Vifaa vya ujenzi Muheza vyaibwa, Waziri Mkuu afura

Dar es Salaam. Ni matumbo joto kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, baada ya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba kuipa kazi Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza baadhi ya watumishi kwa wizi wa vifaa vya ujenzi, akisema yeyote atakayebainika amepoteza kazi.

Dk Mwigulu amezitaka taasisi hizo mbili kukamilisha taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo na kumkabidhi kabla ya kuhitimisha ziara mkoani Tanga, akisisitiza yeyote atakayepatikana hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

“Atakayekuwa amehusika na kazi atakuwa amepoteza hapo hapo, hatuwezi tukawa tunalipa majizi halafu wanaitia hasara Serikali, iunganishwe na taarifa ya Handeni wale waliogandisha saruji, mambo ya ajabu kabisa,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Februari 16, 2026 mkoani Tanga baada ya kufika eneo la kuweka jiwe la msingi la jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na kupewa taarifa ya wizi wa nondo na baadhi ya vifaa vingine vya ujenzi.

Awali kabla ya kutoa maagizo, Waziri Mkuu baada ya kupokea taarifa ya upotevu wa vifaa vya ujenzi alimhoji Mkurugenzi wa Halmashauri, Dk Jumaa Mhina, ni hatua gani zimechukuliwa.

Mkurugenzi huyo alijibu akisema, “Nimepokea taarifa ya wizi wa nondo. Nilipopokea taarifa hiyo niliagiza taratibu za kisheria zifuatwe, kwa kuwa tuliajiri kampuni ya ulinzi ambayo tulikubaliana kwenye mkataba kwamba jambo lolote likitokea kwenye mradi kampuni hiyo italipa,” amesema.

Amesema kilichofanyika ni kuzuia malipo ya Sh14 milioni ya kampuni hiyo ya ulinzi na wakakubaliana kuendelea na shauri hadi walipane.

Mkurugenzi huyo amesema thamani ya nondo zilizoibiwa ni Sh20 milioni na tayari wamezuia Sh14 milioni za kampuni ya ulinzi na sasa wanafuatilia kiasi kilichobaki huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi.

Baada ya majibu hayo, Dk Mwigulu alikatiza akisema, “Hapa hakuna cha uchunguzi, mnachunguza nini? Vyuma vimeibiwa, tofali nataka waliohusika hatua zichukuliwe na hizi fedha zirudi, ujenzi uendelee,” amesema.

Kutokana na hilo, Dk Mwigulu ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia taarifa zote za kina na kumpelekea, na kuwabaini wanaohusika na mradi huo kama wanahusika na wizi wa vifaa hivyo.

“Mnaongea kirahisi kwamba zimepungua. Injinia, ingekuwa ni kwako zimepungua? Yaani tunasubirisha jengo kuisha kisha vifaa vinapotea kiurahisi hivyo,” amesema na kuongeza:

“Mnapeleka vifaa eneo la mradi kisha mnakuja kusema vimepotea kirahisi tu, nondo zimepotea, tofali zimepotea, ‘ring beam’ zimeibiwa na ninyi mpo tu,” amehoji.

Kutokana na ukinzani wa kauli, Waziri Mkuu ametaka ufafanuzi inawezekanaje vifaa hivyo kupotea wakati watumishi hao wanaingia kazini kila siku na wanalipwa mishahara.

“Kamilisha hiyo taarifa ya uchunguzi ili inisaidie kuamua. Haya mambo ya uzembe ya namna hii ndiyo ambayo hatutaki kuyaona yakiendelea,” amesema.

Akizungumzia vifaa vilivyopo stoo, Dk Mwigulu amehoji inawezekanaje vifaa kununuliwa, akitolea mfano viyoyozi na gypsum, na kuhifadhiwa wakati jengo lenyewe bado halijapauliwa.

“Ili siku ya kuvifunga mseme vimeoza. Mshauri elekezi yuko wapi? Mmeweka mshauri elekezi lakini hamsikilizi ushauri,” ameeleza.

Akihoji kamati ya upokeaji wa mizigo, Waziri Mkuu ametaka kufahamu nani aliyekabidhiwa vifaa vilivyopotea.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Raphael Mbwambo, amesema waliyemkabidhi ni mhandisi wa halmashauri.

Mhandisi huyo alipoulizwa na Waziri Mkuu vifaa hivyo alipeleka wapi, amejibu ni kamati ya mapokezi ilipokea vifaa baada ya kukagua na baadaye kuikabidhi kamati ya ujenzi ambayo nayo iliweka vifaa stoo.

Akaongeza kuwa, baada ya hapo hupewa mafundi pale wanapohitaji. Jibu hilo Waziri Mkuu alilikatiza akihoji wamewezaje kupoteza vifaa, mbona vingine havijapotea.

Mhandisi huyo akajibu akisema vifaa hivyo vilipotea baada ya mradi kusimama na ndiyo maana watu walifanya ukaguzi kabla ya kukabidhi kwa walinzi na fedha walipoingiziwa za kukagua vifaa ndipo walibaini upotevu huo.

Kwa majibu hayo, Dk Mwigulu alikatiza kwa mara nyingine akisema mradi kusimama ndiyo wamegawiana vifaa… Baada ya ukimya wa muda mfupi, Waziri Mkuu akatoa maagizo kwa mara nyingine kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga wahusika wote kwenye mradi huo wahojiwe.

“Naona tu mmefanya njama ya kugawana vifaa, mmefanya njama tu. Fuatilia mmoja mmoja na huyo wa ulinzi tujue mhusika, nipate taarifa kabla sijaondoka.

“Haya mambo yanaudhi. Rais anapambana kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ikamilike halafu watu ambao mpo kazini, mnalipwa mishahara, mmesomeshwa kwa kodi za Watanzania, mnazubaa zubaa vifaa vinapotea,” amesema.

Dk Mwigulu ameagiza kupata taarifa za uhusika wa wajumbe wote wa kamati katika upotevu wa vifaa hivyo.

Amesema wote waliopewa fedha siku moja na Halmashauri ya Muheza wamekamilisha miradi yao, lakini Muheza kulitokea kusuasua hadi fedha zikarejeshwa makao makuu huku wananchi wakiendelea kufanyishwa kazi na vifaa vikipotea.

Hali hiyo imemfanya Dk Mwigulu kumuelekeza Kamanda wa Polisi kufanyia kazi maagizo yake na kumpelekea taarifa, kwani hatakuwa na huruma na wezi.

Akizungumzia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Ngarani, Dk Mwigulu amesema mradi huo nao unasuasua; Sh58 milioni zimetolewa lakini mradi haukamiliki.