HATURUHUSU MIMBA ZA UTOTONI – MBUNGE JESCA MBOGO ATOA WITO MKALI MPWAPWA

………….

Na Carlos Claudio, Dodoma

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jesca Mbogo, amesema kuwa jamii haina budi kusimama kidete kupinga mimba za utotoni, akisisitiza kuwa mtoto wa miaka 15 hawezi na hapaswi kubeba jukumu la kuwa mzazi.

Mhe. Mbogo ametoa kauli hiyo katika siku ya pili ya ziara yake wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, mara baada ya kuchaguliwa, ambapo alizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Mazae pamoja na wananchi kuhusu umuhimu wa elimu, nidhamu na kujitambua.

“Haturuhusu mimba za utotoni. Mtu wa miaka 15 ana mtoto? Yaani mtoto anazaa mtoto? Hii haiwezekani na haikubaliki, watoto wangu,” alisisitiza Mbunge huyo.

Katika hotuba yake, Mhe. Mbogo aliwahimiza wanafunzi kuwa na wivu wa maendeleo na kujifunza kwa bidii ili kufikia ndoto zao. Alisema maendeleo yanahitaji juhudi binafsi na maamuzi sahihi.

“Tutamani maendeleo, tuwe na wivu wa maendeleo. Mwenzako anaposoma kwa bidii, usimuite msongo. Anajua anachokitaka kesho yake,” alisema.

Alibainisha kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio, akitoa mfano wa viongozi wakuu wa nchi. “Ukimuona Dkt. Samia Suluhu Hassan pale alipofika, ni kitabu. Ukiona mawaziri, wabunge, wahandisi na wanasheria, ni kitabu. Shule ni muhimu sana,” alieleza.

Mbunge huyo pia aliwataka wasichana kujivunia kusoma na kuzingatia nidhamu, akisema hakuna jambo linaloweza kufanikiwa bila nidhamu.

“Huwezi kufanya kitu kizuri popote pale pasipo nidhamu. Utafaulu vizuri ukiwa na nidhamu, walimu watakupenda, na kila kitu kitaenda sawa,” aliongeza.

Aidha, aliwakumbusha wanafunzi kuwa wazazi wao wanajitolea kwa hali na mali kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora, hivyo ni wajibu wao kuitunza fursa hiyo kwa bidii na maadili mema.

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Legal Women and Children Support, Ushindi Ndule, alisema taasisi hiyo imejikita katika kusaidia wanawake na watoto, ikiwemo kupambana na vitendo vya ukatili na mimba za utotoni.

“Tupo hapa kuwakumbusha kwamba wapo watu wanaopambania haki zenu na kuwalinda. Lakini nanyi mjilinde. Sisi tunaweza kupambana, lakini ni muhimu pia mjitambue na kujua nini ni cha haraka na nini kinaweza kusubiri,” alisema Ndule.

Alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kutofautisha kati ya maamuzi ya muda mfupi yanayoweza kuharibu maisha yao na malengo ya muda mrefu yanayoweza kuleta mafanikio.

Sambamba na hilo, Mhe. Mbogo aliipongeza Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) wilaya ya Mpwapwa kwa kuanza ujenzi wa nyumba ya mradi, ambao ni mpango wa kitaifa unaolenga kuhakikisha makatibu wa wilaya wanakuwa na makazi yao.

Kama sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo, Mbunge huyo alichangia mifuko 10 ya saruji pamoja na shilingi milioni moja taslimu, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine kusogeza mbele ujenzi huo hadi kukamilika.

Ziara ya Mhe. Mbogo mkoani Dodoma imeendelea kuibua hamasa kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa elimu, nidhamu na maamuzi sahihi ndiyo silaha ya kweli ya kupambana na changamoto za kijamii, ikiwemo mimba za utotoni.