Mwanza. Alphonce Kaishozi, dereva wa daladala anayetuhumiwa kumgonga askari wa usalama barabarani, Tumsifu Kileo, na kusababisha kifo chake, amekamatwa baada ya kukimbia na kujificha mkoani Kagera.
Dereva huyo alikamatwa Februari 14, 2026, katika kijiji cha Rubare, Wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera, alikokuwa amekimbilia baada ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza iliyotolewa jana, Februari 16, 2026, jitihada za kumtafuta dereva huyo zilianza baada ya ajali iliyotokea Februari 10, 2026, saa 2:00 asubuhi, katika mzunguko wa Mwanza Hoteli katikati ya Jiji la Mwanza.
Ilielezwa kuwa siku ya tukio, Askari Tumsifu alikuwa amesimama pembezoni mwa barabara akisubiri kusimamisha magari, ili kupisha msafara wa mahabusu kutoka Gereza la Butimba, akiwa amevaa sare za Jeshi la Polisi.
Inaelezwa kuwa daladala aliyokuwa akiendesha Kaishozi, ikiwa na abiria, iliacha njia na kumgonga askari huyo pamoja na mtembea kwa miguu aliyekuwa karibu naye, ambaye ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya afya yake kuimarika.
Katika taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema baada ya ajali hiyo dereva alikimbia, msako ulianza mara moja.
“Tuliendelea na jitihada za kumsaka dereva aliyehusika na ajali hiyo, na tulifanikiwa kumkamata katika kijiji cha Rubare, Wilaya ya Bukoba Vijijini, mkoani Kagera,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa mtuhumiwa amerejeshwa mkoani Mwanza kwa ajili ya mahojiano, na amekiri kuhusika na ajali hiyo, huku taratibu za kisheria za kumfikisha mahakamani zikiendelea baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
“Sasa hivi tunapoongea ameshaletwa katika Mkoa wa Mwanza, anahojiwa na amekiri kuhusika na ile ajali, kwa hiyo, taratibu kwa mujibu wa sheria za kumfikisha mahakamani zinaendelea,” ameeleza Mutafungwa.
Kuhusu mmiliki wa daladala hiyo, Jeshi la Polisi limesema anaendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Nyamagana kwa mahojiano, kwa madai ya kumkabidhi gari dereva ambaye hakuwa ametunza kumbukumbu zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
“Anaendelea kushikiliwa kwa sababu yeye ni mmiliki wa gari na alikuwa amemkabidhi mtu gari ambaye hakuwa ametunza kumbukumbu zake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani,” amesema.
Mutafungwa amewakumbusha madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuacha uzembe unaoweza kusababisha majeraha au vifo kwa watumiaji wengine wa barabara, akisisitiza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuwa makini.