Kamati ya Bunge ya Miundombinu Yaipongeza TCAA kwa Kuimarisha Usimamizi na Maendeleo ya Sekta ya Usafiri wa Anga

 


Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imetembelewa na Kamati ya Bunge ya Miundombunu na kupongezwa kwa jitihada zake za kuisimamia na kuiendeleza sekta ya usafiri wa anga nchini.

Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu ilifanya ziara hiyo mnamo Februari 16, 2026 katika Makao Makuu ya TCAA yaliyopo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo iliongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mutasingwa, kwa niaba ya Mwenyekiti Selemani Kakoso.

Ziara hiyo ya kikazi ilikuwa na lengo la kujua shughuli zinazofanywa na Mamlaka katika utekelezaji wa majukumu yake ya ki udhibiti .

Kamati hiyo iliihimiza TCAA kuendelea kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza Mradi wa ujenzi wa Majengo ya Kisasa ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubalika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile aliyeongozana na kamati hiyo, alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga kupitia ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya anga pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi. Alisema jitihada hizo zinategemea nguvu kazi yenye ujuzi mkubwa, na kwamba CATC, kwa kushirikiana na TCAA, ni nguzo muhimu katika kuzalisha wataalamu watakaoiwezesha sekta ya usafiri wa anga kukua kwa kasi na kwa usalama.

Kwa upande wa TCAA kamati hiyo ilipokewa na Mwenyekiti wa Bodi wa TCAA Dkt. Hamisi Mwinyimvua na kisha kupokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mutasingwa akizungumza akizungumza na menejimenti na watumishi wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Makao Makuu ya TCAA yaliyopo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile akizungumza kuhusu Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Miundombunu aliyotembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) yaliyopo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi wa TCAA Dkt. Hamisi Mwinyimvua akizungumza jambo wakatiwa  ziara ya Kamati ya Bunge ya Miundombunu aliyotembelea Makao Makuu ya TCAA.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi akitoa taarifa kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo kwa  Kamati ya Bunge ya Miundombunu ilipotembelea Makao Makuu ya TCAA yaliyopo Banana-Ukonga jijini Dar Es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Mtumwa Khatib Ameir akitoa neno la shukrani kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea ofisi za TCAA zilizopo Banana-Ukonga. jijini Dar es Salaam.