Jiji la Dar laanza kuwaondoa machinga, bodaboda Kariakoo

Dar es Salaam. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza kuchukua hatua ya kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila wakati wa ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo.

Soko hilo lilikuwa katika ukarabati miaka minne iliyopita baada ya kupata ajali ya moto mwaka 2021, ambapo Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, shughuli iliyoendana sambamba na ujenzi wa soko dogo jipya lenye ghorofa sita.

Akizungumza katika hafla hiyo, ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan, Chalamila alisema kuanza kwa huduma katika Soko Kuu la Kariakoo kutaambatana na kufunguliwa kwa barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.

Bodaboda zikiwa zimeegeshwa katika barabara ya Msimbazi jirani na kituo cha mabasi yaendayo haraka Msimbazi A eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.



Hatua hiyo, kwa mujibu wa Chalamila, inalenga kuongeza usalama wa soko hilo, urahisi wa huduma na kurahisisha uokozi inapotokea changamoto.

“Inawezekana lisiwe jambo zuri na yanaweza kuwa maelekezo machungu kwa wafanyabiashara, lakini huwezi kujenga nyumba yenye thamani ukaziba barabara. Naamini diplomasia itaendelea kutumika pasipo kutumia nguvu kwamba barabara zitabaki wazi,” alisema.

Jana, Jumanne Februari 17, 2026, katika maeneo mbalimbali ya Kariakoo, kulikuwa kumebandikwa matangazo yaliyosainiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, akiwataka wafanyabiashara wanaopanga na kuuza bidhaa katikati ya barabara za mitaa na njia za waenda kwa miguu ambao hawajapangwa waondoe bidhaa zao mara moja.

“Wafanyabiashara wanaopanga na kuuza bidhaa katikati ya barabara za mitaa na njia za waenda kwa miguu ambao hawajapangwa waondoe bidhaa zao mara moja,” lilisomeka tangazo hilo.

Bidhaa zikiwa zimepangwa katikati ya makutano ya barabara ya Msimbazi na Uhuru eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.



Mbali na wafanyabiashara, pia tangazo hilo liliwagusa waendesha bodaboda na bajaji ambao imeelezwa watapaki katika maeneo ya vituo rasmi na wale wasio na vituo watapewa muongozo na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo.

Kwa upande wa magari yote ya kushusha na kupakia mizigo yenye vibali vya kuingia mjini, yataruhusiwa kuingia maeneo ya mjini kuanzia saa mbili kamili usiku hadi saa mbili kamili asubuhi, huku atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Aidha, wafanyabiashara wote wenye maduka wametakiwa kuondoa bidhaa zote zilizopo nje ya maduka yao kinyume na taratibu za biashara.

Wakizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Wamachinga Kariakoo, Stephen Lusinde, amesema chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni ukiukwaji wa sheria na makubaliano yaliyowekwa na mamlaka husika.

Lusinde ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, amesema wamachinga walishapangiwa maeneo maalumu ya kufanyia biashara na makubaliano hayo yalifikiwa baada ya vikao vingi kati ya uongozi wa wilaya, wakurugenzi na viongozi wa wamachinga.

Msongamano wa magari, bajaji na pikipiki kwenye makutano ya barabara ya Msimbazi na Uhuru eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.



Amesema kutokana na changamoto za usimamizi, wakati mwingine viongozi wa wamachinga hujikuta wakijisimamia wenyewe kwa kuwazuia wenzao wasivunje sheria, jambo linalowaletea lawama kutoka kwa jamii na mamlaka, ilhali hawana mamlaka ya kisheria ya kuchukua hatua kali.

“Tunawakamata wenzetu, lakini hatuna mamlaka ya kuwachukulia hatua za kisheria. Hatuna uwezo wa kutoza faini wala kuwafikisha mahakamani,” amesema.

Kwa mujibu wa Lusinde, idadi ya wamachinga wanaofanya biashara Kariakoo kwa sasa inakadiriwa kuwa kati ya 13,000 hadi 15,000, ilhali walio kwenye mfumo rasmi ni 8,900.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Madereva wa Bajaji na Bodaboda, Said Kagomba, amesema suala la katazo la bodaboda kutoingia Kariakoo wanashukuru wameshirikishwa ambapo kumeundwa kamati maalumu kwa ajili ya kuongeza vituo vingine kutoka vilivyo sasa.

“Tunashukuru kabla ya kutolewa kwa tangazo, Serikali imetushirikisha katika hatua zote na kama unakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan wakati anazindua soko, alisema tutafutiwe maeneo maalumu ya kuegesha bodaboda zetu, hilo linafanyika,” amesema.

Kwa mujibu wa Kagomba, hadi sasa kuna vituo 43, lakini ombi lao kwa Halmashauri ni kuongezwa vifike vituo 100 ambavyo vitakuwa na watu kuanzia 30, 50 hadi 100 kutegemea na ukubwa wa kituo.

Akieleza takwimu za bodaboda waliopo katika Jiji la Dar es Salaam hadi sasa, Mwenyekiti huyo amesema wapo zaidi ya 200,000 na kati yao 2,700 wapo Kariakoo pekee.

Kwa upande wa 2026, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Peter Mbilinyi, amesema chanzo cha wafanyabiashara kutoa mizigo nje ni ujenzi wa ngazi na utitiri wa wafanyabiashara wadogo.

“Baadhi ya maghorofa yanaruhusiwa kutoa ngazi hadi barabarani, ngazi zikishatoka nje, mpangaji anaongeza bidhaa zake barabarani. Hii ni sehemu ya tatizo linalohitaji kusimamiwa na jiji,” amesema Mbilinyi.

Mbilinyi amesema tatizo hilo ni la kiusimamizi, akieleza kuwa mipango mizuri imekuwa ikiwekwa lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu, hali inayosababisha watu kurudia tabia zilezile baada ya muda.

“Hata machinga waliwahi kupangwa vizuri, lakini baada ya muda wanarudi, swali ni usimamizi uko wapi? Kama jiji litaamua, linaweza kusimamia,” amesema.