Jamal afunguka mziki Dar City ulivyompaisha

SUPASTAA wa timu ya kikapu ya Dar City, Jamal Ally amezungumzia kwa mara ya kwanza ubora wake katika kikosi hicho kufuatia vaibu ambalo amekuwa akilionyesha katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kiasi cha mashabiki kuanza kumuona kuwa ni nyota mpya ajaye.

Lakini, katikati ya mazungumzo yake na Mwanaspoti, Jamal amedai kwamba mziki aliokutana nao Dar City mara tu baada ya kumwaga wino misimu miwili iliyopita si mchezo, na kwamba mchezaji yeyote akitua katika kikosi hicho na kujitambua ni lazima ataimbwa na mashabiki kutokana na ubora wake.

Alisema kiwango chake tangu alipotua kwa mabingwa hao wa BDL kimekuwa kikiongezeka siku hadi siku kutokana na kuzungukwa na mastaa wa maana kikosini.

Nyota huyo aliyewahi kuichezea Savio katika BDL miaka ya nyuma, alisema kuongezeka huko kwa ubora pia kunatokana na mafunzo bora ya kikapu yanayotolewa katika timu hiyo ambayo msimu huu ilishiriki michuano ya kikapu ya kufuzu fainali za Afrika.

Aliongeza kuwa jambo lingine ni ushindani uliopo katika kikosi hicho kutoka kwa mastaa kimataifa wenye viwango vikubwa anaofanya nao mazoezi kila uchao.

“Kwa kweli kuna vitu sikuwa navyo vya uchezaji nikiwa nje ya timu ya Dar City, nimevikuta nikiwa ndani ya timu hii iliyonifanya nionekane fiti,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya BDL msimu ujao, alisema amekuwa akipambana gym kujiweka vizuri kimwili akitarajia kwamba yatakuwa moto zaidi.


“Nikiwa katika gym nafanya mazoezi kuanzia saa moja asubuhi hadi mbili na baada ya hapo nafanya mazoezi nikiwa peke yangu ya kufunga katika Uwanja wa Don Bosco, Oysterbay,” alisema.

Jamal, anayecheza nafasi ya namba 2 maarufu kama shooting guard, alisema nyakati za jioni amekuwa akifanya mazoezi ya pamoja na wenzake Dar City katika uwanja huohuo.

Alisema ligi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi yanayoendelea katika kambi za timu shiriki.

“Ndiyo maana wachezaji wengi wameanza mazoezi mapema… ni kutokana na ugumu wa ligi utakaokuwepo mwaka huu,” alisema..

Kuhusu wachezaji wa kigeni katika ligi hiyo Jamal alisema wameongeza ushindani uliofanya wazawa wajifunze mbinu mpya za kiuchezaji sambamba na namna ya kukabiliana na ushindani wa namba vikosini.

“Wachezaji wa kigeni wametuzidi. Tuchofanya kwa sasa sisi wazawa tunachukua mbinu za uchezaji kupitia kwao,” alisema.

Akizungumzia mashindano ya Road to BAL Elite 16 yaliyofanyika mwaka jana nchini Kenya, alisema amejifunza mbinu mbalimbali za uchezaji kutoka kwa wachezaji wa kimataifa aliowaona wakiwa na timu zao katika kinyang’anyiro hicho kilicholenga kufuzu fainali za Afrika.

“Nimejifunza pia mbinu za uchezaji na maisha ya nje ya uwanja ambayo mchezaji anapaswa kuishi nayo.”