WAZIRI SANGU AHIMIZA MAJADILIANO YA DHATI KUEPUKA MIGOGORO YA KAZI

.,……

Na Carlos Claudio Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Mhe. Deus Sangu (Mb), amewahimiza viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri nchini kutumia majadiliano ya dhati kama njia kuu ya kutatua changamoto na kuepuka migogoro isiyo ya lazima katika maeneo ya kazi.

Akizungumza leo Februari 17,2026 jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa vyama vya wafanyakazi, waajiri pamoja na mashirikisho yao, Mhe. Sangu amesema Serikali inaamini katika utatu wa ushirikiano (tripartite cooperation) baina ya Serikali, waajiri na wafanyakazi ili kuhakikisha mahusiano ya kazi yanakuwa yenye tija na ustawi kwa pande zote.

“Nawahimiza viongozi kutumia meza ya majadiliano kumaliza tofauti zenu. Tuwe wamoja, tuepuke migogoro isiyo ya lazima na tujenge utamaduni wa kuzungumza kwa uwazi na kwa dhati,” amesema Mhe. Sangu.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mfanyakazi anafanya kazi katika mazingira yenye staha na yanayozingatia utu wa binadamu, ikiwemo wafanyakazi wa majumbani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa ulinzi wa kutosha wa haki zao.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika sekta ya kazi na ajira, ikiwemo uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii inayolenga kuwajali wafanyakazi wote walioajiriwa na wasioajiriwa kwa kutambua mchango wao katika kukuza pato la taifa.

“Tumezindua sera ya kinga ya jamii kwa lengo la kumjali mfanyakazi anayechangia pato la taifa. Tunatambua nguvu kazi ya jamii ni mhimili muhimu wa uchumi wetu,” alifafanua.

Akizungumzia mwelekeo wa uchumi wa kidijitali (digital economy), Mhe. Sangu amesema ni lazima vyama vya wafanyakazi na waajiri vibadili fikra na mbinu za uendeshaji ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na soko la ajira.

“Tunaenda kwenye uchumi wa kidijitali, hata fikra zetu lazima zibadilike. Uendeshaji wa vyama nao unapaswa kuwa wa kisasa, wenye uwazi na unaozingatia katiba,” alisisitiza.

Aidha, amegusia suala la ada na uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi, akieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama na kwa kushirikiana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inapitia upya ada na mifumo ya uendeshaji ili kuhakikisha kuna uwazi, uwajibikaji na usawa.

“Lazima kuwe na mipaka na uwajibikaji. Ndiyo maana vyama vinawekewa msajili. Nia yetu ni kuona vyama vinakuwa imara na vyenye ufanisi katika kuwatetea wanachama wao,” alisema.

Ameonya juu ya baadhi ya vyama vinavyokumbwa na malalamiko ya ufujaji wa fedha za wanachama, akisema Serikali haitasita kuchukua hatua pale inapobainika kuwa fedha za wafanyakazi zimetumika kinyume na taratibu.

“Chama kinaposhindwa kusimamia fedha za wanachama, mfanyakazi anapopata changamoto hataweza kupata msaada wa kisheria anaostahili. Haya tutayafanyia kazi,” alieleza.

Mhe. Sangu pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia katiba za vyama, akibainisha kuwa si sahihi kwa viongozi kung’ang’ania madaraka kwa muda mrefu kinyume na taratibu zilizowekwa.

“Tuboreshe mifumo ya ukaguzi na tuendeshe vyama kikatiba. Si vyema kukuta chama kinaongozwa na viongozi wale wale kwa zaidi ya miaka kumi huku katiba ikiwekwa kando,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Sangu alinukuu andiko kutoka Kitabu cha Mwanzo 2:15 linalosema, “Bwana Mungu akamtwaa yule mtu akamweka katika bustani ya Edeni ailime na kuitunza,” akitumia andiko hilo kusisitiza wajibu wa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kulinda rasilimali alizokabidhiwa.

Aliwahakikishia washiriki kuwa ofisi yake iko wazi kupokea maoni na ushauri, akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha sekta ya kazi na ajira nchini.

“Sisi kama Serikali tumefungua milango ya mazungumzo. Napenda nisikie mengi kutoka kwenu. Tushirikiane kujenga mazingira bora ya kazi na maendeleo ya taifa letu,” alihitimisha.