Madereva Kiwanda cha A- One wagoma wakidai nyongeza ya mshahara

Dar es Salaam. Baadhi ya madereva wa Kiwanda cha A-One Product & Bottlers Ltd kilichopo Kiwalani jijini Dar es Salaam, wamegoma kwa saa kadhaa wakishinikiza nyongeza ya mshahara.

Madereva hao wamedai kuwa, kiwango cha Sh200,000 kwa mwezi wanacholipwa kwa sasa hakikidhi mahitaji yao kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Pia, wameitaka menejimenti kuoanisha mishahara yao na mwongozo mpya wa kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi uliotolewa na Serikali kwa sekta ya usafirishaji, badala ya kuwatambua chini ya sekta ya viwanda.

Kwa mujibu wa Labour Institutions (Minimum Wage for Private Sector) Order, 2025, viwango vipya vya mshahara tayari vimeanza kutumika.

Aidha, Employment and Labour Relations Act inaelekeza kuwa, mishahara hupangwa kulingana na aina ya kazi na sekta husika.

Katika mgawanyo huo, madereva wa malori ya safari za kimataifa hulipwa kati ya Sh480,000 na Sh550,000, huku wa mabasi ya mikoani wakitakiwa kulipwa Sh350,000 hadi Sh450,000.

Madereva wa magari ya biashara na viwandani hulipwa Sh150,000 hadi Sh250,000.

Leo Februari 17, 2025, mwandishi wa Mwananchi aliyefika kiwandani hapo majira ya saa 7:05 mchana alikuta madereva wakiwa wamekusanyika nje ya geti, huku shughuli za uzalishaji na usafirishaji zikisimama kwa muda.

Mmoja wa madereva hao, Yusuph Hassan amesema wamelazimika kugoma baada ya malalamiko yao ya awali kutopatiwa ufumbuzi.

“Dereva anakutana na hatari nyingi barabarani, lakini mshahara wake ni sawa na kazi nyingine zisizo na mazingira hayo. Hii haiko sawa,” amesema.

Dereva mwingine, Salum Mtilu, amesema wamejaribu kufanya vikao bila mafanikio na sasa wanataka kusikilizwa.

“Sh200,000 haitoshi. Tunaomba angalau ifikie Sh300,000 ili tuweze kujikimu,” amesema.

Naibu Meneja wa Rasilimali Watu wa kiwanda hicho,  Neema Kitinya amesema kiwanda kimetekeleza kima cha chini cha Sh200,000 kwa sekta ya viwanda na hakuna anayelipwa chini ya kiwango hicho.

Amefafanua kuwa, madereva hao wako chini ya sekta ya viwanda kwa kuwa mwajiri wao ni kampuni ya uzalishaji.

Hata hivyo, amesema kampuni iko tayari kufanya majadiliano kupitia utaratibu wa mapitio ya mishahara unaofanyika Agosti kila mwaka.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi kiwandani hapo, Ramadhani Ponanga amesema madereva wanaolipwa Sh200,000 ni wale wenye ajira ya chini ya miezi sita.

Amesema kiwango hicho hakijumuishi malipo ya saa za ziada (overtime), na kwamba wapo madereva wanaopokea hadi zaidi ya Sh400,000 kulingana na muda wa utumishi na makubaliano ya ajira.

“Malipo yanatofautiana kwa kuzingatia uzoefu na makubaliano ya awali kati ya mwajiri na mwajiriwa,” amesema Ponanga, akibainisha kuwa chama kinaendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi ili wauelewe vyema mwongozo wa kima cha chini cha mshahara.

Mwanasheria wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kamanda Fundikira amesema mgawanyo wa kima cha chini cha mshahara huzingatia sekta ambayo mwajiri anaiendesha.

Amesema ikiwa mfanyakazi yupo katika kampuni ya viwanda, basi atalipwa kwa kuzingatia mwongozo wa sekta hiyo, bila kujali fani yake.