Unguja. Kwa mwaka 2026/27, Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inakadiriwa kufikia Sh8.217 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh1.235 trilioni.
Ongezeko hilo ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.69 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26 ya Sh6.982 trilioni.
Makadirio hayo yanatokana na mageuzi ya sera na mikakati mbalimbali ya upatikanaji wa mapato ambayo Serikali inapanga kutekeleza kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Februari 17, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Malik Akil wakati akiwasilisha mpango wa Taifa na mwelekeo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, matarajio ya kiwango cha utegemezi wa Bajeti ya SMZ ni kupungua kutoka asilimia 4.9 iliyoripotiwa mwaka 2025/26 hadi kufikia asilimia 4.5 kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Kupungua huko kunatokana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato na mikopo ya ndani.
Dk Malik amesema katika mpango huo, mapato ya ndani yanakadiriwa kufikia Sh6.613 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh1.076 trilioni sawa na ukuaji wa asilimia 19.4 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka 2025/26 ya Sh5.537 trilioni.
Mapato ya ndani yanajumuisha mapato ya kodi na yasiyokuwa ya kodi, mikopo ya ndani na mapato ya mamlaka za Serikali za mitaa na mapato ya taasisi zinazojitegemea.
“Katika mchanganuo huo, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) itakusanya Sh1.684 trilioni. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Zanzibar Sh1.128 trilioni na mapato ya kodi za wafanyakazi kutoka SMT (Paye) walioko Zanzibar ni Sh21 bilioni,” amesema Dk Malik.
Katika makadirio hayo, amesema mapato yasiyokuwa ya kodi yatachangia Sh350.664 bilioni, mikopo ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni Sh2.9 trilioni, mapato ya mamlaka za Serikali za mitaa Sh23.915 bilioni na mapato ya taasisi zinazojitegemea za Serikali Sh505.272 bilioni.
Katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka kwa mwaka 2026/27 amesema Serikali imeandaa mikakati mahsusi ikiwa ni kuongeza kiwango cha fedha kuweka katika mfuko wa kuhudumia madeni ili kuongeza hadhi ya kukopesheka na kuboresha mifumo ya ukusanyaji na kuhakikisha hakuna mapato yatakayokusanywa nje ya mifumo.
Katika mapato yatokanayo na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo yanakadiriwa kufika Sh1.604 trilioni ikiwamo mikopo ya Sh1.062 trilioni na misaada Sh391.750 bilioni, Sh560 bilioni zinazotokana na Mfuko wa Pamoja wa Washirika wa Maendeleo na Sh150 bilioni ni misaada ya kibajeti.
Katika matumizi ya Sh8.217 trilioni, matumizi ya kazi za kawaida inakadiriwa kuwa Sh2.923 trilioni sawa na asilimia 35.58 ya makadirio ya bajeti yote inayojumuisha Sh1.003 trilioni ikiwa ni matumizi ya mshahara.
“Sh698.871 bilioni zitatumika kuendeshea ofisi, Sh701.012 bilioni, matumizi ya huduma za Mfuko Mkuu wa Serikali, Sh14.700 bilioni matumizi ya serikali za mitaa kwa mapato ya ndani,” amesema Dk Malik.
Kwa matumizi ya kazi za maendeleo, amesema Sh5.294 trilioni zinakadiriwa kutumika kwa utekelezaji wa mpango wa maendeleo sawa na asilimia 64.42 ya bajeti yote, zikiwamo Sh2.705 trilioni za matumizi ya miradi mipya ya kimkakati inayoendelea kutoka serikalini na Sh600 bilioni kwa ajili ya mfuko wa kugharamia madeni na Sh542.780 bilioni kwa ajili ya miradi mingine.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea na jukumu lake la msingi la utafutaji wa rasilimali fedha ili kugharamia mpango mkakati wa Serikali hususan miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kuhakikisha uhimilivu wa deni la Serikali unaendelea kwa kiwango kinachokubalika.
Dk Malik ametaja miongoni mwa hatua ambazo Serikali inakusudia kuziwekea mikakati ni pamoja na usimamizi wa mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, kurahisisha taratibu za kodi, kutoa elimu kwa walipa kodi na kuimarisha ukaguzi wa mapato.
“Kuongeza mapato yasiyo ya kodi kwa kuimarisha usimamizi wa mali za Serikali na ufanisi wa mashirika ya umma ili kuongeza wigo wa mapato ya Serikali yanayotokana na gawio na mchango kutoka kwa taasisi zinazojitegemea,” amesema Dk Malik.
Pia, amesema kukuza sekta za uzalishaji ikiwamo, utalii, kilimo, uvuvi, biashara ndogo na za kati (SMEs) na uchumi wa buluu, ili kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani wa kugharamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutegemeana.
Dk Malik amesema SMZ tayari imeshapata uzoefu na kujifunza changamoto na mbinu za upatikanaji wa mikopo, hivyo tutahakikisha makusanyo ya ndani yanaongezeka ili kutuwezesha kuweka akiba ya kutosha katika Mfuko wa Kugharamia Madeni kwa lengo la kuwa na mpango na mkakati endelevu wa kurejesha madeni hayo bila ya kuathiri shughuli nyingine za Serikali.
Akiwasilisha Mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Suleima Ameir amesema Serikali inatakiwa kutoa elimu kwa taasisi na kushirikisha sekta binafsi hasa katika uanzishaji wa kodi mpya na kuweka usawa wa kodi katika maeneo mbalimbali.
Ali amesema kamati inaishauri Serikali kukamilisha mpango mpya wa maendeleo kwa haraka ili kuakisi mipango na bajeti iliyopangwa kutekelezwa mwaka 2026/27.
Amesema ili kufikia ufanisi katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo, kamati inaishauri Serikali kuipa kipaumbele miradi inayoendelea kutekelezwa ikamilike kabla ya kuanza kutekelezwa mipya kwa kuwa, kutaepusha kuongezeka kwa gharama.
Kwa upande wa uimarishaji wa mazingira ya uwekezaji, Ali amesema kamati inaishauri Serikali iendelee kutekeleza mikakati ya kuimarisha mazingira ya wawekezaji kwa kuondoa muingiliano wa majukumu kwa taasisi za udhibiti katika utoaji wa vibali na leseni pamoja na kuondoa tozo sumbufu kama vile leseni za maofisa rasilimali watu katika hoteli za kitalii na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi.
“Ili kufikia matarajio ya maendeleo endelevu, kamati inaisisitiza Serikali kwamba, maendeleo endelevu ya nchi yoyote hutokana na kuimarika kwa uzalishaji wa ndani hususan katika sekta zinazoajiri wananchi wengi kama vile sekta ya kilimo, uvuvi na viwanda,” amesema Ali.
“Hivyo, kamati inaishauri Serikali iweke mikakati mahsusi ya kuimarisha uzalishaji wa viwandani na kuimarisha sekta za kilimo na uvuvi ili kufikia maendeleo endelevu ya nchi na mwananchi mmoja mmoja.”