MASHABIKI wa Simba bado hawaamini kilichoitokea timu hiyo msimu huu katika michuanoi y kimataifa, lakini nahodha wa kikosi hicho, Shomari Kapombe amewatuliza huku akitoa msimamo kwa ajili ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Simba yenye rekodi za kuvutia katika michuano ya CAF, msimu huu kwa mara ya kwanza imeshindwa kwenda robo fainali kutokea makundi tangu ilipotinga hatua hiyo misimu minane iliyopita (2018-2019) hadi msimu huu ikimaliza mkiani mwa Kundi D la Ligi y Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Kapombe mmoja ya wachezaji waandamizi wa timu hiyo, amesema licha ya Simba kushindwa kuendeleza ubora katika anga la kimataifa, anaamini wana nafasi ya kurudi katika michuano hiyo na kutwaa taji la Ligi Kuu Bara ambalo wamelipoteza misimu minne mfululizo.
Mara ya mwisho kwa Simba kubeba ubingwa wa michuano hiyo mikubwa miwili nchini ilikuwa 2020-2021, kabla ya Yanga ‘kujimilikisha’ kwa misimu minne mfululizo.
Lakinim akizungumza na Mwanaspoti, Kapombe amesema wamekubali hawakuwa bora katika michuano ya kimataifa na kuwaomba mashabiki wao kuendelea kuwa pamoja nao kipindi hiki kwani hata wao wanapitia magumu.
Amesema walishazoea kuona ubora, lakini kwa msimu huu wameyumba wakiahidi kurudi imara katika Ligi Kuu Bara na kuwekeza juhudi zote ili kuweza kutwaa mataji yaliyo mbele yao kuwapa furaha Wanasimba.
“Huu sio wakati wa kulaumiana, ni wakati wa kushikamana kuanzia viongozi wa juu hadi mashabiki, lengo letu liwe moja. Hawapaswi kutukatia tamaa au kuisusa timu bado tuna nafasi ya kurudi na kusawazisha makosa, hakuna kinachoshindikana licha ya matokeo kuumiza,” amesema Kapombe.
“Nawaomba viongozi kuongeza umoja na kutuliza amani ya klabu ili tuwe wamoja kupambania timu ambayo licha ya yote bado inaendelea kuwa na rekodi nzuri ambayo bado haijafikiwa na timu yoyote nchini kimataifa. Hatutaki kuipoteza zaidi turudi na kuandika rekodi mpya kwa kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
Kapombe amesema malengo kimataifa ni makubwa wanapoishia njiani na kushindwa kufikia hata rekodi yao wanaumia kama wachezaji, hivyo wanawaelewa mashabiki na wanajua maumivu waliyo nayo pia.
“Ahadi ni kupambana zaidi ya hapa tulipo sasa. Hakuna kinachoshindikana timu tayari imeunganika wachezaji tuliopo tuna malengo sawa. Matarajio ni makubwa, tunahamia kwenye ligi kwa malengo makubwa baada ya kupoteza Ligi ya Mabingwa.”
Akizungumzia kikosi kwa ujumla, Kapombe amesema baada ya mabadiliko ya mara kwa mara ya wachezaji wengine wakitoka na wengine kuingia, sasa anaona timu imepata muunganiko mzuri na nyota waliopo wengi ni bora na wana malengo makubwa.
“Hili linatoa picha ni namna gani tutakuwa na njia rahisi kufikia malengo ya klabu, “amesema. “Timu bora inakuwa na umoja kuanzia ngazi ya mashabiki hadi viongozi, hivyo tunaomba na tunatambua makosa yametokea, tumeteleza ndio matokeo. Sasa tunarudi kutafuta nafasi nyingine, tuwe wamoja tufikie malengo.”
Simba inatarajiwa kushuka uwanjani leo Jumanne kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Greenland. Msimu uliopita Simba ilitolewa nusu fainali ya michuano hiyo na Singida Black Stars.