Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kupanua wigo wa ajira na kuweka mazingira bora ya uwekezaji, ndoto za maelfu ya vijana zimeendelea kugonga mwamba kufuatia kuibuka kwa mifumo ya ajira za mtandao inayowaliza kwa ahadi za utajiri wa haraka.
Changamoto ya ajira kwa vijana imegeuka mwanya unaotumiwa na watu wasio waaminifu kujinufaisha huku Serikali ikibaki kuwa nguzo muhimu kwa vijana wanaotafuta mustakabali bora.
Katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, kumeshuhudiwa ongezeko la kampuni zinazojitangaza kutoa fursa za ajira au biashara mtandao.
Hata hivyo, nyuma ya matangazo yenye mvuto na semina zenye hamasa, kuna masharti yanayowataka vijana kulipa ada ya kujiunga, kisha kuwashawishi wengine kufanya hivyo ili wapate gawio.
Mfumo huo kwa kiasi kikubwa hujengwa katika mtindo wa, “leta mwenzako,” huku mapato ya mshiriki yakitegemea idadi ya watu anaowaingiza.
Baadhi ya kampuni hutoa bidhaa za kuuza, lakini msingi mkuu wa kipato hubaki kuwa ni ada za wanachama wapya.
Lakini nyuma ya pazia la mafanikio yanayochorwa kwenye semina na mitandao ya kijamii, kuna simulizi nzito za maumivu, aibu na kukata tamaa.
Hata hivyo, wapo wachache wanaonufaika na aina hiyo ya ajira hususani wale waliotangulia na wenye mtandao mpana.
Kombo Moshi, mkazi wa Sawewe, Uyui mkoani Tabora, ni miongoni mwa vijana waliokumbwa na mkasa huo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Februari 14 2026, kwa njia ya simu, amesema rafiki yake waliyesoma pamoja alimshawishi kusafiri hadi Mwanza kwa madai ya kupata ajira yenye kipato kizuri.
“Rafiki yangu tuliyesoma pamoja alikuja likizo yake hapa kijijini kisha akaniambia zipo fursa za ajira Mwanza akinitaka niende, nilijiandaa nikasafiri mpaka huko lakini cha ajabu nilipofika hakuwa mtu wangu wa karibu tena, badala yake alinikutanisha na watu wengine,” amesema.
Amesema alipofika, hali ilikuwa tofauti na matarajio, badala ya kuanza kazi, alikutanishwa na watu waliomtaka kulipa Sh500,000 kama ada ya kujiunga na kuahidiwa mapato makubwa iwapo angefanikiwa kuingiza wanachama wapya.
“Nilishangaa kuona rafiki yangu hanipokei kama mtu wake wa karibu. Nilikutana na watu wengine tu waliokuwa wakisisitiza nichangie kwanza. Nikagundua hapa si ajira bali ni mzunguko wa fedha,” amesema.
Akiwa hana fedha za kulipia ada hiyo, Kombo alirejea Tabora akiwa amepoteza gharama za usafiri, chakula na malazi lakini pia usumbufu alioupata wa kupanga safari yenye matumaini ambayo hayakuwa.
Msemani Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 14, 2026 kuhusu suala hilo, ametoa wito kwa vijana kuchukua tahadhari ikiwamo kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali pale wanapotakiwa kutoa fedha ili kujiridhisha na uhalali wa ajira hizo.
“Vijana wachukue tahadhari dhidi ya utapeli unaofanywa mtandaoni. Kama ni suala la ajira wajiridhishe katika mamlaka za Serikali kabla ya kutoa fedha kwa yeyote.
“Ni muhimu kujiepusha na mambo ya kutaka kupata kwa njia za mkato mkato. Kama ni ajira, waulize katika Ofisi ya Kamishna wa Kazi, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya na katika halmashauri kama ajira hizo ni halali au ni matapeli,” amesema Msigwa.
Pia, amesema endapo mitandao ya matapeli itabainika taarifa zipelekwe polisi mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Vyuo vyageuka uwanja wa mawindo
Vijana wa vyuoni nao wamekuwa walengwa wakuu, baadhi wanasema wamepoteza fedha za kujikimu na mikopo ya elimu ya juu baada ya kushawishiwa kujiunga na kampuni hizo.
Kijana mmoja kutoka Tabora (jina limehifadhiwa) amesema alipigiwa simu aende Kahama kwa mahojiano ya kazi ya usimamizi wa mauzo, akiahidiwa tiketi na malazi.
“Hata hivyo, nilipofuatilia nikagundua waliotangulia waliishia kuombwa ada kubwa ya kujiunga na kupewa bidhaa za kuuza, huku wakitakiwa kuingiza wanachama wapya,” amesema.
Kwa mujibu wa vijana kadhaa, semina za hamasa huendeshwa kila siku, zikiahidi mafanikio ya haraka na maisha ya kifahari.
Wengine hukaa kimya kwa aibu baada ya kupoteza fedha, huku baadhi wakijaribu kuendeleza mfumo huo ili kuficha hasara zao.
Bidhaa zisizouzika, deni lisilolipika
Jijini Dar es Salaam, Asha Munuo naye alijikuta kwenye mtego kama huo, amesema alishawishiwa kujiunga na kampuni moja kwa kulipa Sh500,000, akiahidiwa kupewa bidhaa na mfumo wa kupata kamisheni.
“Nilidhani nimepata kazi. Lakini baada ya kulipa, nikapewa bidhaa ambazo hazikuwa na soko. Nikatakiwa kuingiza wanachama wapya ili nirejeshe pesa yangu,” amesema.
Asha amesema hakufanikiwa kuuza bidhaa wala kupata mtu wa kumshawishi kujiunga.
“Nilipogundua kuwa nimeingia kwenye utapeli, sikuona sababu ya kuumiza wengine ili nirejeshe pesa yangu. Nilibaki na hasara,” amesema.
Simulizi kama za Kombo na Asha zinaakisi hali halisi ya vijana wengi wanaokumbwa na mifumo hiyo. Wengi hukopa fedha ili kulipia ada ya kujiunga, wakiamini watarejesha kwa muda mfupi, lakini huishia kubeba madeni na msongo wa mawazo.
Athari hazijaishia kwa vijana pekee, wazazi nao wamejikuta wakiumia baada ya fedha walizotenga kwa ada au mahitaji muhimu kupotea.
Mzazi mmoja jijini Dar es Salaam (jina limehifadhiwa) amesema mwanaye alipoteza Sh800,000 za ada ya chuo baada ya kushawishiwa kujiunga na kampuni moja.
“Nilimwona mwanangu akinyong’onyea. Alikuwa na msongo wa mawazo. Nilipofuatilia ndipo nikagundua ametoa ada yake kwa ahadi za faida kubwa ambazo hazikutimia,” amesema mzazi huyo.
Kutokana na kuongezeka kwa malalamiko, Serikali katika baadhi ya maeneo imechukua hatua.
Februari 10, 2026, wilayani Tabora, vyombo vya ulinzi na usalama vilifanya operesheni ya kushtukiza na kukuta mamia ya vijana wakiwa wamekusanywa katika vituo vitatu kwenye kata za Mpela na Mtendeni kwa madai ya kupewa ajira na fursa za kibiashara.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella alisema vijana hao walitozwa hadi Sh4 milioni kila mmoja wakiahidiwa bonasi kupitia biashara ya mtandao.
Alisema baada ya kubaini hilo, aliwaelekeza wahusika wawarudishie fedha zao na kuifunga kampuni hiyo mara moja
“Na ukiwauliza wanasema wanapigiwa (simu) na vijana wenzao ambao wapo hapo, mbaya zaidi wanawekwa kwenye chumba kimoja vijana zaidi ya wanne na wanatozwa fedha mpaka milioni nne, tumeelekeza wahusika wawarudishie fedha zao,” alikemea mkuu huyo wa wilaya huku akiwataka vijana kuepuka ajira za kitapeli.
Katika tukio hilo, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Shani Mdamu alionya kuwa baadhi ya vijana walikutwa wakiuza bidhaa za afya ambazo hazijasajiliwa na mamlaka husika, jambo linaloweza kuwaweka kwenye hatia ya kisheria bila wao kujua.
Katika hatua nyingine, mwishoni mwa Januari mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano ilizindua mfumo wa kidijitali wa kuratibu, kupokea na kutatua malalamiko ya wafanyakazi ujulikanao kama E-Utatuzi.
Akizindua mfumo huo, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo alisema ni jukwaa litakalowawezesha wafanyakazi kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya mtandao na kuyafuatilia bila vikwazo vya kijiografia.
“Mfumo huu wa kisasa wa E-Utatuzi, unaowezesha kupokea na kushughulikia mashauri kwa njia ya mtandao utawawezesha wananchi kupata haki kwa urahisi, kwa wakati, na bila vikwazo vya kijiografia,” alisema Kisuo Januari 21, 2026.