Mgunda hataki kurudia makosa | Mwanaspoti

BAADA ya vipigo viwili mfululizo katika mechi za Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema hatarajii kurudia makosa kwenye pambno lijalo la michuano ya Kombe la Shikirikisho la CRDB dhidi ya Magnet FC.

Namungo imepoteza mechi hizo zilizopita mbele ya Pamba Jiji kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 na ile ya Tanzania Prisons ilipolala kwa mabao 3-2 zote zikichezwa ugenini na na kuitibulia hesabu zao za kukusanya pointi  na kesho Alhamisi timu hiyo inarudi nyumbani ikiikaribisha Magnet FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema soka ni mchezo wa makosa, walizingua wenyewe na wakaadhibiwa japo haikuwa mipango yao kupoteza mechi mbili mfululizo, lakini ni matokeo ya mpira ambayo yanaumiza na yapo ili yatokee.

“Tumesahau matokeo yaliyopita makosa yalifanyika kama kocha niliyaona na kuyafanyia kazi sasa tunaendelea na maandalizi tayari kwa mchezo ulio mbele yetu tutaingia kwa kuiheshimu timu pinzani bila kujali daraja walilopo,” alisema Mgunda nyota wa kimataifa wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars aliyewahi pia kuzinoa Coastal Union na Simba.

“Tukishindwa kumheshimu mpinzani anaweza kutushangaza mpira sio uzoefu ni mbinu bora na mipango imara ili kutoka katika mtego wa kugawa pointi kwa wapinzani nimeianda timu vizuri matarajio ni kuvuka hatua inayofuata kwa kushinda mchezo,” aliongeza Mgunda.

Mgunda alisema, benchi la ufundi limeshafanya kazi kwa usahihi, kilichobaki ni utekelezaji kupitia wachezaji katika dakika 90 za mechi hiyo aliyobainisha matarajio yake ni kuona nyota hao hawarudii makosa kwa mara nyingine.

“Tunaelekezana ki utu uzima sisi wote tunatambua majukumu yetu, imani kwa vijana wangu ni kubwa na wao wametambua makosa yao hivyo matarajio ni kuwa na mchezo bora na sisi tunatarajia ushindani kutoka kwa mpinzani wetu,” alisema Mgunda.

Msimu uliopita katika michuano hiyo Namungo ilitolewa hatua ya 32 Bora kwa kufungwa mabao 3-0 na Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa Machi 11 mwaka jana, wafungaji waki ni Moubarack Amza aliyefunga mara mbili dakika ya 3 na 86 na Mkenya Shaphan Siwa aliyetupia dakika ya 62.