Sh2.4 trilioni kujenga miradi 26 ya kimkakati Zanzibar

Unguja. Miradi 26 ya kimkakati yenye thamani ya Sh2.411 trilioni imepangwa kutekelezwa katika visiwa vya Unguja na Pemba. Ambapo mpaka sasa Sh869.15 bilioni zimeshatumika.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Februari 17, 2026 wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakari akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mwakilishi wa Mkoani, Khamis Mohammed Amran ambapo alitaka kujua kiasi cha fedha kinachotumika katika miradi ya kimkakati.

Awali, akieleza utaratibu unaotumika katika kugawa miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali lililoulizwa na mwakilishi Khamis, naibu waziri amesema Serikali hupanga na kugawa miradi ya kimkakati kwa kuzingatia Sera na Mipango ya Maendeleo ya Taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP) 2021-2026 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka husika.

Katika mchanganuo huu, amesema Serikali pia huzingatia matokeo ya tafiti na ripoti mbalimbali, tathmini za miradi iliyotekelezwa, pamoja na hali halisi ya upatikanaji wa rasilimali fedha ili kuhakikisha uwezo wa utekelezaji na wenye tija.

Kuhusu ushirikishwaji katika upangaji wa miradi ya kimkakati, amesema wananchi, taasisi zisizo za kiserikali, sekta binafsi pamoja na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hushirikishwa kikamilifu kwa lengo la kuongeza uwazi na kuhakikisha kuwa miradi inayopangwa na kutekelezwa inaleta manufaa ya moja kwa moja ya kiuchumi, kijamii na Taifa kwa ujumla.

Pia, amesema ugawaji wa miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali huzingatia, pamoja na mambo mengine, mahitaji halisi ya eneo husika, uendelevu wa mradi unaopendekezwa, uhimilivu wa kiuchumi, kijamii na kimazingira wa eneo kwa mradi husika na matokeo chanya yanayotarajiwa kwa wananchi na maendeleo ya Taifa.

“Kwa kuzingatia vigezo hivyo, Serikali inahakikisha kuwa miradi ya kimkakati inachangia kikamilifu katika kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati na mrefu,” amesema.