Mwanza. Inaweza ikawa moja ya hukumu za kihistoria baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, kutamka kuwa kifungu cha sheria kinachoruhusu baadhi ya mashahidi wa Jamhuri kutoa ushahidi wao kwa kufichwa kuwa hakitoa haki sawa kwa pande zote.
Ni hukumu ya shauri la kikatiba lililofunguliwa na Wakili Godfrey Basasingohe, iliyotolewa Februari 16, 2025 jijini Mwanza, ambapo njopo la majaji watatu limesema kifungu kinachotoa ruksa ya kutumia mashahidi fiche hakitoi haki kwa pande zote.
Hukumu hiyo inakuja kipindi ambacho baadhi ya mashahidi kwenye kesi ya uhaini inayoendelea dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu wakitoa ushahidi kwa kificho bila mshtakiwa kuwaona kwa sura wala jina.
Katika kesi hiyo, ni mawakili wa upande wa mashtaka pekee wanaowafahamu kwa sura na majina huku majaji wanaoendesha kesi wakiwaona katika kizimba maalumu.
Hali ikiwa hivyo, majaji kwenye shauri tofauti la kikatiba, wamesema kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinachotoa ulinzi wa kisheria kwa mashahidi hakitoi usawa wa sheria kama ilivyoainishwa chini ya ibara ya 12(1) na 13(1) za Katiba ya Tanzania.
Kwa mujibu wa majaji hao – Fahamu Mtulya, Kamana Stanley na Wilbert Chuma, kifungu hicho kinatoa haki za ulinzi kwa shahidi wa mashtaka pekee na kuwanyima haki mashahidi wa upande wa utetezi, hivyo wakalitaka Bunge likifanyie marekebisho.
“Ndani ya miezi 12 kuanzia tarehe ya uamuzi huu, kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifanyiwe marekebisho na Bunge la Tanzania ili kuzingatia kanuni ya ulinzi sawa wa sheria, na kushindwa kufanya hivyo, kifungu hicho hakitakuwa na nguvu ya kisheria,” wameeleza.
Katika shauri hilo la namba 22482 la 2025, Wakili Basasingohe ambaye aliwakilishwa kortini na Wakili Elias Hezron, alifungua shauri hilo dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Katika shauri hilo, mleta shauri ambaye ni muumini wa Haki za Binadamu, alieleza kuwa kifungu hicho cha 194 cha CPA kinacholinda mashahidi wa Jamhuri kinakiuka Ibara za 12(1) na (2) na 13(6)(a) na (d) za Katiba ya mwaka 1977.
Kutokana na ukiukaji huo, Wakili huyo aliomba nafuu tano, moja ni kwamba mahakama itamke kuwa kifungu hicho na kanuni za ulinzi wa mashahidi za mwaka 2025 vinakwenda kinyume na vifungu hivyo vya Katiba kwa kuwanyima ulinzi mashahidi wa utetezi.
Pia, aliomba mahakama itamke kuwa kwa kifungu hicho kutoa ruhusa ya kuwasilishwa maombi ya upande mmoja wa Jamhuri bila kumsikiliza mshitakiwa wala wakili wake kuhusu matumizi ya mashahidi wa kificho ni kumnyima haki ya kusikilizwa.
Halikadhalika, alitaka itamke kuwa hatua hiyo inamnyima pia mshitakiwa haki ya usawa mbele ya sheria, kusikilizwa kwa haki na dhana ya kutokuwa na hatia hadi shauri linapoamuliwa.
Mbali na amri hizo, wakili huyo aliomba pia mahakama itoe amri kwamba ama Bunge au mamlaka nyingine ya kutunga sheria, ichukue hatua ndani ya muda ambao mahakama itaelekeza, kukifanyia marekebisho kifungu hicho cha 194.
Si hivyo tu, aliomba amri hiyo iende mbali zaidi hadi kwenye Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za mwaka 2025, ili kuhakikisha haki ya usawa kati ya upande wa mashtaka na utetezi, na kutoa taratibu za kila hatua za kulinda mashahidi wa utetezi.
Wakili huyo alioomba Mahakama Kuu kuwa wakati inasubiri marekebisho hayo, amri zaidi itolewe kwamba hatua zozote za ulinzi za upande mmoja zilizotolewa chini ya kifungu cha 194 na Kanuni zake, zitakuwa chini ya uhakiki wa haraka wa pande zote, baada ya maombi ya mtuhumiwa au mawakili wake.
Akijenga hoja katika mawasilisho kupitia kwa Wakili Hezron, mleta shauri alidai kwa kifungu hicho ya 194 kutoa haki kwa Jamhuri pekee kunafanya kusiwepo usawa wa kiutaratibu ambao unadhoofisha haki za mtuhumiwa kusikilizwa kwa haki na kinakiuka kanuni ya usikilizwaji wa haki kwa sababu kinamruhusu DPP pekee kupata amri ya upande mmoja ya kuficha mashahidi na hivyo, kumfanya mshitakiwa ashindwe kuandaa utetezi wake kikamilifu.
Katika mawasilisho yao kupitia kwa Wakili wa Serikali Edwin Webiro, wadaiwa walisema kifungu hicho cha 194 kinachobishaniwa, hakikiuki haki ya kikatiba ya usawa kwa mshitakiwa wala kanuni ya haki ya usawakisheria.
Wakili huyo alisisitiza kuwa kifungu cha 194 kinampa DPP mamlaka ya kuomba hatua za ulinzi dhidi ya shahidi, iwe mbele ya taasisi ya mashtaka au katika hatua yoyote ya shauri la jinai.
Alieleza yeye (anavyoona), utaratibu huu umeundwa ili kuhakikisha usalama wa mashahidi na uadilifu wa mchakato wa kesi, bila kuunda faida yoyote isiyofaa au usawa wa kiutaratibu kwa upande wa mashtaka.
Alidai kifungu kilichopingwa hakimzuii DPP kuomba hatua za kumlinda shahidi wa mashtaka bali kinatoa ulinzi bila kutofautisha ni wa Jamhuri au utetezi; na kuwa yeyote anaweza kufaidika na hatua za ulinzi chini ya kifungu hicho, mradi tu anakabiliwa na vitisho, kwa kuwa hakisababishi uwiano usio sawa wa taratibu.
Alisema amri ya ulinzi wa shahidi inatolewa kwa upande mmoja kwa msingi wa kulinda utambulisho na usalama wa shahidi, hasa katika mazingira ambayo kuweka wazi utambulisho wake kunaweza kumletea vitisho au kudhuriwa; na kuwa dhana kwamba kinakiuka Katiba kwa kushindwa kumpa fursa mshitakiwa kupinga amri ya upande mmoja ni potofu.
Katika hukumu yao, majaji hao walisema baada ya kusikiliza ubishani huo wa kisheria, ni wajibu wa mahakama kuamua kama kutotoa nafasi kwa mshitakiwa kujibu ombi la upande mmoja ni kukiuka ibara ya 12(1) na (2).
Pia, mahakama hiyo ina wajibu wa kujibu kama kifungu hicho kinachoruhusu kutolewa kwa amri ya kulinda mashahidi bila kuwapa nafasi utetezi kupinga amri hizo, kunakiuka haki ya kusikilizwa chini ya Ibara ya 13(6)(a) na (b) ya Katiba.
Majaji hao walianza kwa kunukuu ibara ya 12(1) ya Katiba inayosema “Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa na Ibara ndogo ya (2) inayosema kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Halikadhalika majaji hao wakanukuu Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inayosema “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”
“Mapitio yetu ya kifungu cha 194 cha CPA yanaonyesha kwamba mamlaka ya kutuma maombi ya ulinzi wa mashahidi yamewekwa kwa DPP. Waombaji na wahojiwa wote wanakubaliana juu ya msimamo huu,” walisema majaji hao.
Kuhusu kama kifungu hicho kinakiuka misingi ya usawa mbele ya sheria, majaji hao walisema kukiukwa kwa misingi hiyo haipimwi kwa kuangalia maudhui ya kifungu kinachobishaniwa, bali matumizi halisia ya kifungu hicho.
“Ni maoni yetu kwamba kifungu cha 194 cha CPA hakikiuki kanuni ya usawa mbele ya sheria, bali kinakiuka kanuni ya msingi ya ulinzi sawa wa sheria,” walisema.
Majaji hao waliongeza kuwa “Kifungu kilichobishaniwa kinaunyima upande wa utetezi haki ya kuomba ulinzi wa shahidi wake, na hivyo kujenga ulinzi usio sawa wa sheria kati ya upande wa mashtaka na wa utetezi.
“Tofauti hii inadhihirika katika ukweli kwamba shahidi wa upande wa mashtaka pekee wanapewa haki ya ulinzi, wakati mashahidi wa utetezi wametengwa na ulinzi sawa wa kisheria, ambao unaathiri haki ya utetezi ya ulinzi sawa wa sheria.”
Majaji hao wakasema ni muhimu kuzingatia kuwa amri zinazotolewa na kifungu cha 194 kwa asili yake ni interlocutory (jambo linalofanyika katikati ya shauri kabla ya uamuzi wa mwisho), hivyo hazikatiwi rufaa kwa sababu huwa hazimalizi kesi ya jinai.
“Badala yake, inadhibiti jinsi ushahidi unavyotolewa wakati wa kesi, ikijumuisha hatua za kulinda usalama na usalama wa shahidi, bila kuathiri uamuzi wa mwisho wa hatia au kutokuwa na hatia,” walieleza majaji hao katika hukumu yao.
“Amri chini ya kifungu 194, ikiwa ni interlocutory haingii ndani ya nafuu za mwisho na kwa hivyo haiwezi kupingwa kupitia rufaa ya kawaida au taratibu za marekebisho zinazotolewa kwa uamuzi wa mwisho au amri,” walisisitiza.
“Vile vile, tafsiri yenye madhumuni ya ibara ya 13(6)(a) na (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inadhihirisha kuwa ibara hiyo iliundwa kutumika ili kuamua kwamba hatimaye kutatua haki na wajibu wa wahusika.
“Masuala ya amri zisizomaliza kesi ya msingi, kwa asili yake, ni ya muda na ya kiutaratibu, na kwa hivyo hayako nje ya malengo ya kifungu hicho, isipokuwa kama amri yenyewe inatoa haki za wahusika,” walisema.
Ni kwa msingi huo, majaji hao katika hitimisho lao walisema kwa usalama, kifungu cha 194 cha CPA hakikiuki kifungu cha 13(6)(a) na (b) cha Katiba, lakini hakitoi haki sawa kwa pande zote, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 12(1) na 13(10) za Katiba kwa kuwa kinatoa haki ya ulinzi kwa mashahidi wa Jamhuri pekee na kuwanyima haki kama hiyo mashahidi wa upande wa utetezi katika kesi ya Jinai.
Hivyo, wameagiza ndani ya miezi 12 kuanzia tarehe ya hukumu hiyo, kifungu hicho cha 194 kifanyiwa marekebisho na Bunge ili kuzingatia kanuni ya ulinzi sawa wa sheria na kisiporekebishwa ndani ya muda muda huo, hakitakuwa na nguvu ya kisheria.