KOCHA wa Simba, Steve Barker amesema anafurahishwa na namna ambavyo wachezaji wanavyoendelea kujitoa kuipambania timu, anaona ni ishara nzuri kwa ushindani wa Ligi Kuu Bara, baada ya kutolewa michuano ya CAF.
Barker amesema haikuwa lengo lao kuishia hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa, lakini hawana budi kukubaliana na uhalisia na kusisitiza hawana muda wa kupoteza na sasa wanaelekeza nguvu zao kupambania ubingwa wa ligi ya ndani.
“Najivunia viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji siku hadi siku, ligi ya ndani ni ngumu hivyo wanapocheza kwa kiwango cha juu itakuwa rahisi kupata pointi zitakazotusaidia kufikia malengo ya kuwania ubingwa,” amesema Barker na kuongeza;
“Natambua Simba haijachukua taji la ligi kwa muda mrefu, hivyo tuna kazi ya kuifanya ili kurejesha furaha kwa mashabiki na hilo nalisisitiza kwa wachezaji kupambana na kujua deni walilonalo kwa mashabiki wanaowasapoti.”
Ushindi wa bao 1-0 ulioipata Simba dhidi ya Stade Malien kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kocha Barker anauona umebeba heshima na kuwaongezea wachezaji morali ya kupambana zaidi hata kama haujawasaidia kuwavusha CAF. “Kwanza ushindi huo umetupa heshima kuonyesha Simba ni timu yenye ushindani, licha ya kutokuwa na nafasi katika michuano hiyo lakini bado tumeonyesha ushindani, ukiachana na hilo pia unawajengea wachezaji kujiamini na kutamani kufanya makubwa zaidi katika ligi ya ndani,” amesema kocha huyo.