Dar es Salaam. Shahidi wa tisa upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameieleza mahakama walivyopata taarifa za vijana kuhamasishana kuzuia Uchaguzi Mkuu 2025, kumuunga mkono Lissu.
Shahidi huyo, PS 18544 ASP Geofrey Aggrey (47), mkazi wa Arusha, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, kikosi cha Anti Robbery, aliongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…Kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…Kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli… Tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, leo Jumanne, Februari 17, 2026, Aprili 3, 2025, akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya doria maeneo mbalimbali ya Arusha, alipata maelekezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi (SP) Boni Mgogo, kupitia simu ya upepo (redio call) kuwa katika eneo la Morombo, kijiwe cha Bajaji, kuna vijana wanahamasishana kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Walikwenda eneo la tukio ambapo waliwakuta vijana waliokuwa wakihamasishana kuzuia uchaguzi na kuwaweka chini ya ulinzi. Vijana hao walianza kukimbia lakini walifanikiwa kuwakamata wawili, P4 na P7, na akaelekeza watuhumiwa hao wapelekwe Kituo cha Polisi Murieti.
Pamoja na watuhumiwa hao, pia walikamata bajaji nne, mbili kati yake zikiwa za watuhumiwa wawili waliokamatwa.
Kituoni hapo walipata maelekezo tena kutoka kwa Kaimu RCO Arusha, akimtaka awapeleke watuhumiwa hao wawili katika ofisi za RCO Arusha, ambako aliwahoji kwa nini wanakula njama za kutaka Uchaguzi Mkuu usifanyike. Walijibu kuwa wanaunga mkono kauli ya Mwenyekiti Tundu Lissu ya kuzuia uchaguzi na kukinukisha.
Kisha alielekezwa tena na Kaimu RCO Arusha kufungua jalada la uchunguzi, kisha akapewa maelekezo ya kuwahoji kwa kina watuhumiwa hao kwa kushirikiana na askari wengine, naye akaandika maelezo yake.
Baada ya kumaliza ushahidi wake wa msingi, shahidi huyo alihojiwa na mshtakiwa kwa maswali mbalimbali ya dodoso.