::::::::::
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda , ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuibua na kulea waandishi bunifu wa Kitanzania ili kuongeza upatikanaji wa vitabu vya ubora kwa matumizi ya shule na kuimarisha fasihi ya Kiswahili nchini.
Akizungumza Mapema leo jijini Dar es Salaam Februari 17, 2026, wakati wa uzinduzi wa vitabu vya washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Mkenda amesema TET ina jukumu la kuandaa na kusambaza vitabu vya kiada na ziada kwa kushirikiana na waandishi wa ndani ili kuhakikisha wanafunzi wanapata machapisho bora na yanayoendana na mtaala wa taifa.
Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwa waandishi wazalendo ili kuongeza wingi wa vitabu vinavyoakisi mazingira ya Kitanzania, akibainisha kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuinua kiwango cha elimu na kujenga utambulisho wa kitaifa kwa wanafunzi.
Akizungumzia kuhusu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, amesema imelenga kuongeza idadi ya vitabu vinavyoandikwa na Watanzania pamoja na kuhamasisha ubunifu katika uandishi.
Prof. Mkenda amesema tuzo hiyo imepewa jina la Julius Kambarage Nyerer kwa kutambua mchango wake katika kukuza fasihi ya Kiswahili, ikiwemo kutafsiri kazi za William Shakespeare kwa ustadi wa hali ya juu.
Akizungumzia sekta ya uchapishaji, amesema Serikali itanunua na kusambaza vitabu vya washindi katika shule na maktaba ili kuwapatia waandishi na wachapishaji soko la uhakika na kuongeza thamani ya kazi zao.

.webp)
.webp)