Mbeya. Zaidi ya wananchi 6,000 ikiwamo vikundi 570 vya vijana, wanatarajia kukutana jijini Mbeya kwa ajili ya kongamano la elimu na fursa na mnyororo wa uchumi katika ufugaji nyuki, litakalofanyika mapema mwezi ujao.
Kongamano hilo litawaweka pia pamoja wafugaji wa nyuki wakiongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akitarajia kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.
Akizungumza leo Jumanne, Februari 17, 2026, Mkurugenzi wa GeoAfrica Consultant, Lukelo Mgana, amesema kongamano hilo litawakutanisha vijana kwa lengo la kutoa elimu juu ya ufugaji nyuki na fursa za kiuchumi badala ya kutegemea ajira baada ya kumaliza masomo.
Amesema wanatarajia tukio hilo litabainisha na kutatua kilio cha ajira kwa vijana kupitia shughuli za ufugaji nyuki, akibainisha washiriki ni taasisi za elimu ikiwa ni vyuo vikuu na kati, makundi mbalimbali kama bodaboda, bajaji na wananchi wengine.
“Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 6,000, ambapo vikundi vya vijana ni 570, tunaamini tukio hilo kubwa litabainisha changamoto, utatuzi wake na mwelekeo mpya wa sekta hii ya ufugaji katika mnyororo wa uchumi,” amesema.
“Zipo fedha zilizotolewa na Serikali Sh200 bilioni ambazo ni mahsusi kwa vijana, tutajadiliana fursa hizo kupitia ufugaji nyuki na hakuna kiingilio kwa washiriki, tutakuwa na Waziri Nanauka na mgeni maalumu, Pinda,” amesema Mgana.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Wafugaji nyuki (Tabedo), David Lyama amesema ipo changamoto ya ukosefu wa elimu na muunganiko wa chama hicho.
Mkurugenzi wa GeoAfrica Consultant, Lukelo Mgana (shati nyeupe) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la Ufugaji Nyuki litakalofanyika jijini Mbeya. Pembeni yake ni mwakilishi wa Chama cha wafugaji Nyuki (Tabedo), David Lyama
Amesema kupitia mkusanyiko huo utawapa mwanga mpya wa kuweza kutambuana na kupeana elimu na uzoefu, akieleza kilio cha soko kwa zao la asali inatokana na kutofahamu mzunguko wa shughuli hiyo.
“Wengi kuanzia kupaki asali hawana elimu ya ufahamu, madhara yake kilio cha asali kinakuwa kingi, ila tunaamini kongamano hilo litamaliza changamoto hiyo na bado mwitikio si mkubwa kama ilivyo kwenye kilimo.”
“Mapori ni mengi na nyuki haihitaji chakula wala matunzo au kupelekwa hospitali, unakuta mtu amepaki asali kwenye chupa la konyagi, hapa inapoteza ubora hivyo tutaelimishana,” amesema Lyama.
Ameongeza baada ya kongamano hilo wataweka utaratibu maalumu wa kuwasajili wafugaji nyuki na kuwatembelea mtaa kwa mtaa ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa rasmi na kufikia malengo.