Barker anavyolichambua boli la Mpanzu Simba

JANA usiku kikosi cha Simba kilikuwa uwanjani kucheza mechi ya kusaka tiketi ya CAF kwa msimu ujao dhidi ya Green-land, huku baadhi ya mashabiki wa Msimbazi wakionekana kama hawakielewi kiwango cha kiungo mshambuliaji Elie Mpanzu, lakini kocha wa timu hiyo amemaliza utata fasta.

Kocha huyo, Steve Barker, amewatuliza mashabiki na wapenzi wa Simba kwa kuwaambia Mpanzu yupo vizuri na wala hana tatizo lolote kiasi cha wao kuona kama ameshuka kiwango kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker alisema Mpanzu bado ni mmoja kati ya wachezaji muhimu wa kikosi hicho, hivyo hataki apimwe kwa kuangalia mabao au asisti zake uwanjani.

Barker aliyetua katikati ya Desemba mwaka jana akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini, alisema Mpanzu ana mchango mkubwa katika utekelezaji wa falsafa na mbinu zake uwanjani, kwani ana nguvu za kutosha kuisaidia timu wakati imepoteza mpira.

MPA 01


“Nina furaha na Mpanzu. Ni mmoja kati ya wachezaji wazuri nilionao katika timu yetu. Ukiangalia falsafa tuliyojiwekea utaona jinsi gani anafanya kinachostahili. Nafurahia nidhamu yake wakati timu haina mpira anasaidia sana,” alisema Barker na kuongeza:

“Ana juhudi sana uwanjani, lakini ana kasi kubwa pia kwenda eneo la wapinzani wakati tunawahi kutafuta mabao. Ni mchezaji muhimu sana kwetu. Anaweza asifunge au kuasisti, lakini akarahisisha upatikanaji wa mabao ya timu uwanja-ni.”

Kuhusu ukame wa kufunga, Barker alisema hilo ni kawaida kwa wachezaji. Hata hivyo anaamini kwa juhudi zake mabao yatakuja wakati wowote.

“Najua watu wanataka kuona anafunga au anatengeneza asisti, ni sawa. Hata sisi makocha tunatamani hilo naye pia huenda anataka iwe hivyo, lakini wachezaji wakubwa wanapitia nyakati kama hizi. Kitu muhimu mashabiki wanatakiwa kumpa nguvu kwa hali zote,” alisema Barker na kuongeza:

“Ukiangalia juhudi zake uwanjani unaona kabisa mabao yatakuja, ni mchezaji mwenye njaa ya ushindi, haya yote yatamsaidia kutoka hapa haraka.

MPA 02


“Mashabiki watulie, Simba bado ina mechi nyingi watamuona sana Mpanzu akicheza na kuwapa furaha ambayo wanaihitaji kama tu watakuwa sehemu ya utulivu wake wa akili.”

Mara ya mwisho Mpanzu kufunga bao katika Ligi Kuu ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Januari 18, 2026, na matokeo yaliyoisha kwa sare ya 1-1, lakini akiwa ni mmoja ya nyota wenye asisti nyingi kwa sasa wa timu hiyo, akiwa nazo tatu sambamba na Andrew Chamungu wa Namungo na Maxi Nzengeli wa Yanga, wakiwa nyuma ya kinara Duke Abuya wa Yanga mwenye asisti tano.

Hata hivyo, pamoja na mchango wa Mpanzu, baadhi ya mashabiki na wapenzi wanaona kama kiwango kimeshuka na kumsakama, licha ya hivi karibuni Ofisa Mtendaji wa Simba, Ahmed Ally, kumtetea kwamba nyota huyo raia wa DR Congo alikuwa na matatizo ya kifamilia yaliyochangia kucheza kwa presha, lakini kwa sasa amesharudi sawa na Wana-simba wajiandae kupata uhondo.