Juni 18, 2010, meneja wa zamani wa kasri la Epstein, lililopo Palm Beach, Alfredo Rodriguez, alihukumiwa miezi 18 jela.
Makosa ya Alfredo yalikuwa ni kutotokea polisi, badala yake akawa anataka kuuza jarida lenye matukio aliyorekodi alipokuwa anafanya kazi nyumbani kwa Epstein.
Ofisa wa FBI, Christina Pryor, alisema vitu alivyokutwa navyo Alfredo, vingesaidia sana kwenye kesi ya Epstein, lakini akawa hataki kutoa ushirikiano kwa polisi.
Baada ya kutoka jela, Epstein alihakikisha maofisa wengi wa mamlaka za dola wanakuwa karibu naye.
Matthew Menchel, aliyekuwa mkuu wa mashitaka ya jinai Jiji la Miami, alikuwa wa kwanza kueleza dhamira ya Acosta kutomshitaki Epstein.
Baadaye, Menchel akawa mtu wa karibu na Epstein. Rekodi za kipolisi zinaonesha kwamba, walikutana kila siku kuanzia mwaka 2011 mpaka 2017.
Tangu kusainiwa makubaliano ya Acosta na Epstein, kisha tajiri huyo kutoka jela, malalamiko ya umma yalikuwa haki kutotendeka.
Ilionekana Epstein ni “dude” lenye “miguvu” lililoishinda dola. Malalamiko hayo yalisababisha msukumo wa vyombo vya habari Marekani kuripoti na kufukua uhalifu wa Epstein tangu mwaka 2002.
Swali lilikuwa kwa nini aliyetenda makosa yanayostahili kifungo cha maisha jela, bado anatamba uraiani?
Upande wa pili ilibainika kuwa katika dili la makubaliano, Epstein alitoa “ofa” ambayo timu ya waendesha mashitaka iliona ni bora kwao, hivyo kuamua kuwaacha watoto walioathiriwa na Epstein wakiwa hawajui hatima ni nini. Epstein aliwaahidi kuwapa taarifa ambazo zingewezesha kuwatia hatiani watu wawili muhimu kwenye kashfa kubwa ya kifedha Marekani, iliyotokea muongo wa kwanza wa karne ya 21.
Ni kashfa kuhusu kufilisika kwa benki kubwa ya uwekezaji Marekani ya Bears Stearns.
Watu wawili, Matthew Tannin na Ralph R. Cioffi, ambao wote kwa nyakati tofauti walikuwa mameneja wa mfuko wa uwekezaji (hedge funds), katika benki ya Bears Stearns.
Machi 16, 2008, benki hiyo ilifilisika na kusitisha kufanya kazi zake, hivyo kuacha maumivu kwa matajiri wakubwa na taasisi zilizokuwa zimewekeza fedha kwa faida (hedge funds), hati fungani na hisa.
Ufisadi mkubwa ulifanyika hedge funds. Epstein kwa kufahamu Serikali ya Marekani ilihitaji taarifa za kuwezesha Tannin na Cioffi kutiwa hatiani, aliwashawishi, wakakubali, kisha yeye akapata unafuu wa kifungo kwenye kasi yake ya uhalifu wa ngono kwa watoto.
Kwa kukumbusha, Epstein aliwahi kuwa mfanyakazi wa Bears Stearns na alikuwa msimamizi wa akaunti za matajiri wakubwa.
Hata alipoachishwa kazi Bears Stearns, Epstein aliendelea kuwa mteja wa benki hiyo, na ni yeye aliyetengeneza fedha nyingi kwa kuwasaidia baadhi ya matajiri kuokoa fedha zao, kipindi cha kufilisika kwake.
Hii ilikuwa kashfa kubwa kwamba matamanio ya kuwakamata waliohusika na upotevu wa fedha za matajiri, ulisababisha kupuuzwa kwa mabinti wadogo waliotendewa ukatili na Epstein kwa kushirikiana na wenzake (wateja wake).
Kubainika kwa hili, kuliongeza presha ya umma, hasa kupitia vyombo vya habari. Mijadala mingi ilijenga hukumu ya kijamii kuwa Epstein ni dubwasha ambalo mamlaka za kisheria zilishindwa kumbananisha kwenye mizania ya haki.
Mwandishi wa habari, Julie K. Brown anaingia kwenye muktadha. Mwaka 2008, Julie alifanya kazi kubwa kuhakikisha Epstein anafikishwa kwenye mamlaka zinazotakiwa ili haki itendeke.
Julie akiwa mfanyakazi kwenye Gazeti la Miami Herald, aliandika makala mfululizo, zilizokuwa na kichwa cha habari, “Perversion of Justice”, kikiwa na maana ya “upindishaji wa haki.”
Ndani yake, Julie alieleza historia nzima ya vitendo vya Epstein na jinsi ambavyo imekuwa ngumu kwa haki kutendeka.
Aliandika kuhusu makubaliano ya kutoendelea na mashitaka mwaka 2008, kisha alijumuisha tuhuma za Epstein kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000, mabinti wadogo aliotuhumiwa kuwabaka, pamoja na maelezo kuwa, bilionea huyo alikuwa akiendesha genge la usafirishaji wa binadamu, wahusika wakiwa wasichana wadogo, aliowatumia kwa kuwabaka na kuwapasia wateja wake, ambao nao waliwatumia kujistarehesha.
Nguvu ya makala za Julie, ilikuwa mahali alipokuwa akibainisha kwamba mtandao wa Epstein wa ubakaji watoto wadogo, ulihusisha watu wenye nguvu kifedha na kimamlaka. Julie alisema, watu hao ndiyo sababu ya bilionea Epstein, kuendelea kudunda licha ya kuwa na tuhuma nzito, zenye ushahidi kwamba ni mbakaji.
Julie alibainisha kwamba, vigogo ndiyo waliochezesha makubaliano ya mwaka 2008, ili kumlinda Epstein, maana kushitakiwa kwake kungewaweka kwenye hatihati ya kushitakiwa na kuaibika katika kijamii.
Kazi kubwa ya Julie, iliungwa mkono na wanahabari wengine. 2018, ukawa mwaka wa kila kitu cha Epstein kumulikwa na kuanikwa.
Umma ukajua mengi na kuamka kupaza sauti. Dhahiri shahiri, isingekuwa salama kama Epstein asingefikishwa mahakamani na kupokea hukumu ya haki. Virginia Giuffre, mrembo aliyebakwa kwenye Kasri la Epstein, ushuhuda wake wa kubakwa na bilionea huyo, pamoja na wenzake, kama ilivyoripotiwa na Julie, ulijenga hasira ya umma.
Julai 6, 2019, Epstein alikamatwa akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Teterboro, uliopo New Jersey, alipokuwa anarejea Marekani akitokea Ufaransa.
Alifunguliwa mashitaka ya usafirishaji binadamu kwa ajili ya ngono na ubakaji wa mabinti wadogo (walio chini ya umri wa 18).
Kisha, maofisa wa FBI, walivamia Kasri la Epstein, Herbert N. Straus House, lililopo Manhattan, New York.
Ndani yake walikuta ushahidi wa kutosha kwamba, nyumba hiyo ilitumika sana kwa shughuli za ngono.
Ushahidi kuwa Epstein alisafirisha binadamu, tena mabinti wadogo kwa ajili ya shughuli za ngono, ulipatikana. Maelfu ya picha za utupu zilikutwa ndani yake.
Wote ambao picha zao za utupu zilikutwa ndani ya Kasri la Epstein, walikuwa wanawake.
Fedha, Dola 70,000 za Marekani, madini ya almasi na hati ya kusafiria ya Australia, iliyokuwa na picha ya Epstein, lakini jina tofauti, ikionesha kwamba mwisho wa matumizi yake ulikuwa mwaka 1987.
Hapa ilikuwa ikionesha kuwa, kabla ya Epstein kuwa maarufu, alishafanya uhuni wa kughushi hata pasipoti.
Hati hiyo ya kusafiria ilionesha aliingia na kutoka kwenye nchi za Ufaransa, Hispania, UK, na Saudi Arabia. Maaelezo ya kwenye hati hiyo ya kusafiria, yalionesha Epstein alikuwa mkazi wa Saudi Arabia, wakati hakuwahi kuishi kwenye nchi hiyo, zaidi ya kuongia na kutoka.
Wakili wake alitoa utetezi kwamba Epstein kwa kuwa alikuwa Myahudi, angeweza kutekwa aliposafiri nje ya Marekani, kwa hiyo hati ya kusafiria ya Australia ingesaidia kuwafanya watu wasimgundue kwa urahisi.
Julai 8, 2019, waendesha mashitaka kwa kushirikiana na Kitengo cha Rushwa cha Umma (PCU), cha Wilaya ya Kusini, New York, chini ya wakili Geoffrey Berman, walimfungulia Epstein mashitaka ya usafirishaji watu kwa ajili ya ngono, na kula njama ya kusafirisha watoto kwa ajili ya ngono. Hati ya mashitaka ilieleza kuwa, makumi ya watoto wadogo wa kike waliingizwa kwenye kasri kwa ajili ya kufanyishwa mapenzi.
Ilibidi pia makubaliano ya kumpa kinga Epstein ya kutoshitakiwa, yapitiwe chini ya Jaji Kenneth Barra.
Epstein, aliomba dhamana, alinyimwa. Aliweka fedha ili kuwalainisha. Alisema kuwa, alikuwa tayari kuweka Dola 100 milioni za Marekani kisha angekaa kwenye kizuizi nyumbani kwake New York, lakini alikataliwa.
Jaji Richard Berman, alisema kuwa Epstein alikuwa hatari kwa jamii, kumpa dhamana kungesababisha maisha ya wengi yawe kwenye hatari, vilevile angeweza kukimbia mashitaka yake.
Agosti 10, 2019, Epstein alikutwa amefariki dunia. Taarifa ya kitababu ikasema alijiua.
Agosti 29, 2019, mashitaka dhidi ya Epstein yalifungwa, lakini uchunguzi mpya ulifunguliwa kwa ajili ya kuwanasa washirika wenzake.