KOCHA wa Transit Camp, Shadrack Nsajigwa, amesema matokeo mabaya ya timu hiyo raundi ya pili hayatokani na kuhamishia mechi za nyumbani kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani, tofauti na walivyokuwa Kituo cha Ufundi cha TFF.
Kauli ya Nsajigwa, inajiri baada ya kuanza raundi ya pili ya Ligi ya Championship kwa kuchapwa mechi mbili kwenye Uwanja wa Filbert Bayi inaoutumia nyumbani, ikianza kwa mabao 2-1, dhidi ya Kagera Sugar, kisha bao 1-0, mbele ya Geita Gold.
“Kuzungumzia suala la uwanja kwangu nadhani sio sababu iliyochangia, tunapaswa kutambua ushindani katika Ligi ni mkubwa na hii ndio raundi ngumu kuliko ya kwanza, changamoto ni umaliziaji ambao tunaendelea kupambana nao,” amesema Nsajigwa.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, aliyejiunga na Transit Camp akitokea Namungo alipokuwa ni kocha msaidizi wa Juma Mgunda, amesema katika mechi 12, zilizobaki ataendelea kutengeneza timu ya kuendana na ushindani.
Msimu huu kikosi hicho cha maafande kinashika nafasi ya nne na pointi zake 36, baada ya kushinda mechi 11, kikitoka sare tatu na kupoteza minne kati ya 18, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.