Kero nne kutikisa ziara ya Mwigulu Kilimanjaro

Moshi. Wakati Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akitarajiwa kuanza ziara ya siku nne mkoani Kilimanjaro kuanzia kesho, Februari 18, baadhi ya wananchi wa mkoa huo wameeleza matarajio yao juu ya masuala wanayotaka yapatiwe kipaumbele.

Wananchi hao wamesema wanatarajia ziara hiyo itasaidia kushughulikia migogoro ya ardhi, matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na vitendo vingine vya ukatili vinavyoathiri ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wao, ujio wa Waziri Mkuu unatoa fursa kwa Serikali kusikiliza kero zao moja kwa moja na kuzitafutia suluhisho la kudumu.

Wanaamini ziara hiyo inaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko chanya katika utatuzi wa changamoto zinazoendelea kwa muda mrefu.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa mkoa huo wamesema kumekuwa na changamoto sugu, hususan migogoro ya ardhi, ambayo imewaathiri wananchi wengi.

Wamedai kuwa baadhi ya watu wamevunjiwa makazi yao na kulazimika kuishi katika mazingira magumu baada ya kukosa haki zao.

Mkazi wa Wilaya ya Moshi, Anastazia Kavishe, amedai kuwa hivi karibuni bibi mwenye umri wa miaka 89, Sesilia Martin, mkazi wa Longuo, alivunjiwa nyumba yake katika eneo aliloishi tangu mwaka 1961 kwa madai ya kuvamia ardhi hiyo.

Amesema suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi, jambo linaloongeza hofu na maumivu kwa wananchi wengine wanaokabiliwa na migogoro kama hiyo.

“Jiulize huyu bibi ameishi kwenye hii eneo  tangu mwaka 1961, amezikwa mume na watoto, halafu leo hii mtu anakuja au chama fulani kinasema huyu bibi kavamia hili eneo anatakiwa kuondoka, aende wapi na uzee huu,” amesema mwananchi huyo.

Amesema: “Tunakuomba Waziri Mkuu unapokuja Kilimanjaro aanze na hawa viongozi wazembe ambao wapo na wanashindwa kutatua matatizo ya watu, huyu bibi zimeisha siku 270 mvua ni yake jua ni lake hana mahali pakwenda. Huyu bibi hana anayemsaidia, Waziri msaidie huyu bibi,” amesema.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, mmoja wa wananchi wa kata ya Mbokomu, Ester Kiwia,  amesema kata hiyo imekuwa na changamoto kubwa ya maji hali ambayo inawalazimu kuyanunua kwa gharama kubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akizungumzia ziara ya siku nne ya ujio wa Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, mkoani humo.



“Sisi huku kwetu kuona maji ni kama dhahabu, sio kiangazi au mvua zikinyesha, tunamwomba Waziri Mkuu atusaidie kwa hili, tunateseka hapa Mbokomu,” amesema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, Agness Tesha amesema wananchi wana matarajio makubwa na ujio wake na kwamba wanaamini atawasikiliza na kutatua kero zao ambapo baadhi ya mamlaka husika zimeshindwa kuzipatia majibu.

“Tunatamani kumuona Mwigulu, yapo matatizo makubwa ambayo wananchi tunayo na yameshindwa kupatiwa ufumbuzi, tunaamini kuja kwake ni kupona kwetu,” amesema mwananchi huyo.

Mkazi mwingine, wa Mkoa huo, Peter Kessy, amesema ujio wake huenda ukazaa matunda kwani wapo baadhi ya wananchi wa mkoa huo ambao wamekuwa na kero mbalimbali, lakini wakati mwingine wanashindwa kuzifikisha katika mamlaka husika kutokana na baadhi yao kushindwa kuonana ana kwa ana na wahusika.

“Wakati mwingine ukiwa na changamoto yako unaweza kwenda kwenye ofisi husika, unakaa kwa muda mrefu bila kusikilizwa na hata mwisho wa siku kile kilichokupeleka akarudi nyumbani ukiwa na mawazo zaidi, kwa sababu ya kero zilizopo kwenye ofisi za Serikali,” amesema mwananchi huyo.

RC azungumzia ujio wa Waziri Mkuu

Akizungumzia ujio wa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kiongozi huyo atafanya ziara ya kikazi ya siku nne mkoani humo kuanzia Februari 18.

Amesema katika ziara hiyo, Waziri Mkuu atatembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

“Waziri Mkuu ataanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani hapa ambapo ataingia kesho Februari 18 na kumaliza Februari 21. Tutampokea akitokea mkoani Tanga na kuanza ziara yake rasmi Jimbo la Same Mashariki, katika kata ya Ndungu,” amesema RC Babu.

RC Babu amesema akiwa Same Mashariki, atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kata ya Ndungu na baadaye atapewa taarifa rasmi ya maendelezo ya barabara Same-Mkomazi ambayo imeanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikianza na kilomita 36.

Amesema akiwa  Wilaya ya Mwanga, Waziri Mkuu huyo ataweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya hiyo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazolikabili wananchi wa Wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema,  atakwenda Wilaya ya Rombo kukagua barabara ya ‘lower road’ inayojengwa kilomita 52 kwa kiwango cha lami, kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Amali ya Mwalimu Steven Memorial na kutembelea kituo cha Forodha cha Tarakea.

Amesema akiwa Wilaya ya Moshi, Waziri Mkuu atatembelea barabara ya Mabogini, Spencon-Mabogini-Kahe- Chekereni barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya Sh7 bilioni pamoja na stendi ya kimataifa ya mabasi ya Ngangamfumuni iliyopo Manispaa ya Moshi.

Aidha, amesema katika Wilaya za Hai na Siha atakagua miradi ya shule,  barabara pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la utawala katika Hospitali ya Kibong’oto.