…………..
CHATO
MBUNGE wa Jimbo jipya la Chato Kusini, Pascal Lukas Lutandula, ameeleza sababu kuu iliyomsukuma kununua mitambo ya ujenzi wa barabara kwa gharama zake binafsi ndani ya siku 100 za Ubunge wake, kuwa ni baada ya kushuhudia vifo vya watu wawili waliogonga kalavati wakiwa na usafiri wa bodaboda kisha kupoteza maisha.
Hatua hiyo ilimsukuma kugombea Ubunge wa Jimbo hilo ili aweze kutatua changamoto za ubovu wa miundombinu ya barabara na kero zingine za wananchi ikiwemo elimu, afya, maji, kilimo na michezo.
Awali akiwa kwenye kampeni za Ubunge kwenye Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025, Lutandula aliwaahidi wananchi kuwa ndani ya siku 100 za Ubunge wake atakwenda kutimiza ahadi ya ununuzi wa mitambo hiyo, jambo ambalo hatimaye limetekelezwa ndani ya siku 94 tangu kuapishwa kwake.
Akiwa kwenye mkutano maalumu wa hadhara baada ya kufikisha mitambo hiyo jimboni kwake leo na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa kata ya Bwanga wilayani Chato, ameahidi kuwa hatakuwa Mbunge wa maneno mengi bali vitendo.
Amesema nia yake ni moja na njema ya kuwatumikia wananchi hao kwa uaminifu mkubwa na ndiyo maana kabla ya siku 100 za Ubunge wake amelazimika kutumia gharama binafsi kununua mitambo ya kuchonga barabara, kukamilisha zahanati, vituo vya afya na vyumba vya madarasa vilivyokuwa vimetelekezwa kwa zaidi ya miaka saba.
Hata hivyo, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walio wakiwakilishwa na Katibu wao, ambaye pia ni Diwani wa kata ya Chato Jimbo la Chato Kaskazini, Mange Ludomya, wamempongeza Mbunge huyo kwa kuguswa na changamoto za wananchi kwa vitendo.
Wamesema kitendo cha Mbunge kununua mitambo ya ujenzi wa barabara na umaliziaji wa vyumba vya madarasa na zahanati kwa pesa zake binafsi ni moyo wa kizalendo zaidi, huku wakimwomba mitambo hiyo pia isaidie kutatua changamoto za barabara zilizoko Jimbo jirani la Chato Kaskazini.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia mapokezi ya mitambo hiyo, wamesema uamuzi huo utasaidia kunusuru afya za wajawazito na watoto wachanga ambao wanakabiliwa na adha kubwa ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na wakulima ambao wamekuwa wakishindwa kufikisha sokoni mazao yao kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bwera, Josephat Manyenye, ameonyesha kushangazwa na Mbunge huyo kutumia pesa za familia yake zaidi ya Shilingi Bilioni 1 kwaajili ya ununuzi wa mitambo hiyo ili iwanufaishe wananchi.
Amewataka wananchi kuendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kuwa na maisha marefu na utumishi wenye dhamira njema kwa jamii huku akiwataka wananchi kujisifu kwa kuchagua Mbunge mwenye maono na dhamira ya kweli

