Dar es Salaam. Hatima ya uhalali wa maombi ya mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali itaamuliwa Machi 3, 2026.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Lissu amewasilisha maombi akiomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaiwa mwenye maslahi.
Wajibu wa maombi katika shauri hilo ni pamoja na wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake, kwa upande mmoja, na wadhamini wa Chadema pamoja na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.
Hata hivyo, wajibu wa maombi hayo, ambao ni wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake, wamemwekea pingamizi la awali ambalo limesikilizwa leo Jumanne, Februari 17, 2026, na pande zote zimetoa hoja zake kutetea misimamo yao.
Usikilizwaji wa pingamizi
Katika pingamizi hilo, wadai wanadai Lissu hajatimiza sifa za yeye binafsi kuingia katika shauri hilo, na kwamba kiapo chake kinachounga mkono hati ya maombi hayo kina kasoro za kisheria kwa kuwa hajathibitisha kuwa taarifa zilizomo amezipata wapi, kwani yuko gerezani tangu Aprili.
Lissu, akijibu hoja hizo, amedai ana maslahi stahiki kuingia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Amri ya I, Kanuni ya I–X (ya kwanza mpaka ya kumi) za Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai (CPC), zinazomruhusu mtu mwenye maslahi katika shauri kuomba kuingizwa.
Akifafanua maslahi hayo, Lissu amesema yeye ni mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2004 na kwamba kwa sasa ndiye mwenyekiti wa chama hicho, hivyo ana maslahi makubwa katika kesi hiyo kwa kuwa amri zitakazotolewa kama zilizoombwa zinamhusu moja kwa moja kama mwanachama.
Kuhusu hoja ya uthibitisho wa taarifa zilizomo katika kiapo chake alikozipata wakati yuko gerezani, amesema kuwa zinatokana na ufahamu wake binafsi.
Kwa mujibu wake, yote yanayoendelea katika kesi hiyo anayafahamu kwa kuyasoma tangu uamuzi wa Juni 10, 2025 wa zuio la chama kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapomalizika, ambao unapatikana kwa umma.
Amesema kama upande wa wadai una wasiwasi na ufahamu wake binafsi kuhusiana na taarifa hizo, wana haki ya kumuita katika kizimba cha ushahidi na kumhoji maswali ya dodoso, ili kujiridhisha na ufahamu wake kuhusiana na taarifa hizo kama anazifahamu au la.
Alipoulizwa na Jaji Mwanga kuwa amri hizo zikitolewa zinamgusa vipi, amesisitiza kuwa yeye kama mwanachama, amri yoyote itakayotolewa, kama ni kuzuia shughuli za chama au kama ni chama kudaiwa, naye kama mwanachama inamgusa moja kwa moja.
Kwa upande wake, Bodi ya Wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa chama, kupitia kiongozi wa jopo la mawakili wake, Dk Rugemeleza Nshala, wameunga mkono maombi na hoja za Lissu kuwa ana maslahi stahiki katika kesi hiyo.
Mahakama, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, imeahirisha shauri hilo mpaka Machi 3, 2026, itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo.
Uamuzi huo ndio utakaotoa uhalali wa maombi hayo ya Lissu kustahili kuwepo mahakamani na hivyo kusikilizwa, au kutokustahili na hivyo kutupiliwa mbali.
Ikiwa mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo, mahakama itaingia katika hatua ya kusikiliza maombi hayo ya Lissu katika ustahili wake na baadaye kuyatolea uamuzi.
Lakini kama mahakama itakubaliana na pingamizi hilo, maombi hayo ya Lissu yatatupiliwa mbali bila hata kuyasikiliza.
Katika kesi ya msingi, wadai wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo, wanaomba mahakama hiyo itamke wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, Marejeo ya mwaka 2019, na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Pia wanaiomba mahakama hiyo itamke ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile, wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika, pamoja na gharama za kesi.
Wadai hao wanawakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na wakili Shaban Marijan, anayesaidiana na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis.
Wadaiwa wanawakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na Dk Rugemeleza Nshala na Hekima Mwasipu pamoja na mawakili wengine kadhaa.