Kocha Laizer aanika tatizo la Fountain Gate

FOUNTAIN GATE inapitia wakati mgumu, ikiwa haijashinda tangu mwaka huu 2026 uanze kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara, lakini kocha wa kikosi hicho, Mohammed Ismail ‘Laizer’ amelitaja tatizo linalowasumbua.

Iko hivi; Fountain imefikisha mechi tano bila kushinda, ikitoa sare mbili na kupoteza mechi tatu, ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa nyumbani Novemba 26, 2025 kwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Kama haitoshi, kwenye mechi hizo tano zilizopita imefanikiwa kufunga bao moja pekee ililolipata kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Namungo, Februari 4, 2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema tatizo kubwa linaloikwamisha timu hiyo ni ubora wa washambuliaji ambao bado wanahitaji kuongezewa utulivu wa kutumia nafasi.

Laizer amesema kikosi chake kinacheza vizuri na kutengeneza nafasi, lakini bado wanashindwa kuzitumia.

“Tunapitia wakati mgumu kidogo lakini naamini hali hii itaondoka, tatizo letu kubwa ni kama unavyosema kule mbele hatufanyi mambo kwa utulivu unaotakiwa,” amesema Laizer.

“Ingekuwa hatutengenezi nafasi ingekuwa mbaya zaidi, lakini timu inatengeneza, shida yetu vijana wamekosa utulivu, inawezekana inasababishwa na matokeo ambayo tunayapata, ile hali ya kujiamini imepungua.

“Hatukati tamaa, tunaendelea kuwapa mazoezi mazuri zaidi tofauti, lakini pia kuifanyia kazi saikolojia yao ili wawe sawa tuweze kutoka eneo hili.”

Laizer amesema anawaomba mashabiki wa soka Arusha kuja viwanjani kuishangilia timu hiyo na hamasa yao itawaongezea nguvu wachezaji wake.

“Tumetoka Manyara si kwa ubaya, nia njema kabisa tumekuja Arusha, unajua Arusha iliizaa Manyara, ni kama tumekuja kwa mama ili tuongeze baraka, mashabiki wa hapa wakija kwa wingi viwanjani utawaongezea kitu wachezaji wetu,” amesema.

Fountain itakuwa na mchezo mwingine wa ligi Februari 26, mwaka huu ikiikaribisha Tabora United, mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ulioko Arusha saa 10:00 jioni.

Juzi Jumanne, timu hiyo iliichapa Mapinduzi FC bao 1-0 katika hatua ya 64 Boya ya Kombe la Shirikisho (FA).