Planet yaivuruga Mwanza Eagles | Mwanaspoti

BUGANDO Planet imeitikisa Mwanza Eagles katika nusu fainali ya kwanza ya mashindano ya Dunda Wish Basketball  baada ya kuifumua kwa pointi 69-56.

Nusu fainali hiyo inachezwa kwa mfumo wa timu kukutana mara tatu (best of three play-off), na inafanyika katika Uwanja wa Mirongo uliopo mjini Mwanza.

Katika mchezo huo, Eagles ilianza kuongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 23-17 kabla ya vipindi vilivyofuata kuwa 10-14, 15-26 na 8-12.

Mchezaji Edmond James kutoka Bugando Planet aliongoza kwa kufunga pointi 17, akidaka mipira ya ribaundi mara saba, akipokonya (steals) mara saba na kuzuia mipira (block) mara nne.

Kwa upande wa timu za wanawake, Eagles Queens iliiadhibu Joseph & Mary School kwa pointi 71-33.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Mwanza, mratibu wa mashindano hayo, Frank Matarange alisema timu nne ndizo zinazoshiriki nusu fainali hiyo.

Alizitaja upande wa wanaume kuwa ni Bandari (Mwanza), Mwanza Octopus, Mwanza Eagles na Bugando Planet.

Kwa mujibu wa Matarange, timu nane zilishiriki mashindano hayo huku Profiler Swish Basketball, Oratorio, Kisesa Warriors na Switch zikishindwa kutinga hatua ya nusu fainali.