DTP YAWEKA MSINGI IMARA WA TANZANIA KUWA KITOVU CHA TEHAMA AFRIKA

………………

Na Carlos Claudio.

Mradi wa Tanzania ya Kidigitali (DTP) umeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya TEHAMA baada ya kukamilisha ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano iliyokuwa ikitangazwa hapo awali, huku minara hiyo ikiwa tayari inafanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia utekelezaji wa shughuli za mradi huo, Mratibu Mkuu wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali, Bakari Mwamgugu, amesema mafanikio yaliyopatikana ni makubwa na yenye matokeo chanya katika kufikia malengo ya kuijenga Tanzania ya kidigitali.

“Tumefanikiwa kukamilisha ujenzi wa minara 758 ambayo sasa inafanya kazi. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za mawasiliano na intaneti zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan katika maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma hizo,” amesema Mwamgugu.

Mbali na ujenzi wa minara hiyo, mradi huo pia umefanikiwa kuanzisha vituo 32 vya huduma, pamoja na kuongeza uwezo wa intaneti kwa kiwango cha juu cha Gigabits 60 kwa sekunde (Gbps). Kati ya hizo, Tanzania Bara inanufaika na Gbps 40 huku Zanzibar ikipewa Gbps 20.

Ongezeko hilo la uwezo wa intaneti linalenga kuhakikisha kuwa ofisi za Serikali zinapata huduma ya intaneti kwa bei nafuu na yenye kasi, hatua itakayochochea utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuharakisha safari ya kuelekea kwenye uchumi wa kidigitali.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kikosi Kazi kutoka Benki ya Dunia (World Bank), Paul Seaden, amepongeza utekelezaji wa mradi huo akieleza kuwa umekuwa wa mafanikio makubwa kuanzia hatua za usimamizi hadi utekelezaji wake.

“Ilikuwa ni mradi wenye mafanikio makubwa katika utekelezaji na usimamizi wake. Sisi kama Benki ya Dunia tutaendelea kuunga mkono shughuli zilizobaki ili kuhakikisha tunafikia malengo yote yaliyokusudiwa kabla ya kufungwa rasmi kwa mradi mwezi Oktoba,” amesema Siden.

Ameongeza kuwa ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia umechangia mafanikio hayo, na kwamba matarajio ni kuona shughuli zote zilizosalia zikikamilika kwa wakati ili kuhitimisha mradi kwa mafanikio makubwa zaidi.

Naye Dkt. Angelino Miso, Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo na Huduma za TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili kwa kina utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidigitali na hatua zilizofikiwa hadi sasa.

Amesema mwaka 2024, kupitia Wizara na chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilizinduliwa rasmi Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali wa miaka 10 (2024–2034), unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa kidigitali barani Afrika.

“Wizara kama msimamizi wa sekta imekuwa ikisimamia utekelezaji wa mkakati huu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuboresha miundombinu ya TEHAMA na mawasiliano ili kuhakikisha huduma zinapatikana nchi nzima,” amesema Dkt. Miso.

Ameeleza kuwa pamoja na kuboresha miundombinu, Wizara imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sekta kupitia nyaraka na miongozo mbalimbali ya TEHAMA na mawasiliano, sambamba na kuendeleza uwezo wa wataalamu wa ndani ili kukidhi mahitaji ya soko la kidigitali.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kidigitali (digital inclusion) ili kuhakikisha wananchi wote, bila kujali mahali walipo, wananufaika na huduma za TEHAMA na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali.

Kwa ujumla, mafanikio ya Mradi wa Tanzania ya Kidigitali yanaonesha dhamira thabiti ya Serikali katika kuimarisha sekta ya mawasiliano na TEHAMA, na kuweka msingi imara wa mageuzi ya kidigitali yatakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

=