NMB yakutanisha pamoja Wananchi kupitia Kijiji Day

Wananchi wa Kijiji cha Somanga wameiomba Benki ya NMB kufanya bonanza mara kwa mara ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uwekaji na fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi hiyo.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 16, 2026 baada ya kumalizika kwa mashindano yaliyoandaliwa na benki hiyo, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Somanga, Fatuma Ramadhan ameishukuru benki hiyo katika utoaji wa huduma maeneo ya vijijini, kupata elimu ya uwekaji na utunzaji wa fedha, na kuomba iwe inafanya mabonanza kama hayo mara kwa mara.

“Niwashukuru NMB kwa kutupa elimu ya fedha, binafsi nilikuwa sifahamu chochote lakini walichokifanya leo ni kikubwa mno, tunawaomba  wawe wanafanya mara kwa mara ili wengi wanufaike kama ilivyotokea kwetu,” amesema Ramadhani

Meneja Mauzo Kanda ya Kusini wa NMB, Frank Njawala amesema maana ya kufanya bonanza la Kijiji Day ni ili kuwafikia wakulima wote wadogo wadogo maeneo ya vijijini  na kutoa elimu ya kifedha, huduma za fedha na kushiriki michezo kwa kuwaunganisha pamoja wananchi.

“Kijiji Day inasaidia kwa wakulima, wafanyabiashara, wananchi wa kawaida kupata elimu ya kifedha  kukutana pamoja, kufungua account pamoja na kufanya miamala ya hapo kwa papo bila kwenda mbali,” amesema Njawala.

Pia mbali na hayo, lakini wanajifunza jinsi ya kutunza fedha katika vikundi vyao, kupata fursa za mikopo mbalimbali ambayo inatolewa na NMB.

Kwa upande wa Kaimu Meneja wa NMB Wilaya ya Kilwa, Agustino Manguya amesema  bonanza la Kijiji Day kwa mkoa wa Lindi ni mara yao ya pili kufanya hivyo na  malengo yao ni kuwafikia wananchi wote ambao wapo vijijini kupata fursa mbalimbali zinazotokana na taasisi hiyo.

Amesema wameamua kufanya katika Kijiji cha Somanga ili  kuwajulisha wananchi kuwa kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti za NMB, kwani kuna fursa nyingi na pia malengo ya benki ni kuwafikia wananchi wote wa vijijini.

“Napenda kuwaambia wananchi wa Somanga na Kilwa kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kufungua akauti za NMB kwani kuna fursa nyingi ambazo zinapatikana katika benki hiyo ikiwemo mikopo ya wakulima, wanawake na wafanyabiashara,” amesema Manguya.                                                                                                   

Hata hivyo, michezo mbalimbali ilichezwa ikiwemo kukimbiza kuku, soka, kukimbia kwa magunia pamoja na kukimbia na yai mdomoni.