Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Thobias M. Makoba, tarehe 18 Februari 2026 amekutana na Prof. William A. L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika ofisi za Makamu Mkuu wa Chuo zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wawili walijadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya Kitengo hicho kipya cha Wizara hususan katika eneo la utafiti, kujengea uwezo watumishi, kuandaa makongamano ya pamoja na mikutano ya kimataifa na namna ya kuimarisha ushirikiano na vyuo vingine vya Afrika.
Aidha Viongozi hao pia walijadili umuhimu wa kuandaa mikakati ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo mojawapo ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi.
Kwa upande wake, Prof.Anangisye alieleza utayari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushirikiana na Wizara ya Mambo ya nje katika kutekeleza masuala muhimu waliojadili na kukubaliana katika kikao hicho kwa manufaa ya pande zote mbili.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Thobias M. Makoba, alimshukuru Prof. Anangisye kwa mapokezi mazuri na utayari wa ushirikiano na Wizara katika kukuza Diplomasia ya uchumi.




