Chama Cha Mapinduzi kimesema kukamilika kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria unakwenda kuwa mkombozi kwa wananchi wa Urambo, Sikonge na Kaliua.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa Kenani Kihongosi amesema hayo wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaogharimu kiasi cha Sh bilioni 143.
“Niseme kwa dhati Urambo ilikuwa na changamoto kubwa ya maji, maji yalikuwa ni shida lakini serikali ya CCM iliahidi kwenye ilani yake kwamba itakwenda kujenga mtandao mkubwa wa maji ambao ni gridi ya maji ya taifa kama ambavyo tulivyo na gridi ya umeme kwa hiyo kila kijiji kitapata maji safi na salama,”alisema.
Kadhalika Kihongosi alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) Mayunga Kashirimu kukamilisha kazi iliyobaki ndani ya siku 14 ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Ujenzi wa mradi huo unahusisha kulaza mabomba kwa urefu wa kilometa 190, kujenga matangi matano yakiwemo makubwa matatu yenye uwezo wa kubeba lita milioni mbili na kufunga viungio vya mabomba ambapo mpaka sasa wamebakiza mita 220 kukamilisha kazi iliyobaki.

.jpeg)

