CUF hapatoshi: Wajumbe saba waliotimuliwa warejea kwa kishindo

Dar es Salaam. Mvutano ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umeendelea chukua sura mpya, kila uchwao na hali si shwari tena ni sakata linalowaka kama moto wa mafuta ya petroli ukiwaacha wanachama wakitazamana kwa mashaka na taharuki, bila kumjua Pilato wa kuamua.

Unawakumbuka wale wajumbe saba wa baraza kuu la uongozi waliovuliwa uanachama kwa tuhuma za kuwatembezea wenzao kichapo wakati wa vikao vya kuandaa wagombea wa uchaguzi mkuu wa 2025? Kama ulidhani walisambaratika basi imekula kwako.

Ilikuwa saa tano na robo hivi, Oktoba 6, 2025, walikinukisha katika ukumbi wa Shaban Mloo uliopo, makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, kwa kuwafungia wenzao ndani ya ukumbi na kuwasambazia vichapo kiasi cha baadhi yao kujeruhiwa. Hali hiyo ilisababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuwakamata baadhi yao kwa mahojiano zaidi.

Kundi hilo sasa limerejea ndani ya chama,  likiwa na msimamo mkali mithili ya ngiri anayewindwa na simba porini, wanadai wao bado ni wajumbe halali na hawatambui uamuzi wa kuwafuta uanachama uliotangazwa Agosti 7,2025 na Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Lipumba.

Msingi wa dhoruba zote hizo ni hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uchaguzi uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wenzake watano. Kwa maelezo yao, ikiwa msingi wa uongozi uliowafukuza umetenguliwa, basi hata uamuzi dhidi yao hauna nguvu kisheria wala kikatiba.

Wajumbe hao saba waliorejea na mikwara mizito ni Dauda Hassani, Yasin Ngotwa, Abdallah Dugwa, Faki Mohamed, Rashid Hamad, Mohammed Nassor na Yusuph Mussa walifutwa uanachama kufuatia kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Agosti 6, 2025, na uamuzi huo kusomwa hadharani siku iliyofuata na Profesa Lipumba.

Hata hivyo, mpasuko ndani ya chama ulianza mapema, pale Msajili wa Vyama vya Siasa alipotoa uamuzi Februari 13 mwaka huu wa kutengua uchaguzi wa Desemba 2024 uliomweka Profesa Lipumba na timu yake madarakani.

Mbali na Profesa Lipumba, walioathirika na uamuzi huo ni Makamu Wenyeviti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar) na Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, pamoja na Naibu makatibu wakuu Magdalena Sakaya (Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).

Sababu kuu ya kutenguliwa kwa uchaguzi huo ni kwamba washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa, kinyume na matakwa ya katiba ya chama inayotaka mshindi apate zaidi ya asilimia 50 ya kura. Kwa mujibu wa msajili, mchakato huo ulipaswa kurudiwa.

Uamuzi huo umeipasua CUF vipande viwili. Kundi moja linapinga hatua ya msajili na limeeleza nia ya kwenda mahakamani, likidai kuwa halikupewa haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kufanyika. Wengine, wakiamini ni fursa ya mwanzo mpya, na wapo kwenye maandalizi ya kuitisha mkutano wa kuchagua uongozi mpya.

Mwananchi imezungumza na kinara wa kundi hilo, Mjumbe wa Baraza Kuu Kanda ya Unguja, Mussa, amesema uongozi wa juu umetenguliwa kwa kukiuka taratibu za chama kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, Ibara ya 258, pamoja na Katiba ya CUF, Ibara ya 77 na vifungu vyake.

“Tulifukuzwa uanachama.Lakini kwa mujibu wa barua ya Msajili inatambua uongozi uliokuwepo kabla ya huu mpya. Hivyo, tumerejeshwa ndani ya chama na katika nafasi zetu kama kawaida, na sisi ni wajumbe halali wa Baraza la Uongozi la Chama Taifa,” amesema.

Amesema kwa uelewa wao, chama hicho kwa sasa hakina uongozi maalumu, bali kinaongozwa na Wajumbe wa Baraza Kuu, ambao wao pia ni wajumbe halali.

“Na mimi ni mjumbe pamoja na wenzangu sita. Ingawa wanatutafsiri kuwa tunaleta vurugu, nchi yetu inaongozwa na sheria, na sheria hiyo hiyo imeturejesha kundini,” amesema.

Kundi hilo limeungana na baadhi ya wanachama wanaounga mkono uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, hivyo katika kikao cha Baraza Kuu kitakachokaa siku ya Ijumaa kuandaa hoja za mkutano mkuu nao watashiriki kama wajumbe halali.

Wakati Mussa akieleza hayo, kwa mujibu wa barua ya msajili iliyotumwa CUF ya kubatilisha uchaguzi uliomweka Profesa Lipumba na wenzake watano madarakani, ofisi hiyo ilieleza kuwa inautambua uongozi uliokuwepo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo uliobatilishwa.

Hata hivyo, Sakaya amesema kinachoendelea ndani ya chama hicho ni uvunjaji wa taratibu, sheria na Katiba ya chama.

“Tunajua walio nyuma yao lakini hatutakubali chama chetu kugeuzwa na kupangiwa mambo wakati kina kila kitu, ikiwemo miongozo ya namna ya kuendesha shughuli zake,” amesema.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea