Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesimulia tukio la mwanafunzi wa kidato cha kwanza mkoani Tanga kubakwa na muhusika kuachiwa huru, akitoa maagizo kijana huyo asakwe na kukamatwa.
Dk Mwigulu amesema baada ya kijana huyo kupimwa vinasaba (DNA) na kubainika mimba ni yake, aliachiwa huru kutokana na maelezo yaliyoandikwa kutoonyesha kama binti yule alikuwa mwanafunzi.
“Nilisema mkuu wa shule aje adhibitishe kama yule alikuwa anasoma au hasomi, sasa yule aliyembaka yule mtoto akamatwe na kama kesi ilimalizwa kwa rushwa irejewe upya, lazima wabakaji wahukumiwe,” amesema Dk Mwigulu.
Mtendaji huyo mkuu wa Serikali ametoa maagizo hayo leo Jumanne, Februari 17,2026 wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga alikofanya ziara kukagua jengo la oxygen.
Amesema aliyefanya tukio hilo la ubakaji ana umri wa miaka 53 na binti aliyetendewa tukio hilo ni mtoto akisisitiza huo ni ubakaji wa makusudi na haupaswi kufumbiwa macho.
“Huu ni ubakaji wa makusudi na si jambo la kufumbia macho, nyie mnaofanyiana undugu na ubakaji sisi hakuna hiyo, sisi wafugaji ukiwa na kundi la mifugo ukawa na dume anapanda wenzake tulikuwa tuna hasi, sasa kwenye sheria na katiba haikusema hivyo lazima sheria kali ichukuliwe kwa wahusika,” amesema.
Pia, Waziri Mkuu ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa jalada la tukio hilo kama ulifanyika mchezo watu wote waliohusika waunganishwe kwenye tukio hilo.
Awali, Mbunge wa Lushoto Mjini, Profesa Riziki Shemdoe, amesema moja ya mambo ya maendeleo yaliyofanyika katika jimbo la Lushoto ni kupatiwa Sh5 bilioni kwa ajili ya shughuli za afya ikiwemo ujenzi wa mtambo wa kuzalisha hewa safi ya Oxygen.
Mbunge huyo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), amesema kwa sekta ya elimu, kuanzia mwaka 2021 hadi 2026 wamepatiwa Sh17 bilioni na zimetumika kwenye ujenzi wa shule za msingi, sekondari, ukarabati wa shule na kutoa fedha za elimu bila ada.
“Katika ujenzi wa barabara tumepewa Sh12 bilioni na zimetumika kujenga barabara mbalimbali
“Barabara nyingi zina changamoto lakini ndani ya siku 100 tumepokea Sh4.5 bilioni za ujenzi wa barabara za Malibwi hadi Mlalo na zitajengwa kilomita tatu kwa Sh2.5 bilioni,” amesema.
Profesa Mdoe amesema changamoto nyingine wanayokumbana nayo wananchi ni ukosefu wa stendi na soko.
Amesema katika kutatua changamoto hiyo wameandaa andiko kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi na tayari limepelekwa Wizara ya Mipango wakiomba Sh6 bilioni kwa ajili ya kujenga stendi na soko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema uwekezaji katika sekta ya afya kwa mkoa huo umeongezeka.
Amesema mwaka 2021 ununuzi wa vifaa tiba walikuwa na Sh100 milioni sasa umeongezeka na kufikia hadi Sh400 milioni.