeya limewasihi wananchi wanaokumbwa na matukio hayo kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi ili kuweza kufuatilia na kuchukua hatua za haraka kwa wahusika.

Matukio hayo yanatajwa kushamiri katika mitaa ya Makunguru, Ilemi, Isanga, Soweto na Mwenge, ambapo kundi hilo linatajwa kutumika kukwapua simu, mikoba na kujeruhi wananchi nyakati za usiku.

Inadaiwa kundi hilo linatumia pikipiki ambapo huficha pleti namba japokuwa inadaiwa hawajasajiliwa wala kutambulika na umoja wa Bodaboda, wengine kutembea kwa makundi muda mwingine mtu mmoja mmoja.

Pia katika msako wa hivi karibuni wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Januari 27 hadi Februari 5 tayari umekamata watuhumiwa wawili Charles Oden na Isack Charles kwa kuingilia mfumo wa kibiashara, huku uchunguzi ukionesha baadhi ya simu ziliibiwa maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.

Kauli ya uongozi wa bodaboda

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Umoja wa wasafirishaji ‘bodaboda’, jijini Mbeya, Aliko Fwano amesema matukio hayo yamekuwapo kwa takribani miaka mitatu sasa, akieleza wanaendelea na doria kila kituo cha bodaboda kubaini wahusika.

Amesema kwa siku za nyuma kulikuwapo na changamoto ya kuuawa kwa waendesha pikipiki ‘bodaboda’, lakini uongozi kwa kushirikiana na Jeshi la polisi waliweza kuchunguza matukio hayo na kuyakomesha.

“Hayo matukio hayajaanza leo ni kama miaka mitatu, lakini tunaendelea na doria kwakuwa bodaboda wetu wamesajiliwa kwa vikundi na tunawatambua, tunahangaika na hao wanaotuchafua mitaani.”

“Awali kulikuwepo na matukio ya kuwaua bodaboda lakini tunashukuru Jeshi la Polisi walivyotupa ushirikiano kwa kutokomeza uhalifu huo, na sasa tunaendelea kuomba jeshi letu litupe ushirikiano tuondoe hili kundi,” amesema Fwano.

Hata hivyo ameongeza kuwa wapo watuhumiwa wanapokamatwa huwekewa nguvu na baadhi ya viongozi akieleza kuwa ili kukomesha vitendo hivyo inahitaji ushirikishwaji wa jamii, viongozi na umoja wa bodaboda.

Baadhi ya waendesha pikipiki wamesema makundi hayo si waliopo kwenye mfumo wao bali wengine hutokea maeneo ya mbali kuja maeneo ya mjini kufanya uhalifu.

Victor Mwanjalila amesema uongozi wa bodaboda unapaswa kufuatilia zaidi kwa kuwa watuhumiwa huenda wanatoka sehemu za wilayani kuja mjini kufanya vitendo vya uhalifu na kuharibu picha yao jijini humo.

Amesema wamekuwa wakipata malalamiko ya baadhi ya wananchi maeneo mbalimbali wakilia kukwapuliwa simu na mikoba hasa wakati wa jioni, hali ambayo inawapa wakati mgumu kufanya majukumu yao.

“Sisi tunaheshimu kazi zetu kwa kuwa Serikali inatutambua, hao wanaofanya uhalifu huo tunahisi wengi wao wanatoka nje ya Jiji kwani hawana vituo maalumu, wala kutambulika popote” amesema Mwanjalila.

Naye Paschal Gilbert amesema Jeshi la Polisi linapaswa kuweka mitego katika maeneo korofi hasa eneo la Isanga darajani, Ilemi na Mwenge akieleza kuwa mitaa hiyo ndio inatajwa kushamiri vitendo hivyo.

“Wengine tumeamua inapofika saa 2 usiku tupaki vyombo vyetu tulale, vilio kwa wananchi vimekuwa vingi, niombe au kushauri Polisi waweke mitego maeneo hayo, hata sisi tunakutwa na matukio usiku” amesema Gilbert.

Demtrida Ntakija mkazi wa Soweto amesema Februari 5,2026 akitoka kwenye majukumu yake alikwapuliwa simu yake aina ya Tecno ikiwa ni mara ya pili kukutwa na tukio hilo katika barabara ya Mkapa mtaa wa Makunguru.

“Nimelizwa mara mbili, awali walinikwapua mkoba ni vile haukuwa na vitu muhimu sana zaidi ya pesa Sh20,000, siku hiyo simu niliishika mkono wa kushoto nikawa naongea, lakini juzi eneo lilelile wakanikwapua simu” amesema Demetrida.

Naye Daud Faustine amesema mitaa ya Ilemi na Mwenge si salama kwa kuwa matukio hayo yamewakuta wengi na baadhi yao wamepigwa na kujeruhiwa na kunyang’anywa mali zao.

“Nilikabwa nikanyang’anywa simu na fedha taslimu, wakiona unawazidi nguvu wanakujeruhi, Jeshi la Polisi litusaidie kufanya doria maeneo hayo mara kwa mara” amesema Faustine.

Kwa upande wake, Samuel Ndoni amesema alivamiwa na kundi la vibaka waliompiga na kumjeruhi na kuchukua fedha Sh38,000 na bidhaa alizokuwa amenunua dukani ambapo alitoa taarifa kituo cha Polisi Mwanjelwa.

“Nilikuwa natoka redioni kazini, nimefika pale Uhai Mwenge ndio nikavamiwa ilikuwa saa 2 hivi usiku, wakanipiga na kuchukua simu na Sh38,000 na bidhaa nilizokuwa nimenunua” Amesema Mwandishi huyo wa kituo cha Highlands FM.

Naye mwandishi wa habari, Rashid Mkwinda amesema Januari 20,2026 alivamiwa na vibaka waliompiga na kumjeruhi hadi kulazwa hospitalini huku wakimnyang’anya fedha taslimu.

“Ilikuwa saa 6 usiku mtu huyo alikuwa akinifuata nyuma sikuhofia kitu kwa kuwa watu walikuwa bado barabarani, alikuwa ameshikilia kitu kama simu na tochi ya mwanga mkali”

“Nikajua labda ni mpangaji mwenzangu pale nyumbani mtaa wa Kati Soweto, ile nimefika mlangoni nikapigwa kichwani, nageuka nikaongezewa kipigo, nikaanguka nikapiga kelele.”  

“Ninachokumbuka begi lililokuwa na kamera nililirusha kwa ndani likanusurika kuibiwa, ila simu mbili zilikuwa mfukoni na Sh55,000 walizichukua na kukimbia, ambapo majirani walikuja kunisaidia kunipeleka hospitali,” amesema Mkwinda ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe.

Akielezea matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga amesema hajapata taarifa hizo, akiwaomba wananchi kutoa taarifa kituo chochote cha polisi wanapokutwa na majanga hayo ili waweze kufanyia kazi kwa haraka.

Hata hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ilieleza katika msako uliofanywa Januari 27 hadi Februari 5 waliwashikilia watuhumiwa wawili kwa kuingilia mfumo wa kibiashara wa kampuni ya ukopeshaji simu.

Waliokamatwa kwa tuhuma hizo ni Charles Oden ‘Mwakasege’ ambaye ni fundi simu mkazi wa Meta na Isack Charles ‘Bebwa’ mkazi wa Shewa jijini Mbeya ambao baada ya upekuzi ofisini kwao walikutwa na simu aina ya Samsung 53, Infinix 21, Tecno 13,Itel 11, Yas 1.

“Simu zilizokamatwa zilifanyiwa ukaguzi wa awali na kutambuliwa na kampuni zinazokopesha watu mbalimbali na nyingine zimetambuliwa ziliibiwa maeneo tofauti jijini Mbeya.”

Kamanda huyo ametoa rai kwa wananchi wenye tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali kuacha mara moja na badala yake watafute shughuli halali kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi kwa jamii.