Wawili washikiliwa tuhuma mauaji kiongozi wa CCM, Polisi yamsaka kinara wa ‘TFF’

Mbeya. Wakati watu wawili wakishikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Itumbi, wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, Elia Sambala, Jeshi la Polisi mkoani humo linamsaka mtu mmoja anayesambaa mitandaoni akijinasibu kuhusika na tukio hilo.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo mkoani humo leo Februari 16, 2026, imeeleza Sambala alikutwa shambani kwake akiwa amejeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye kali kichwani na watu wasiojulikana, tukio lililotokea Februari 11 mwaka huu.

Imeeleza kuwa Sambala alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya matibabu, ambapo uchunguzi wa awali ulibaini chanzo kuwa mgogoro wa masilahi.

Taarifa hiyo imefafanua kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi kupitia askari wa kuchunguza matukio ya mauaji, walianza msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili na ufuatiliaji zaidi unaendelea kwa wengine waliohusika.

“Chanzo cha tukio ni mgogoro wa masilahi wa eneo la uchimbaji madini ya dhahabu, ambapo mmoja wa wanafamilia ya Sambala alilikodisha kwa wawekezaji raia wa China kwa ajili ya shughuli za uchimbaji bila kushirikisha ndugu wengine,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imebainisha kupitia mtandao wa kijamii kunasambazwa picha mjongeo ikionesha mtu mmoja anayejinasibu kuhusika na tukio hilo la mauaji ya kiongozi huyo wa CCM.

Imeeleza Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu huyo anayejiita kiongozi wa Tanzania Freedom Fighter (TFF), kuacha kuongelea jambo ambalo ni tofauti na uhalisia na kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii kupotoshwa ukweli.

“Aache kutumia vibaya mitandao ya kijamii kupotosha ukweli na kuhamasisha uhalifu dhidi ya taasisi, viongozi na wananchi, upelelezi unaendelea na jitihada za kumtafuta mtu huyo ili kumkamata na hatua za kisheria zinaendelea,” imeeleza taarifa hiyo.