Hii hapa sababu Ruto kuitisha mkutano wa dharura EAC

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, William Ruto, ameita mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Machi 7, 2026 jijini Arusha, kujadili mgogoro mkubwa wa kifedha unaotikisa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mkutano huo, utakaokuwa wa kwanza kufanyika baada ya zaidi ya mwaka mmoja, unatarajiwa kujadili mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha na hatua za kupunguza matumizi ndani ya EAC, baada ya nchi wanachama kushindwa kuwasilisha zaidi ya Dola 89.3 milioni  (Sh232.78 bilioni) zinazodaiwa na taasisi za jumuiya hiyo.

Rais Ruto, ambaye ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi wa EAC, anatarajia marais wote wanane wa nchi wanachama kushiriki, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu mgogoro huo uko mikononi mwa viongozi hao.

Waziri wa Kenya anayeshughulikia Masuala ya EAC, Mikoa Kame na Maendeleo ya Kanda, Beatrice Askul, amesema mkutano huo utashughulikia uhaba wa fedha, kupitisha mfumo mpya wa ufadhili uliopendekezwa na Baraza la Mawaziri la EAC, na kukubaliana namna ya kuratibu matumizi.

“Rais wa Kenya ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano wa wakuu wa nchi ana nia ya dhati kuona viongozi wanatoa msimamo wao kuhusu suala hili, kwa sababu wao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ndani ya EAC,” amesema Askul.

Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inaidai nchi wanachama dola 89,372,865, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiongoza kwa deni la dola milioni 27, ikifuatiwa na Burundi (dola milioni 22.7), Sudan Kusini (dola milioni 21.8), Somalia (dola milioni 10.5), Rwanda (dola milioni 5.2) na Uganda (dola milioni 1.1). Kenya na Tanzania pekee ndizo zilikuwa zimelipa kikamilifu mchango wa dola milioni saba kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Ukosefu huo wa fedha umeathiri kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa taasisi muhimu za EAC, zikiwamo Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mahakama ya Afrika Mashariki na taasisi nyingine za kikanda.

Karani wa EALA, Alex Obatre, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kutokana na ucheleweshaji wa michango ya nchi wanachama, hali iliyosababisha wabunge na watumishi kutolipwa mishahara tangu Novemba 2025.

“Ukosefu wa fedha umeathiri utekelezaji wa bajeti ya 2025/26, ikiwamo kucheleweshwa kwa mishahara, posho, shughuli za Bunge na majukumu ya kisheria,” alisema katika taarifa kwa wabunge na watumishi.

Mbunge wa Kenya katika EALA, David Sankok, amethibitisha kuwa wabunge hawajalipwa kwa muda mrefu na vikao vya Bunge hilo vimekwama.

Amezilaumu baadhi ya nchi wanachama kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa kifedha, akiitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa haijawahi kuchangia hata senti, huku Sudan Kusini ikiwa na deni kubwa.

Sankok amependekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa kiuchumi ndani ya EAC utakaoruhusu kila nchi kugharamia moja kwa moja mishahara na posho za wabunge wake, badala ya mfumo wa sasa unaotegemea michango ya pamoja ya jumuiya.

Mwishoni mwa juma, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Dk Abdullah Hasnuu Makame, naye aliwataka wakuu wa nchi kukutana kujadili namna ya kuziba nyufa ili kuinusuru jumuiya hiyo.

“Hili jambo inatakiwa wakuu wa nchi wakae wenyewe katika kikao chao, walitafakari, waangalie ni wapi kuna nyufa na wapi kuna matatizo, warekebishe. Chombo chetu, EAC, hakitakiwi kianguke, hakitakiwi kisimame.

“Tunakwenda na ile nadharia ya baiskeli, baiskeli haisimami kwa sababu ikisimama imeanguka. Baiskeli haina gia ya kurudi nyuma, inakwenda mbele. Basi, jumuiya yetu inatakiwa iende mbele,” amesema mbunge huyo.

Kwa sasa, wabunge 63 wa EALA hulipwa zaidi ya dola 7,000 kwa mwezi kwa mishahara na posho, huku malipo hayo yakitegemea fedha kutoka kwa nchi wanachama.