Agosti 10, 2019, Epstein alikutwa amefariki dunia. Taarifa ya kitababu ikasema alijiua.
Agosti 29, 2019, mashitaka dhidi ya Epstein yalifungwa, lakini uchunguzi mpya ulifunguliwa kwa ajili ya kuwanasa washirika wenzake.
Baada ya kifo hicho, FBI waliwaweka kwenye rada watu 10, wakiamini walishirikiana na tajiri huyo kutenda uhalifu dhidi ya mabinti wadogo.
Baadhi ya watu hao ni Ghislaine Maxwell, Jean-Luc Brunel, Les Wexner, Darren Indyke, Richard Kahn na Lesley Groff.
Julai 2, 2020, Ghislaine alikamatwa na FBI, akiwa Bradford, New Hampshire. Maofisa wa FBI walitumia teknolojia ya IMSI catcher (stingray), ambayo hutumika kunasa mawasiliano ya anayefuatilia, vilevile kujua mahali alipo (tracking).
FBI walitumia teknolojia kuifuatilia simu ambayo Ghislaine alikuwa anaitumia kuwasiliana na mumewe, Scott Borgerson, dada yake, Isabel Maxwell, na wanasheria wake.
Kisha alifunguliwa mashitaka ya kutenda uhalifu wa makosa sita, ikiwamo kushawishi watoto kufanya vitendo vya ngono, kusafirisha watu kwa ajili ya ngono na kusema uongo chini ya kiapo.
Mahakama iliambiwa kuwa kati ya mwaka 1994 na 1997, Ghislsine alisaidia, aliwezesha, na alichangia kuwafanyia ukatili wa kingono wasichana wadogo, huku akitambua kuwa mmoja wa waathirika hao alikuwa na umri wa miaka 14.
Ushahidi mahakamani ulithibitisha kuwa Ghislaine, moja kwa moja, na kwa kujirudia, tena kwa miaka mingi, alishiriki mpango wa kutisha wa kushawishi na kusafirisha wasichana wadogo waliokuwa na umri wa miaka 14, kisha kuwafanyia ukatili wa kingono yeye mwenyewe, na kwa kushirikiana na Epstein.
Desemba 29, 2021, Ghislaine alikutwa na hatia. Juni 28, 2022, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Waendesha mashitaka walikuwa wameomba Mahakama itoe adhabu isiyopungua miaka 30 jela. Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja nyingine upande wa utetezi, hukumu ikawa ya miaka 20 jela.
Novemba 2025, mjumbe wa Congress, Jamie Raskin, alieleza ndani Baraza la Wawakilishi Marekani kuwa Ghislaine alikuwa akipata huduma za upendeleo. Kwanza amefungwa kwenye gereza lenye ulinzi mdogo, Bryan, Texas, hupewa chakula tofauti, wageni wake huruhusiwa kuingia na kompyuta, amepewa mbwa wa kumliwaza, pia alikuwa na fursa ya kutuma nyaraka au pepe popote alipotaka.
Kwa upendeleo aliokuwa akiupata Ghislaine, kama ilivyoelezwa na Raskin, lawama zote ni kwa uongozi wa Rais wa Marekani, Donald Trump. Kipindi Ghislaine alipokamatwa, Trump alitoa ujumbe wa kumtakia kila la heri, ulioibua gumzo kuhusu msimamo wake dhidi ya uhalifu mkubwa. Ikumbukwe, Trump alikuwa rafiki wa Epstein na Ghislaine alikuwa mfanyakazi, mshirika na mpenzi wa Epstein.
Jean-Luc Brunel, alikuwa mgunduzi wa wanamitindo. Brunel alipata umaarufu wa kimataifa alipokuwa anaendesha kampuni ya mitondo ya Karin Models.
Kisha, Brunel alianzisha kampuni ya mitindo ya MC2 Models Management. Ni raia wa Ufaransa aliyeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwenye sekta ya mitindo.
Waathirika wengi ambao vielelezo vyao vilikusanywa na FBI, walilitaja jina la Brunel na maelezo yao yalifanana kuwa mgunduzi huyo wa wanamitindo ndiye alikuwa akiwakuza wasichana wadogo na kuwaandaa kwa ajili ya kushiriki vitendo vya ngono mwenye makasri ya Epstein.
Mwaka 2019, kipindi FBI wakiwa wanajipanga kumfuatilia, polisi Ufaransa walifungua mashitaka dhidi ya Brunel.
Ni wakati ambao alikuwa akiishi kwa kujificha, akiogopa kukamatwa na kuunganishwa kwenye mashitaka ya Epstein.
Desemba 16, 2020, Brunel alikamatwa na polisi wa Ufaransa, alipokuwa Uwanja wa Ndege Charles de Gaulle, akijaribu kutorokea Dakar, Senegal.
Februari 19, 2022, Brunel alikutwa amefariki dunia kwenye chumbs chake, Gereza la La Sante. Uchunguzi wa kitabibu ulibainisha kwamba Brunel alijinyonga yeye mwenyewe.
Maelezo hayo yalikataliwa na wengi, wakitaka uchunguzi zaidi, maana inaonekana kuwa watu wenye kuonekana kuwa na taarifa za ndani kuhusu uhalifu wa Epstein, walikufa vifo vinavyofanana; kujiua.
Epstein alidaiwa kujiua, kama ilivyo kwa Virginia Giuffre, ambaye alikuwa mwathirika wa vitendo vya Epstein na wenzake, baadaye mwanamke huyo aligeuka sauti ya waathirika wa ukatili wa Epstein.
Kumekuwa na nadharia kuwa wahusika hawakujiua, isipokuwa wameuawa na watu wenye nguvu zaidi ili kuficha ushahidi dhidi yao kuwekwa hadharani.
Hapo majina nakubwa yanatajwa. Shauku kubwa ya umma ni kuona kila aliyetajwa kwenye Mafaili ya Epstein, anabainika uhusika wake na endapo atakuwa alishirikiana naye kuwabaka watoto wadogo wa kike au kuwafanyia ukatili wowote wa kingono, sheria ichukue mkondo dhidi yao.
Sauti ya umma Marekani na nchi nyingine ambazo zimekuwa na wahusika wengi waliotajwa kwenye Mafaili ya Epstein, inataka kuona haki inatendeka kwa wote walioathiriwa.
Hiyo ndiyo sababu ya uwepo wa shinikizo la kutaka kila kitu ndani ya Mafaili ya Epstein, kiwekwe wazi, umma ujue.
Moja ya mambo ambayo yamewashangaza wengi kupitia sakata la Mafaili ya Epstein, ni jinsi bilionea huyo alivyoweza kujenga mtandao mkubwa wa matajiri, wanasiasa wakubwa na watu wengine mashuhuri, wakiwamo wasanii, kisha kuwafanya nao kuwa sehemu ya uhalifu wake kwa watoto wadogo wa kike.
Dhahiri, Epstein alifahamu mapema kwamba ili apate utajiri mkubwa ilikuwa lazima ajiweke jirani na mabilionea wa dunia, awaingize kwenye uhalifu, atunze ushahidi dhidi yao, ambao ndiyo hasa alioutumia kupata alichotaka.
Maneno mawili ya Kiingereza, “blackmail”, likiwa na maana ya kumuingiza mtu kwenye mtego, akishaingia, unamtaka atoe fedha au masilahi mengine, ili usitoe siri zake hadharani, na “extortion”, kujipatia fedha au masilahi mengine kwa vitisho, kutokana na taarifa ulizonazo.
Epstein, aliwafanyia “blackmailing” na “extortion” wateja wake ili kutajirika na kubaki salama.
Hii ndiyo sababu kila mtu wa Serikali aliyethibitika kuwa alifanya vitendo vya uhalifu wa kingono na Epstein kwenye makasri yake, aligundulika kutoa taarifa za siri kuhusu Serikali kwa Epstein, ambaye alizitumia kujinufaisha kifedha.
Kwa matajiri, mfano wa karibu ni bilionea Les Wexner. Kati ya mwaka 1987 mpaka 2007, sehemu kubwa ya utajiri wa Wexner ililiwa wakati inasimamiwa na Epstein.
Mwaka 1989, Wexner alimmilikisha Epstein jumba lake la Herbert N. Straus, lililopo Manhattan, New York.
Halafu, akasaini kiapo cha kisheria (power of attorney), kumpa Epstein mamlaka ya usimamizi wa mali zake.
Wakati tuhuma za Epstein zikiwa zimezagaa, Wexner hakutaka kusikia lolote na hakuchukua uamuzi wowote kujitenga na mhalifu huo wa ngono kwa mabinti wadogo. Ni kipindi ambacho uhusika wa Wexner ulianza kufuatiliwa kwa ukaribu na FBI.
Ilionekana kuwa Wexner aliishi ndani ya mitego. Kwamba aliingizwa kwenye uhalifu na Epstein, ushahidi ukatunzwa, kwa hiyo ilibidi ajisalimishe kwake ili asiumbuliwe.