Mradi wa kidijitali wa Dola milioni 150 kubadilisha taswira ya uchumi wa Tanzania

Arusha. Benki ya Dunia imeeleza kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), unaolenga kuchochea safari ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja (zaidi ya Sh2,596 trilioni) ifikapo mwaka 2050.

Mradi huo wa miaka mitano (2021–2026), unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Marekani milioni 150 (takribani Sh389.5 trilioni), unalenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kuweka msingi imara wa uchumi wa kisasa kwa kujenga na kuimarisha mifumo ya teknolojia nchini.

Akizungumza jijini Arusha jana, Februari 16, 2026, wakati wa ziara ya tathmini ya maendeleo ya mradi huo, Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Kidijitali wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini kutoka Benki ya Dunia, Paul Seaden, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi yenye mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, na kwa sasa uko katika hatua za mwisho za utekelezaji.

“Mradi unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, ndiyo maana tumekuja kutathmini hatua tulizofikia, hasa ikizingatiwa kuwa imesalia takribani miezi minane kabla ya kufungwa rasmi.

“Kikubwa ni kuhakikisha kama kuna changamoto zozote zimejitokeza katika hatua hizi za mwisho zinajulikana na zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati,” amesema.

Amesema katika kipindi cha utekelezaji wa miaka minne, mafanikio makubwa yamepatikana, ikiwemo upanuzi wa intaneti, uunganishaji wa taasisi za umma kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na kuanzishwa kwa vituo vya ubunifu vinavyolenga kukuza ujuzi wa kidijitali na ajira kwa vijana.

Kwa mujibu wa Seaden, muundo wa mradi huo unaogusa miundombinu, sera, huduma za umma na uendelezaji wa ubunifu, umeifanya Tanzania ya kidijitali kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine zinazotekeleza miradi ya kidijitali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia katika nchi za Afrika.

Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Kidijitali wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini kutoka Benki ya Dunia, Paul Seaden.



Awali, Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania, Bakari Mwamgugu, amesema mradi huo wa miaka mitano (2021–2026) umeleta mabadiliko yanayoonekana katika sekta ya mawasiliano.

Amesema hadi sasa minara 758 ya mawasiliano imekamilika na inaendelea kutoa huduma, hatua inayopanua wigo wa huduma za 3G na 4G, hususan katika maeneo ya vijijini na maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na huduma ya uhakika.

Aidha, ofisi 851 za Serikali zimeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku uwezo wa intaneti ukiongezwa hadi gigabiti 60 kwa sekunde (Gbps), hatua inayochangia upatikanaji wa huduma za mtandao kwa kasi na gharama nafuu ndani ya taasisi za umma.

“Katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, vituo 32 vya huduma pamoja vimeanzishwa kupitia ofisi za posta, vikikusanya huduma za taasisi mbalimbali katika eneo moja ili kurahisisha upatikanaji na kupunguza muda wa kusubiri.”

Amesema mradi huo pia unatekeleza ujenzi wa vituo vinane vya ubunifu katika mikoa ya Lindi, Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.

“Vituo hivyo vinatoa mazingira wezeshi kwa wabunifu, watafiti na wajasiriamali chipukizi kukuza mawazo yao na kuyaendeleza kibiashara.”

Amesema kituo cha Arusha, kilichotembelewa na ujumbe wa Benki ya Dunia, kinatarajiwa kuwa na maabara maalumu ya ubunifu (fabrication lab) kwa ajili ya uchakataji na urejelezaji wa vifaa vya kielektroniki, pamoja na kutoa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kwa vijana na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Salome Kessy, amesema mradi huo unatekelezwa sambamba na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10 (2024–2034), unaolenga kuimarisha mchango wa Tehama katika ukuaji wa uchumi.

Amesema mkakati huo unakusudia kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, maboresho ya sera na mifumo ya usimamizi, pamoja na ujumuishaji wa wananchi wote katika huduma za kidijitali.

Amesema matokeo yanayotarajiwa kupitia mradi huo ni kunufaisha zaidi ya Watanzania milioni 13 na huduma mpya za mawasiliano.

“Lengo ni kufikia angalau asilimia 80 ya matumizi ya intaneti kitaifa na kuongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya huduma za umma zinazotolewa kwa njia ya mtandao,” amesema.