Miaka minane aidai Halmashauri Dar Sh50 milioni, kliniki ya sheria yamsaidia

Dar es Salaam. Baada ya kusota kwa zaidi ya miaka minane akifuatilia malipo ya zaidi ya Sh50 milioni kutoka moja ya halmashauri ya Ubungo jijini Dar es Salaam, hatimaye Frida Raphael ameona mwanga wa matumaini kufuatia kusikilizwa kwa shauri lake katika kliniki ya sheria inayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Frida, mmiliki wa kampuni ya Morah Supplies and Manufacturer, amesema alishinda zabuni ya kuhudumia halmashauri hiyo, akatekeleza majukumu yake kikamilifu, lakini malipo yakawa changamoto kubwa iliyomlazimu kuzunguka ofisi mbalimbali kwa miaka mingi bila mafanikio.

“Nilifanya kazi kwa mujibu wa mkataba, nikawasilisha vifaa na nyaraka zote kama ilivyotakiwa. Lakini malipo yakawa safari ndefu. Nimekuwa nikifuatilia kwa zaidi ya miaka nane,” amesema Frida kwa sauti yenye mchanganyiko wa huzuni na faraja.

Amesema katika kipindi chote hicho alikumbana na misukosuko ya kifedha, ikiwamo kushindwa kulipa ada za watoto kwa wakati na kuendesha biashara kwa taabu huku akiendelea kusimamia deni lake kwa subira.

“Kuna mikopo nilichukua nikawa nashindwa kurejesha kwa sababu sina pesa na ninaowadai wananizungusha mara nikienda wananilipa Sh3 milioni napunguza deni na kulipa ada za watoto huku nikiendelea kuhangaikia pesa yangu,” amesema Frida.

Amesema katika mapambano ya kupata haki yake amekuwa akizungushwa kila siku na kumuingiza kwenye ofisi tofauti, na mwisho wa siku alikuwa anaishia kwenye benchi za ofisi hizo bila mafanikio.

Frida amesema kutokana na uchelewaji wa haki yake alishaandika barua katika ofisi mbalimbali na hata kupeleka Ikulu lakini hakupata haki yake kwa wakati, huku akielezwa kuna nyaraka hazipo sawa kwa wadaiwa.

Hata hivyo, alipopata taarifa za uwepo wa kliniki ya sheria katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, aliamua kufika na kuwasilisha malalamiko yake. Ndani ya muda mfupi, shauri lake limesikilizwa na wahusika kuahidi kulifanyia kazi haraka.

“Kwa kweli nimepata faraja kubwa, nilikuwa nimechoka kuzunguka ofisi bila majibu ya moja kwa moja. Leo nimesikilizwa na nimeahidiwa kulipwa hivi karibuni,”amesema.

Akizungumza kuhusu suala hilo, leo Jumatano, Februari 18, 2026 Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu wa kliniki hiyo, Ipyana Mlilo amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafuatilia kwa karibu hadi Frida atakapopata haki yake.

“Lengo la kliniki hii ni kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa haraka. Tutafuatilia hadi haki ipatikane,” amesema Mlilo.

Pia, Mulilo amesema hadi kufikia Februari 17, 2026 mashauri 156 yamesikilizwa ambapo siku ya kwanza Februari 16, 2026 mashauri yalikuwa 49 na siku iliyofuata ni 107.

Mashauri ambayo yamejitoza katika kliniki hiyo ni migogoro ya ardhi 59, mirathi 24, ndoa 24, madai 13, waliofuata elimu 10, matunzo manne na jinai 16.

Amesema kliniki hiyo imekuwa msaada kwa wananchi mbalimbali wanaokabiliwa na changamoto za kisheria, hasa wale waliokwama katika mifumo ya madai na migogoro ya muda mrefu.