Dar es Salaam. Serikali imetangaza nafasi 1,086 za ajira katika sekta ya afya kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ikilenga kuimarisha utoaji wa huduma katika wizara, idara zinazojitegemea (MDAs), na mamlaka za serikali za mitaa (LGAs).
Kwa mujibu wa tangazo lenye kumbukumbu Na. JA.9/259/01/C/20 la Februari 13, 2026, nafasi nyingi ni za daktari daraja la II (Medical Officer Grade II) 492, zikifuatiwa na ofisa afya mazingira msaidizi daraja la II 172 na ofisa muuguzi msaidizi daraja la II, 100.
Nafasi nyingine ni tabibu msaidizi daraja la II, 90, daktari wa upasuaji wa kinywa na meno daraja la II, 65, ofisa muuguzi daraja la II, 50, fiziotherapia daraja la II, 39, mhandisi vifaa tiba daraja la II, 31, tabibu wa kinywa na meno daraja la II, 30 na daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama daraja la II, 17.
Kwa upande wa sifa, waombaji wa udaktari wanatakiwa kuwa na shahada ya udaktari, kumaliza mafunzo kwa vitendo (internship) na kusajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika.
Kada za uuguzi zinahitaji wahitimu wa shahada au stashahada waliosajiliwa na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania, huku wahandisi vifaa tiba wakitakiwa kuwa wamesajiliwa na Bodi ya Wahandisi Tanzania.
Kwa ofisa afya mazingira msaidizi, waombaji wanapaswa kuwa na stashahada ya sayansi ya afya ya mazingira na kusajiliwa na Bodi ya Wataalamu wa Afya Mazingira.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, waombaji wote lazima wawe raia wa Tanzania wasiozidi umri wa miaka 45, isipokuwa kwa nafasi za taasisi za kijeshi ambapo ukomo wa umri ni miaka 25 kwa wasio na shahada, na miaka 30 kwa wenye shahada. Waombaji wenye ulemavu wamehimizwa kutuma maombi na kuainisha hali zao katika mfumo wa maombi.
Maombi yote yanatakiwa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao kupitia Recruitment Portal ya Ofisi ya Rais ndani ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ifikapo Februari 27, 2026. Maombi yatakayowasilishwa nje ya utaratibu uliowekwa hayatazingatiwa.
Waombaji wanatakiwa kuambatisha barua ya maombi iliyosainiwa, vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa na wakili au mwanasheria pamoja na cheti cha kuzaliwa. Matokeo ya muda (provisional results), hati za matokeo (result slips) na “testimonials” hazitakubaliwa.
Tangazo hilo limesainiwa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.