Wadau watoa mapendekezo kuinusuru EAC

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Kenya, William Ruto akiitisha kikao cha dharura cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutokana na changamoto za kifedha, wadau wametoa mapendekezo kuikwamua EAC katika sintofahamu hiyo.

Moja ya mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kuwa na vyanzo mbadala vya mapato, kuishirikisha sekta binafsi pamoja na kuhakikisha nchi zinazodaiwa zinalipa michango yao ili kuinusuru jumuiya kwa sasa.

Wamewataka wakuu wa nchi kuja na suluhisho katika mtanziko huo na siyo kukutana pekee halafu mambo yakabaki vilevile.

Mkutano huo, utakaokuwa wa kwanza kufanyika baada ya zaidi ya mwaka mmoja, unatarajiwa kujadili mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha na hatua za kupunguza matumizi ndani ya EAC, baada ya nchi wanachama kushindwa kuwasilisha zaidi ya Dola 89.3 milioni (Sh232.78 bilioni) zinazodaiwa na taasisi za jumuiya hiyo.

Waziri wa Kenya anayeshughulikia Masuala ya EAC, Mikoa Kame na Maendeleo ya Kanda, Beatrice Askul amesema mkutano huo utashughulikia uhaba wa fedha, kupitisha mfumo mpya wa ufadhili uliopendekezwa na Baraza la Mawaziri la EAC, na kukubaliana namna ya kuratibu matumizi.

Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inaidai nchi wanachama dola 89,372,865, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiongoza kwa deni la dola milioni 27, ikifuatiwa na Burundi (dola milioni 22.7), Sudan Kusini (dola milioni 21.8), Somalia (dola milioni 10.5), Rwanda (dola milioni 5.2) na Uganda (dola milioni 1.1). Kenya na Tanzania pekee ndizo zilikuwa zimelipa kikamilifu mchango wa dola milioni saba kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Wakizungumzia hatua hiyo ya Rais Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa wakuu wa nchi wa EAC, wameeleza kwamba namna ya kuikwamua jumuiya huku wakitarajia kikao hicho kitakuja na suluhisho tarajiwa.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Dk Abdullah Hasnuu Makame amesema suluhisho la kifedha ambalo linatakiwa kufanyika ni nchi zinazodaiwa kulipa madeni yao kwani ni hitaji la kisheria, ambayo itasaidia uendeshaji wa shughuli za jumuiya.

Amesema amepata taarifa kwamba tayari Uganda wamemalizia kiasi cha fedha walichokuwa wakidaiwa wakati Burundi waliomba wawe wanalipa kila baada ya miezi mitatu huku Somalia na Sudan Kusini, hatima yao kwenye hilo ikiwa haijulikani.

“Burundi, Somalia, DRC na Sudan Kusini, kwa kweli sijajua kama wataweza kulipa, ingawa Burundi hivi karibuni imeteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambako analipa michango yake kikamilifu na kule ECA ambako ana nafasi kubwa ya kiutendaji.

“Burundi halipi michango hapa EAC tu, lakini kule kwingine analipa, DRC ana sababu zake za kisiasa lakini kama ni hivyo asingeingia kwenye jumuiya hii kwa sababu inahitaji ujirani mwema, usuluhishi wa migogoro. Kama kuna migogoro kati ya DRC na Rwanda, basi kulikuwa na makosa kuipa hadhi ya uanachama,” amesema.

Amesema wakuu wa nchi watakapokutana, endapo kikao hicho kitafanyika, angependa kuona wakizungumzia jambo hilo na kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo

“Siwezi kusema wachukue hatua gani kwa sababu wao ndiyo wakuu, wakiamua kuwekeana vikwazo, wataamua wenyewe. Wakiamua wasiwekeane vikwazo watu walipe fedha, watafanya hivyo…cha msingi waje na suluhisho, bila suluhisho jumuiya ipo katika wakati mgumu sana,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema ili kupata suluhisho la kifedha kwenye jumuiya, mfumo wa kisheria wenye meno unahitajika. Amesema EAC iwe na kanuni za wazi, nchi isiyolipa ipoteze haki fulani (mfano haki ya kupiga kura au kunufaika na baadhi ya miradi).

Pia, amependekeza vyanzo mbadala vya mapato. Amesema tozo ndogo ya kikanda kwenye bidhaa zinazoingia. Amesema kuwe na ushirikiano na sekta binafsi kwa kuweka mfuko maalumu wa maendeleo ya kikanda.

Mbali na hayo, Shoo amependekeza kuwe na uwiano wa michango, ipangwe kulingana na ukubwa wa uchumi wa nchi, si mfumo wa sawa kwa wote.

Amesema kuwe na uwajibikaji na uwazi kwa maana ya wananchi wa nchi wanachama waone manufaa ya moja kwa moja ya EAC. Bila uhalali wa kisiasa, amesema michango itaendelea kuwa ajenda ya pembeni.

“Hatua ya Ruto ni ya kisiasa na kimkakati, lakini suluhisho haliko kwenye mkutano pekee  lipo kwenye mageuzi ya mfumo wa ufadhili wa EAC. Kama jumuiya haitapata mfumo thabiti wa mapato na uwajibikaji, changamoto ya nakisi ya bajeti itaendelea kujirudia,” amesema.

Ameongeza kwamba: “Huu ni mtihani wa uhai wa taasisi za kikanda Afrika Mashariki  si suala la fedha tu, bali la dhamira ya kisiasa ya umoja.”