Mbinu sita zinazotumiwa kukwepa kodi Tanzania

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeelezea maeneo yanayotumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi nchini ikiwemo katika utoaji wa risiti, ulipaji wa mishahara, kodi na uagizaji wa bidhaa.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Februari 17, 2026 katika uzinduzi wa kituo cha kodi cha TRA, Masaki, jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa kusogeza huduma karibu na walipakodi unaofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Kamishna wa Operesheni, Charles Mabula amesema katika sekta ya ujenzi wafanyabiashara wamebuni mbinu ya kuunda kampuni hewa ili kuficha ukubwa halisi wa biashara zao.

Amesema baadhi huanzisha kampuni moja na baada ya muda huifunga, kisha kufungua nyingine, huku kampuni ya tatu ikitumika kufanya miamala ya uongo.

Kampuni hizi hutengeneza risiti feki na nyaraka za mauzo na manunuzi bandia, mfano mauzo hewa ya Sh1 bilioni na manunuzi hewa Sh900 milioni njia hii inawekwa kusaidia kupunguza kiwango cha kodi kinachotakiwa kulipwa, jambo linaloikosesha Serikali mapato kila mwaka.

Katika biashara za usafirishaji amesema ukwepaji kodi umechukua sura nyingine kwani wapo wafanyabiashara wanaodai kusafirisha bidhaa kwenda nchi jirani kama Burundi, lakini hazifiki huko.

Badala yake, hutumia vitambulisho feki vya watu au kampuni za nje, kubadilisha taarifa za mizigo njiani na hata kuondoa stika za usafirishaji kwenye magari ili kuficha uhalisia wa safari.

“Hatua hizi hupelekea bidhaa kubaki nchini na kuuzwa bila kulipiwa ushuru wa forodha, hali inayopunguza mapato ya Serikali na kudhoofisha biashara halali,” amesema.

Amesema pia baadhi ya kampuni za nje zimetajwa kutumika kama kampuni hewa kwa niaba ya zile za ndani.

Kampuni hizo husajiliwa kwa majina bandia na kutumika kama wapokeaji wa mizigo inayoelezwa kuwa inaenda nje ya nchi hata hivyo mizigo hiyo hubaki nchini:“Hatua hiyo pia hutumika kuficha wamiliki halisi na kukwepa kodi za bidhaa zinazodaiwa kupelekwa nje.”

Eneo lingine ni uagizaji wa bidhaa kupitia kampuni bandia nao umeendelea kuwa njia nyingine ya ukwepaji kodi, kwani baadhi ya wafanyabiashara huunda kampuni hewa kuagiza bidhaa kutoka nje na zinapowasili nchini wao wenyewe huzipokea nje ya mfumo rasmi wa TRA.

“Bidhaa hizo huuzwa bila kutoa risiti na Serikali inapoteza kodi ya mapato na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Sekta za bidhaa za ujenzi zimekuwa zikihusishwa zaidi na mbinu hii,” amesema.

“Ukwepaji wa kodi pia umejitokeza katika ajira za wageni nchini. Baadhi ya kampuni hulipa wafanyakazi wa kigeni mishahara miwili mmoja mdogo unaolipwa nchini kwa matumizi ya kawaida, na mwingine mkubwa unaolipwa moja kwa moja kutoka nje ya nchi.

Njia hii imekuwa ikitumiwa kuzuia kukatwa kwa kodi ya mapato (PAYE) kwenye sehemu kubwa ya mshahara, hali inayosababisha Serikali kukosa mapato halali kutoka kwa wataalamu wa kigeni wanaofanya kazi nchini,” amesema.

Mabula amesema wafanyabiashara wengine wamekuwa wakificha ukubwa halisi wa biashara zao kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu mauzo na manunuzi.

“Wengine hawatoi risiti kwa wateja wa mwisho, huku wakifanya miamala ya kifamilia au kirafiki isiyo rasmi ili kuonekana wanaendesha biashara ndogo. Njia hii imekuwa ikitumiwa sana katika biashara za rejareja, ambapo ni vigumu kwa mamlaka kugundua mapato halisi yanayopatikana,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara kuacha kutumia njia zozote za ukwepaji kodi na kulipa kwa hiari ili kuwezesha biashara kufanyika kwa usawa.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema kufunguliwa kwa tawi hilo kunalenga kuhakikisha kunakuwa na ulipaji wa kodi kwa usawa kwa kuondoa wale wanaokwepa kwa visingizio mbalimbali.

 “Kufunguliwa kwa tawi hili ni moja ya kutanua wigo wa walipakodi ambao hautaongezeka kwa kuongeza kiwango cha kodi kinacholipwa bali kwa kuongeza idadi ya watu wanaopaswa kulipa kodi,” amesema.

Kwa upande wake, Victoria Soka ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) amesema kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni moja ya hatua ya kusogeza huduma karibu na walipakodi na kuondoa ulazima wa wao kwenda ofisi ya Kinondoni.

Pia alitumia nafasi hiyo kushukuru juu ya mfumo wa IDRAS ambao amesema kwa sasa unafanya vizuri huku wakiendelea kujifunza juu ya changamoto zilizopo, lakini wamekuwa wakishauriana na TRA na kutoa mrejesho.

 “Lakini mpaka sasa tunaona mfumo ni mzuri na kwa kweli pia ule muda wa kwenda TRA sasa tunafanyia maofisini ukiwa mbali ukiwa karibu hivyo tunawashukuru kwa jinsi ambavyo mnasaidia katika kuhakikisha watu wanalipa kodi kwa urahisi,” amesema.