Ukraine yalipa wanajeshi kuhifadhi mbegu zao za kiume

Dar es Salaam. Ukraine inakabiliwa na tatizo kubwa la kidemografia, lililozidiwa na uvamizi wa kijeshi wa Russia.

Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali imeanzisha mpango wa kufadhili wanajeshi wake kugandisha mbegu za kiume (sperm) na mayai kwa wanajeshi wa kike ili kulinda mustakabali wa familia zao na taifa kwa ujumla.

Shirika la Utangazaji la BBC leo Jumanne, Februari 17, 2026 limemnukuu Maxim (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 35 na mwanajeshi wa kikosi cha walinzi wa taifa wa Ukraine aliye mstari wa mbele mashariki mwa nchi, akisema anatamani wanajeshi wengi zaidi wazungumzie afya ya uzazi na kufikiria mustakabali wao.

 “Wanaume wetu wanakufa. Hazina ya vinasaba vya Ukraine inapotea. Hili ni suala la uhai wa taifa letu,” amezungumza kwa njia ya simu kutoka eneo la mapigano.

Aliporejea likizo hivi karibuni, mkewe alimshawishi kwenda kliniki jijini Kyiv na kuacha sampuli ya mbegu. Sampuli hiyo iligandishwa bila malipo chini ya mpango maalumu kwa wanajeshi.

Ikiwa atafariki vitani, mkewe atazitumia kupata mtoto waliyekuwa wakitamani. Lakini hata kama ataendelea kuishi, anaona hatua hiyo ni muhimu.

Amesema vitisho vya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) za Russia vipo kila mahali, hata kilomita kadhaa kutoka mstari wa mbele. Msongo wa mawazo unaathiri uwezo wa uzazi, hivyo ni lazima wafikirie kesho ya taifa lao.

Kliniki binafsi zilianza kutoa huduma ya kuhifadhi mbegu au mayai (cryopreservation) bure kwa wanajeshi mwaka 2022, mwanzoni mwa uvamizi wa Russia.

Mwaka uliofuata, Bunge la Ukraine liliingilia kati kuweka sheria na kutenga fedha za serikali kuratibu huduma hiyo.

Mbunge Oksana Dmitrieva, aliyeshiriki kuandaa sheria hiyo, amesema: “Wanajeshi wetu wanalinda mustakabali wetu, lakini wanaweza kupokea wao binafsi. Tulitaka kuwapa nafasi hiyo.”

Hata hivyo, mwanzoni sheria hiyo ilisababisha malalamiko makubwa ilipoeleza kuwa sampuli zote ziharibiwe iwapo mfadhili atafariki. Hilo lilibainika pale mjane mmoja wa vita aliponyimwa ruhusa ya kutumia mbegu ya mumewe aliyefariki.

Sheria ilifanyiwa marekebisho na sasa sampuli zinahifadhiwa bure, hadi miaka mitatu baada ya kifo cha askari, na mwenzi wake anaweza kuzitumia iwapo kuna ridhaa ya maandishi.

Hatua hiyo pia inalenga kukabili mzozo wa demografia uliokuwepo hata kabla ya vita, lakini sasa umeongezeka kutokana na vifo vya maelfu ya wanaume vijana vitani na mamilioni ya raia hasa wanawake waliokimbilia nje ya nchi kama wakimbizi.

Miundombinu ya nishati ikiendelea kushambuliwa na makombora ya Russia, maisha katika miji kama Kyiv yamekuwa magumu zaidi.

Katika Kituo cha Kitaifa cha Tiba ya Uzazi cha Kyiv, ambacho kilianza kupokea wanajeshi Januari mwaka huu, ni askari wachache tu waliojiandikisha hadi sasa, lakini uongozi una matumaini idadi itaongezeka.

Mkurugenzi Oksana Holikova anaeleza kuwa idadi ya wajawazito imepungua kwa nusu tangu vita ianze. Msongo wa mawazo, mashambulizi ya mara kwa mara na hofu ya kukimbilia mafichoni wakati wa ujauzito vimewafanya wanawake wengi kuahirisha maamuzi ya kupata watoto hali anayoiita “ugonjwa wa kuahirisha maisha.”

Kwa baadhi ya familia, changamoto ni za kisheria na kihisia. Katerina Malyshko na mumewe Vitaly walikuwa wakitafuta mtoto kwa muda. Walikuwa na viinitete vitatu vilivyohifadhiwa kliniki, wakisubiri hatua ya kupandikizwa.

Lakini Vitaly aliuawa kwa shambulizi la bomu. Katerina alizuiwa awali kuendelea na matibabu kwa kutumia viinitete hivyo. Ilibidi aende mahakamani, na baada ya miezi sita ya mapambano ya kisheria, alishinda kesi na kuruhusiwa kuvitumia.

 Anasema ushindi huo ulimletea furaha na huzuni kwa wakati mmoja furaha ya kulinda ndoto yao, na huzuni ya kumpoteza mumewe.

Kwa sasa hajawa tayari kujaribu kupata mtoto, akisema bado ana maumivu makubwa. Hata hivyo, anataka haki ya kuamua wakati atakapokuwa tayari. “Watoto wa wanajeshi waliouawa wanapaswa kupewa nafasi ya kuishi katika nchi ambayo wazazi wao waliifia,” amesema.

Changamoto kubwa inabaki kuwashawishi wanaume wengi zaidi kujiunga na mpango huo. Wengi huona aibu au hushindwa kuzungumzia matatizo ya uzazi na athari za kisaikolojia za vita.

Maxim anaamini wanajeshi wanapaswa kuhamasishwa rasmi kugandisha mbegu wanapoandikishwa, kama wanavyotoa sampuli za DNA kwa utambuzi endapo watafariki.

“Kinachokosekana ni kuzungumzia zaidi na kueleza kwa nini ni muhimu,” amesema. “Kwa sababu sisi wanaume, hatutafanya jambo mpaka tusukwe kufanya hivyo.”