FYATU MFYATUZI: Hebu tufyatue dhana ya familikrasia katika kisiasa

Leo nazamia rubaa za kimataifa na kitafiti. Baada mtoi wa marehemu rafiki yangu kutemeshwa bungo tokana na kupata ukwasi kwa kutumia surname, leo nazamia dhana mpya iitwayo Familikrasia, yaani unene wa kifamilia kama sehemu ya demokrasia mamboleo. Nitarejea utafiti wangu wa shahada ya uzamizi, PhD kama wengi waijuavyo.

Tasnifu hii ni ya kumi tena ya kubukua siyo kudukua, kununua, au kuzawadia kimagumashi kwa kukimbia umande.

Ila nashauri mniite Fyatu na si daktari maana, udaktari siku hizi, umechafuka baada ya kuvamiwa na kuishiwa maana sababu mazwazwa wameunajisi na kuutumia vibaya.

Lengo kuu ni kutaka kubaini kama familikrasia ina manufaa kikaya au kifamilia au vyote hasa baada ya kutema bungo au kufika ukomoni. Katika utafiti huu kuna matabaka makuu mawili ya ufyatuzi na ujembuzi.

Katika kutafiti dhana hii tata nilianzia mtaani kwangu Idodomya, we koma!! na kuelekea Equatorial Guinea, kwa Tarampu. Nilimalizia kwa M7 ambako familikrasia imeota mizizi na kutamalaki kitambo sasa. Katika variables nilizotumia, kuna makundi makuu mawili yaani, kupeana ulaji kifamilia au kirafiki kwa kutegemea uhusiano wa damu au wa kindoa.

Vigezo nilivyobaini ni utoi au ukweee. Mfano, kwa M7, vitegemezi na Bi Mkubwa ni sehemu ya sirkal ya Bwana Mkubwa kama sambamba na kwa Trampia ambako wakwe wanatesa katika ulaji. Kule Guinea ya Ikweta, vitegemezi vya munene vinatesa pia.

Utafiti huu wa kidoktari na kifyatu uligundua mambo makuu yafuatayo: Kwanza, wahanga wanachukia familikrasia kimyakimya wakiogopa kupotezwa na kupatilizwa. Hili, limebainishwa na dhana ya Unapokula Kula Usijali Kesho Utajiju (UKUKU) ambapo wahusika hugeuka waroho, wakabila, mafisadi, na ving’ang’anizi kwenye ulaji kiasi cha demokrasia kuwa kichekesho, kikaragosi, na ghasia.

Katika kufanya hivyo, hutenda makosa ambayo huwagharimu baadaye. Pia, nimegundua ukuku ndiyo ulisababisha maanguko na vifo vya akina Kashafi na Sir Damu.

Pili, familikrasia inachukiwa kwa sababu huhalalisha ufyatuaji mkubwa wa njuluku za mafyatu kutokana na uroho uliojificha nyuma ya ukuku.

Tatu, utafiti umegundua kuwa wengi, kama si wote, wa walaji hukosa vigezo vya kisomi isipokuwa ukaribu uwe wa kiukoo au kirafiki na mteuaji.

Hivyo, wengi huwa mazwazwa na wasanii wa kawaida wasio na sifa yoyote hata ya kuongoza kundi la nyumbu.

Nne, familikrasia hujihadaa na kujenga mfumo wa utukufu uchwara ambao msingi wake mkuu ni kutumia vitisho na kuzawadiana ili kuhimili vishindo vya uchakavu, ufisadi, na ulazimishi wake.

Hii inapotokea, hujengeka upofu au myopia kwa kisambaa ambao nao hujenga kujisahau na kutojiamini kiasi cha kila asiyekuwamo kuonekana adui na tishio. Hivyo, huleta ukandamizi, usanii, ubabaishi, n.k. Muhimili wa familikrasia ambao ni kichwa chake hujijengea uungufyatu kiasi cha kutengeneza viini vya kujiteketeza wenyewe.

Tano, familikrasia hulindwa kwa woga na kushuku. Hili, husababishwa na kupwaya na kutokubalika vizaavyo kutojiamini, kuaminika, na woga.

Sita, familikrasia hubebwa na ukosefu wa aibu, udhu, ufyatu, na ukatili vya kutisha. Mfumo huu, unaweza kuua yeyote anayetaka kuuzuia, kuupinga, kuukosoa, hata kuuondosha. Hivyo, kusababisha maumivu kwa mafyatu mbali na kuwanyonya.

Saba, familikrasia hutegemea sana matumizi mabaya ya njuluku na raslimali za mafyatu hongo ya, ulaji, maguvu, majungu, vishawishi, ghilba, na vitisho.

Kwa mtoi wa rafiki yangu, rahis wa zamani tena jobless, kilikutwa na mimamli kibao iliyotaifishwa. Je,viko vingapi duniani hii gunia?

Nane, familikrasia hutegemea kulindana, kung’ang’ania unene ukichelea kung’olewa ambapo jinai yake hufichuka na kuishia ghaibu au lupango hata kuuawa kama ilivyotokea kwa watajwa hapo juu. Tisa, utafiti umeonyesha kuwa ukuku kwa mfano, kuna uwezekano wa wahalifu wa kiunene kunyatuliwa roho na mafyatu wenye hasira wanapouchoka na kuamua kuuangamiza usiwaangamize.

Walaji wengi katika familikrasia wamethibitisha kuwa mifyatu mifala, milafi, yenye tamaa, na katili. Pia, mingi ya mifyatu hii ni mitoi, mikwezi, hata washirika wa bedroom hupenda ujiko kutanua ilhali upstairs ni kweupe.

Haina aibu na ni michafu usipime. Ingekuwa nazo sawasawa, ingeonea aibu udandizi, wizi, na ulaji wa njuluku za mafyatu bila stahiki isipokuwa unene wa mabuda, maza, au wakweee zao.

Pamoja na kushauri utafiti zaidi, tunapendekeza waathirika si kuuchukia tu ufamilikrasia bali waukabili na kuuondolea mbali ili kupata haki na maendeleo kwa ujumla. Katika penye ufamilikrasia kunakuwapo na amani mawenge ambapo haki na usawa hutoweka kiasi cha kaya kuwa kama pango la majembuzi.

Hivyo, dawa ya kuondokana na ufamilikrasia ni kuwapo na kutamalaki kwa haki, maadili, na mageuzi ya kweli kimfumo.

Mwisho, ufamilikrasia ni jinai inayoanza kuzoeleka na kuota mizizi katika kaya nyingi za uswekeni hasa zinazojifanya kuendelea.

Ushauri ni kwamba uchukiwe na kupigwa vita kulhali na na kuogopwa kama ukoma. Hii bangi, hivi niko wapi na nafanya nini yarabi!