Wasira na mkakati wa kuikabili rushwa-2

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)- Bara, Stephen Wasira amesema mafanikio ya kuikabili rushwa nchini yatafikiwa iwapo wananchi watajengewa msingi wa kuichukia.

Amesema si CCM wala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zitakazofanikiwa kuikabili rushwa, kwa sababu ni kitendo kinachofanywa kwa siri kati ya mtoaji na mpokeaji.

Wasira anakuja na kauli hiyo kuhusu rushwa wakati ripoti ya taasisi ya Afrobarometer ya mwaka 2024, inaonyesha asilimia 75 ya wananchi waliohojiwa wanaamini kuna hatari ya kuadhibiwa ikiwa wataripoti rushwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 35 ya wananchi waliwasiliana na polisi kuhitaji kulipa hongo ili kuepuka matatizo, huku asilimia 30 walitoa rushwa ili kupata msaada polisi, asilimia 16 huduma za afya na 14 kupata viambatanisho.

Rushwa pia, imekuwa ikiripotiwa ndani ya chaguzi za vyama na kwa mujibu wa ripoti ya Takukuru ya mwaka 2024, asilimia 65 ya matukio ya kugawa rushwa yalitambuliwa katika michakato ya uchaguzi.

Wasira ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Kwa mtazamo wake, rushwa si suala la Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee, bali chama hicho kinapaswa kuiongoza jamii ya Watanzania kuipinga na kuichukia.

Amesema hata Takukuru haiwezi kumaliza rushwa, kwa sababu yenyewe inasubiri taarifa ndiyo ishughulikie kama ilivyo mahakama.

“Tumesema lazima tuanze kujenga utamaduni wa kuwafundisha vijana wadogo maadili ya nchi yao, ingawa kwa sasa jamii imebadilika,” amesema.

Wasira, amesisitiza rushwa ni tatizo nchini na anakiri ipo, si tu katika chaguzi za ndani za chama hicho, bali pia ndani ya nchi kwa ujumla.

Amesema madhumuni ya CCM ni kuhakikisha hakuna dhuluma, vitisho, rushwa wala uonevu, lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezwaji wake.

“Ndiyo maana ni lazima kuishirikisha jamii ichukie rushwa. Rushwa ni janga kubwa kwa sababu anayetoa anatoa na anayepokea anapokea wanakaa kimya,” amesema.

Kuna ukimya kwenye rushwa

Mara nyingi, amesema pande zote mbili inayotoa na kupokea rushwa hukubaliana kunyamaza, hakuna anayekiri kutoa au kupokea.

“Ikitokea mmoja akasema, inatoa nafasi kwa wengine kuuliza mlionana wapi? Tatizo ni kuwa wote wanatoa na kupokea rushwa, lakini hakuna hata mmoja anayesema,” amesema.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Wasira amesema lazima jamii ihusishwe na ufike wakati iichukie rushwa, kwani wengi wanaotoa rushwa hawafanyi hivyo kwa kupenda, bali wanalazimika.

“Kwa mfano, unaenda hospitali kutafuta dawa, unazungushwa na kuambiwa huwezi kupata dawa bila kutoa fedha. Mtu anatoa si kwa kupenda, bali kwa kutaka kupona,” amesema.

Amesema wakati mwingine mtu anajikuta njia panda, asitoe rushwa ili awe mzalendo lakini ahatarishe maisha yake, au atoe ili apate huduma.

Mfano mwingine wa mazingira magumu ya rushwa alioutoa ni mtu anapowekwa kizuizini polisi na kutakiwa atoe chochote ili kupata dhamana.

“Inakuwa ngumu kwa sababu unataka uhuru wako. Unatoa fedha, unatoka, halafu unanyamaza. Tafsiri yake unahalalisha. Ilitakiwa utoke na utoe taarifa, ili anayehusika awe na hofu kwamba anaweza kuulizwa alizipataje fedha hizo,” amesema.

Amesema utamaduni wa jamii kunyamaza unawafanya baadhi ya watu wajione huru kupokea rushwa, ndiyo maana amekuwa akihimiza jamii ikatae kutoa na kupokea rushwa ya aina yoyote.

“Rushwa ni tatizo kubwa na ni hasara. Kuna rushwa ndogondogo hospitalini na polisi, pia kuna rushwa kubwa, kama mtu kupewa zabuni ya kutengeneza barabara. Yeye anataka faida ya asilimia 10 na anayempa zabuni pia anataka asilimia 10,” amesema.

Amesema jumla inakuwa asilimia 20, jambo linalomuathiri mkandarasi ambaye hulazimika kupunguza gharama kwa kujenga chini ya kiwango.

“Matokeo yake, barabara inayopaswa kudumu miaka 15 hudumu kwa takribani miaka mitatu tu kabla ya kuharibika,” amesema Wasira.

Amesisitiza rushwa haiwezi kumalizwa na chombo kimoja wala kuisha mara moja, bali jamii yote inapaswa kuichukia na hiyo itasaidia kupunguza kasi.

Ameeleza kiwango cha rushwa kwa sasa hakilingani na zamani, akitolea mfano wakati anaanza siasa za ubunge akiwa na umri wa miaka 25, alikwenda kugombea bila kutumia fedha kwa maana hongo kwa wapigakura.

“Nilikuwa na Sh1,500 tu. Hiyo ndiyo fedha niliyokuwa nayo nilipoenda kuwania ubunge na nilikopeshwa na TANU (Chama cha Tanganyika African National Union). Wakati huo nilikuwa Katibu Mtendaji, baada ya kuwaaga kuwa naenda kuwania ubunge, Mwenyekiti wangu alinipatia mkopo huo na nikasaini,” amesema.

Amesema aliunganisha fedha hiyo na mshahara wake, akasafiri kwenda Bunda, mkoani Mara, kuwania ubunge na akafanikiwa kushinda na kuingia bungeni kwa mara ya kwanza.

“Sasa niambie, kama kweli walionichagua wangesema niwape fedha na kiwango nilichokuwa nacho ni Sh1,500, unadhani ingekuwaje? Lakini sasa mambo yamebadilika sana,” amesema.

Kuhusu suala la CCM kuungwa mkono na baadhi ya vyama vya upinzani vinavyodaiwa kuwa vya kimkakati wakati wa uchaguzi, amesema yanayozungumzwa ni hisia tu, zisizo na ushahidi.

“Katika daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa kuna vyama 19 vilivyosajiliwa, vyote vina lengo linalofanana na CCM la kutafuta dola. Sasa inawezekanaje waiunge mkono CCM, ilhali wao pia wanataka kutawala? CCM inapambana kubaki madarakani; kwa hiyo naona kuna mkanganyiko hapo,” amesema.

Amesema CCM haina chama adui wala chama rafiki na si kwamba hawakutani na vyama vingine, wanakutana na kujadiliana kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

“Tukijadiliana huwa tunapiga picha. Walikuwepo viongozi wa CUF, NCCR-Mageuzi, CCM na ACT-Wazalendo. Kwa hiyo si kweli kwamba CCM ina uadui na chama chochote. Sote tunatafuta kitumbua kimoja, hivyo ni lazima tubishane,” amesema.

Amesema kila unapokaribia uchaguzi, kila chama huandaa ilani kwa lengo la kuvutia wapiga kura na hakuna vyama rafiki kwa CCM.

“Ingekuwa ajabu kama kuanzia asubuhi hadi jioni tungefanya mambo mabaya tu. Kama chama kinatusifu kwa kazi nzuri, hakiwi chama rafiki, kinakuwa kinasifu kazi tu,” amesema.

Amesema wakati wa uchaguzi vyama hivyo haviendi kuwashawishi wananchi kuichagua CCM.

Amesema nje ya siasa, viongozi wa vyama ni marafiki na wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara. Akitoa mfano wa aliyekuwa kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kwamba wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara.

“Akiwa na shida tunapigiana simu. Ukifiwa, mwenzako anakuja. Lakini majukwaani tunapambana kwa hoja, na tukikutana kwenye vyombo vya habari tunapishana kwa hoja tu. Hata Freeman Mbowe tumekuwa tukizungumza kwa simu,” amesema.

Katika maelezo yake, amesema si wote wana uhusiano wa karibu, baadhi yao ni wakali zaidi. “Mwingine siwezi kumtaja, amekasirika mwaka mzima. Kwa kweli ni hatari kukasirika kuanzia Januari hadi Desemba, unaweza kupata presha.”

Ameongeza kuwa wanazungumza na viongozi wengi, akiwemo Joseph Selasini wa NCCR-Mageuzi na kwamba hakuna tatizo lolote katika mawasiliano yao.

CCM kujiimarisha, kujihuisha

Ameeleza CCM kimekuwa kikifanya shughuli mbalimbali kujiimarisha na kujihuisha kuendana na mahitaji ya kizazi cha wakati husika.

“Sisi tunajua kwamba tuna chama kinachoenda na wakati na tunajua asilimia zaidi ya 60 ya wapigakura wetu ni vijana. Tunatunga sera zinazoakisi mahitaji ya wapigakura,” amesema.

Ameeleza pamoja na ukongwe wake, CCM hakijawahi kuwa na mawazo ya kizamani, bali inajibadilisha kuendana na wakati, ndiyo maana nyakati zote kinaongoza.