Mwanaharakati Jesse Jackson afariki dunia

Chicago. Mchungaji na kiongozi wa haki za kiraia wa Marekani, Jesse Jackson amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84.

Taarifa iliyotolewa na familia yake imethibitisha kuwa amefariki leo, Februari 17, 2026, nyumbani kwake akiwa amezungukwa na wapendwa wake, akiacha urithi mkubwa wa mapambano ya haki, usawa na utu kwa watu wote duniani.

Jackson alijulikana zaidi kama mmoja wa waliomfuata na kushirikiana kwa karibu na Dk. Martin Luther King Jr. katika harakati za haki za kiraia za miaka ya 1960 dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Kazi yake ilileta mabadiliko makubwa ya kijamii na kuibua matumaini kwa mamilioni ya watu waliokuwa hawana sauti.

Alizaliwa Oktoba 8, 1941, na alikulia katika eneo lililokuwa na ubaguzi mkali wa rangi kusini mwa Marekani.

Akiwa mwanafunzi, alijihusisha na maandamano ya kupinga ubaguzi, vitendo vilivyochagiza safari yake ya uanaharakati.

Baada ya kuuawa kwa Martin Luther King mwaka 1968, Jackson akawa mmoja wa viongozi wakuu wa harakati za haki za kiraia nchini Marekani.

Aliunda mashirika kadhaa ya kiraia kama Operation PUSH na baadaye Rainbow/PUSH Coalition, ambayo yaliangazia umuhimu wa usawa wa kiuchumi, ajira na haki za rangi.

Aligombea uteuzi wa kuwa mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Democratic mara mbili, mwaka 1984 na 1988, na kumfanya kupata umaarufu mkubwa hasa kwa sauti ya watu walioachwa nyuma kisiasa na kijamii.

Kutokana na mchango wake, alipata tuzo ya Presidential Medal of Freedom, heshima ya juu kabisa ya kiraia nchini Marekani.

Changamoto za afya na mwisho wa safari

Jackson aliendelea kupigania haki hata baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa Parkinson’s na baadaye Progressive Supranuclear Palsy, hali ya neva iliyoathiri mwili na kuzuia baadhi ya shughuli za kawaida.

Matamshi ya familia na jamii

Familia ya Jackson ilisema:“Alikuwa kiongozi wa huduma sio tu kwa familia yake, bali kwa maskini, wasio na sauti na wale waliopuuziwa kote duniani.

“Tunawaomba muendeleze mapambano ya yale aliyoishi kwa ajili ya haki, usawa na upendo.”

Viongozi wa siasa na jamii za kila upande wa kisiasa wameitaja kazi yake kuwa ya mchango mkubwa katika historia ya haki za binadamu na ustawi wa wanajamii.