Dar es Salaam. Unaweza kusema ni filamu mpya imeibuka ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), baada ya wanachama wa chama hicho kugawanyika katika makundi mawili; moja likidai linaelekea mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kuwaengua viongozi wa kitaifa waliopo, huku lingine likiwa katika maandalizi ya kufanya mkutano wa kuchagua uongozi mpya.
Msingi wa utofauti huo ni uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uchaguzi uliofanyika mwaka 2024, uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake watano.
Mbali na Profesa Lipumba, wengine walioathirika na uamuzi huo ni Makamu Mwenyekiti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya (Bara), na Ali Juma Khamis (Zanzibar).
Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha CUF wanaounga mkono uamuzi wa Msajili wakijadiliana na kufanya maandalizi ya mkutano wa Baraza Kuu wa siri unaotarajiwa kuketi siku mbili zijazo kwa ajili ya kufanya mkutano wa kuchagua viongozi wapya.
Sababu ya kutenguliwa kwa uchaguzi huo ni kuwa washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama, inayohitaji mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali, hivyo mchakato ulipaswa kurudiwa.
Kufuatia uamuzi huo wa Msajili, umesababisha wanachama wa chama hicho kugawanyika katika makundi hayo mawili, wapo wanaopinga uamuzi huo na kudai wanaenda mahakamani kwa kuwa uamuzi huo umefanyika bila kuzingatia haki, ikiwemo kupewa haki ya kusikilizwa.
Wanachama hao wanadai wakati uchaguzi huo unafanyika ulihudhuriwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye mwishoni alieleza kuridhishwa na mchakato mzima, wamehoji ikiwa malalamiko yaliwasilishwa tangu mwaka 2024, kwa nini hakukuwa na uamuzi hadi sasa.
Kwa upande wa wanachama wanaounga mkono uamuzi wa Msajili, na kukiri uchaguzi huo ulikuwa batili, wanadai Baraza Kuu litafanyika Ijumaa ya wiki hii na siku itakayofuata watachagua Mwenyekiti mpya wa chama hicho, huku wakisema wana baraka zote kutoka Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa.
Hata hivyo, akijibu hoja za wanaokimbilia mahakamani, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amehoji ni haki ipi ambayo CUF hawakupewa, akisisitiza ofisi hiyo iliwapa nafasi ya kujieleza.
“Hawa wanashindwa kuelewa ni nafasi ipi hawakupewa. Kutoa nafasi ya kujieleza si lazima waitwe ofisi ya Msajili, walipewa nafasi ya kujieleza kwa njia ya barua. Sasa wanataka nini?” amehoji Nyahoza.
Katika maelezo yake, amesema katika mgogoro uliowahi kutokea kati ya Profesa Lipumba, na aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu), ofisi ya Msajili ilitoa uamuzi wa kumtambua Lipumba na kumkana Maalim Seif, na chama kiliridhia. Amehoji kwa nini sasa wanapinga uamuzi.
“Hatukuchelewa kutoa uamuzi, tulikuwa tunafanya uchunguzi wa madai yaliyoletwa na wanachama wao. Baada ya kujiridhisha, ndipo tukatoa uamuzi,” amesema.
Nyahoza amesema hayo alipozungumza na Mwananchi leo Jumanne, Februari 17, 2026, dakika chache baada ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Magdalena Sakaya, kukutana na waandishi wa habari makao makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sakaya amesema hawakubaliani na uamuzi huo na wameamua kwenda mahakamani, akisema hawatakubali kupokonywa madaraka na Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Tuna mpango wa kwenda mahakamani kwa kuwa hatujatendewa haki. Tunaenda kupinga uamuzi wa Msajili, na amri ikitolewa, tuko tayari kufanya uchaguzi kwa utaratibu wa chama chetu. Hatuwezi kupangiwa uongozi na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” amesema Sakaya.
Amesema chama hicho kina Katiba, kimesajiliwa kikatiba na kisheria, kina sheria, kanuni na misingi inayokifanya kuwa taasisi imara inayopaswa kujitegemea na kujiendesha kwa kuzingatia utawala bora bila kuingiliwa.
Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, akizungumza leo Februari 17, 2026 na vyombo vya habari kabla ya kuvurugika na Jeshi la Polisi kuingilia na kuhamasisha amani.
Sakaya amesema chama kina vyombo vya uamuzi, na iwapo Msajili anaona uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti ulikuwa na dosari kwa kuwa kura hazikuzidi asilimia 50, basi hoja hiyo haina msingi, kwa kuwa kati ya wagombea tisa, zaidi ya nusu ya kura zilipatikana kwa mujibu wa utaratibu wa chama.
Amesema katika mkutano huo, Baraza liliridhia kuwa atakayepata kura nyingi ndiye mshindi, na Mkutano Mkuu uliamua hivyo kwa mujibu wa mamlaka yaliyo ndani ya Katiba ya chama.
“Tukienda mahakamani na ikibainika kuna makosa, tutakuwa tayari kurudia uchaguzi, lakini si kwa shinikizo la Msajili. Leo tunaambiwa ratiba inatoka, na tunasikia tetesi kuwa kesho Baraza Kuu linafanyika, ilhali mimi kama mjumbe sina taarifa,” amesema.
Amesema ofisi ya Msajili imekuwa ikitoa taarifa za kuandaa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu bila kuwajulisha wajumbe halali wanaotambulika na Katiba ya chama, jambo alilodai ni ukiukwaji wa Katiba.
“Nipo hapa tangu asubuhi hadi jioni sina taarifa yoyote. Umma ujue kuwa CUF si chama cha kawaida, ni chama cha ukombozi kilichoasisiwa mwaka 1992, kina uongozi wake. Kama kuna shida, lipo Baraza Kuu la chama,” amesema.
Amesema Baraza hilo lililopitishwa siku ya uchaguzi lina mamlaka ya kuamua hatua zinazofuata kwa mujibu wa Katiba ya chama, likiwemo jukumu la kuandaa Mkutano Mkuu.
“Hatuko tayari kuwekewa uongozi. Tuko tayari kurudia uchaguzi endapo uamuzi wa haki utapatikana kwa kuzingatia Katiba yetu,” amesema.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zinaeleza Baraza Kuu la chama hicho linatarajiwa kukutana kwa siri Alhamisi wiki hii kuandaa mkutano mkuu utakaofanyika Jumamosi kwa ajili ya kuchagua safu mpya ya uongozi.
Kwa mujibu wa Daud Hassani, mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu wanaounga mkono uamuzi wa Msajili, amesema Baraza Kuu litaketi kuandaa hoja za Mkutano Mkuu utakaofanyika Jumamosi kwa lengo la kupata uongozi mpya.
“Ni kweli, tupo kwenye majadiliano na Msajili, tuna baraka zake. Tunafanya uchaguzi kupata uongozi mwingine, tarajia kiongozi mpya baada ya uchaguzi huo,” amesema.
Sakaya alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, amekiri kuzipata, lakini akasema hajapewa taarifa rasmi, licha ya kuwa yeye ni mjumbe halali wa Baraza hilo.
“Sijapewa taarifa, na kama uongozi huo utafanyika, hatutaukubali isipokuwa uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa taratibu za chama chetu,” amesema.
Gari la polisi likiwa linaondoka katika ofisi za Chama cha CUF zilizopo Buguruni, Dar es Salaam leo Jumanne, Februari 17, 2026.
Kwa upande wake, Nyahoza alipoulizwa ni lini atatoa ratiba ya kukielekeza chama hicho kufanya uchaguzi wa viongozi wa miaka mitano, kama aliyoahidi, amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa ni la kiofisi.
“Hatutaweza kutoa taarifa kwa sasa kwa sababu kuna barua wamewasilisha. Haya ni mambo ya kiofisi; siwezi kuyazungumzia kwa vyombo vya habari,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za Baraza Kuu kukutana, Nyahoza amejibu hawezi kusema lolote kwa kuwa ni masuala ya kiofisi.
Hata hivyo, wakati Sakaya akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari, kundi la wanachama wa chama hicho wanaounga mkono uamuzi wa Msajili liliingia makao makuu ya chama hicho, likiwa linapiga ngoma na kuimba nyimbo tofauti huku likiwa na mabango yanayoeleza kuridhia kilichoamuliwa na Msajili.
Hali hiyo ya kelele ilikuwa kubwa kiasi cha Sakaya kulazimika kusitisha mkutano wake huo kwa muda kupisha vurugu hizo zilizodumu kwa dakika 10 hivi. Baada ya kuanza kuzungumza tena, kundi hilo lililokuja na waandishi wake lilianza kufanya mkutano kusifu uamuzi wa Msajili: “Tuna imani na Msajili.”
Wakati kiongozi wa kundi hilo, Daud Hassan, akiendelea kuongea, wafuasi wenzake walikuwa wanapiga kelele wakisogelea ukumbi ambao mkutano wa Sakaya unafanyika, hali hiyo ilizidisha vurugu kati ya wanaopinga uamuzi wa Msajili na wanaounga uongozi uliopo.
Ndani ya muda mfupi, polisi wakiwa na mitutu ya bunduki walitinga makao makuu ya chama hicho na kuingilia kati kutuliza mvutano huo uliokuwa unaendelea kutokota katika ofisi hizo zilizopo maeneo ya Buguruni, huku wakihamasisha amani itawale.
Polisi hao walitapakaa kila kona ya ofisi hiyo, kisha baadhi yao walianza kufanya mazungumzo, viongozi wote walionekana kuwa mstari wa mbele, baada ya hapo baadhi yao walitakiwa kwenda Kituo cha Polisi Buguruni kwa majadiliano, ingawa baada ya muda mfupi walirudi tena makao makuu ya chama hicho.
Hata hivyo, Hassan alipoulizwa inakuaje wanaleta vurugu, katika majibu yake alidai viongozi hao hawatambuliki baada ya barua ya Msajili, hivyo ofisi za makao makuu hayo zinatakiwa kubaki chini ya Baraza Kuu ambalo yeye ni mmoja wa wajumbe.