Same. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amechangisha jumla ya Sh2.8 milioni kwenye mkutano wake wa hadhara, kwa ajili ya malipo ya fundi ujenzi aliyejenga vyoo vya Shule ya Sekondari Gonja.
Fundi huyo amekuwa akidai fedha hizo tangu mwaka 2022, lakini hakuwahi kulipwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, jambo ambalo limemshangaza Dk Mwigulu na kuamuru fundi huyo alipwe mara moja uwanjani hapo.
Waziri Mkuu ameanza ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro, ambapo amekagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi. Kiongozi huyo ametokea mkoani Tanga, ambako alibaini ubadhirifu wa fedha za umma katika baadhi ya maeneo, hususan Muheza.
Akiwa wilayani Same, Kilimanjaro, leo Februari 18, 2026, Dk Mwigulu amesikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya mabasi ya Ndungu wilayani humo, na mmoja wa waliojitokeza ni fundi aliyejenga vyoo hivyo.
Akitoa maelezo yake mbele ya Waziri Mkuu, fundi huyo ameeleza kuwa, kutokana na kutolipwa fedha hizo, ndoa yake iliingia matatani baada ya kuamua kuuza mifugo yake ili kuwalipa wasaidizi wake.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulipewa vyoo vya kujenga katika Sekondari ya Gonja toka mwaka 2022, nimejenga vyoo hivyo. Nimebabaishwa kupewa malipo yangu mpaka leo hii, nadai Sh2.8 milioni, sijalipwa. Nimewapa watu kazi mpaka nimeuza ng’ombe zangu, na ndoa yangu imekuwa na mgogoro kwa sababu ya hii kazi.
“Mkuu wa wilaya, mkurugenzi wanajua, lakini kuna mhandishi mmoja, ameshaondoka, aliwahi kuniomba rushwa, nikamwambia sitoi rushwa wala sipokei rushwa, na hivyo naona ndiyo sababu sijalipwa pesa zangu mpaka leo. Naomba kama kuna uwezekano nisaidie hizo fedha niwalipe hawa vijana, ninaonewa,” amesema.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Dk Mwigulu alimwita Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, ambaye amekiri kufahamu malalamiko hayo na kwamba alimwagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kuyashughulikia.
“Ni sahihi kwamba huyu mzee alipewa kazi za kujenga vyoo, hili suala nimelishughulikia, nikamwagiza mkurugenzi kufanya malipo hayo,” amesema Mgeni.
Kabla mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Jimson Mhagama, hajajibu kuhusu malipo hayo, Waziri Mkuu aliwataka kutoa fedha zao kwa kuchangishana ili kumlipa fundi huyo, kwani fedha hiyo haiwezi kutoka serikalini kwa kuwa muda mrefu umepita.
“Hapo mlipokaa, toeni, kila mtu mwenye fedha mfukoni, toeni sasa hivi nione mnamlipa.
“Mwaka 2022 hadi leo, vyoo vinatumika tangu mwaka 2020, hamjawahi kupata Sh2 milioni? Lipeni hapa hapa,” amesema Waziri Mkuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo alimjibu: “Mheshimiwa, tunamlipa leo leo.”Mkandarasi huyo aliitwa pembeni, kila mmoja akajipapasa mfukoni, baadaye mlalamikaji huyo aliondoka eneo hilo akiwa na furaha.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu, amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro, kuchunguza miradi ambayo fedha zake zimeshatolewa na haijakamilika na kumpa majibu kabla hajaondoka mkoani humo.
Amesema ipo miradi ya shule, afya pamoja na barabara ambayo haijakamilika, ilhali Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu amehoji ujenzi wa Zahanati ya Sujigojanza, ambayo Serikali imetoa fedha lakini haijakamilika.
“Hizi fedha zimekuja siku nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Sujigojanza, ni kwa nini hamjatekeleza mradi huu? Takukuru, naomba tufuatilie kabla sijamaliza ziara ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro, nipate majibu,” amesema Waziri Mkuu.
Akijitetea, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Same, Mhagama, amesema kilichokwamisha mradi wa zahanati hiyo ni mgogoro uliopo baina ya kijiji na kijiji.
Aidha, amesema baadhi ya miradi haijakamilika kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, akimuahidi kukamilisha miradi hiyo.
Jana, Dk Mwigulu alihitimisha ziara yake mkoani Tanga, akimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, kurudi Halmashauri ya Muheza na kusafisha watumishi wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za mradi wa jengo la ofisi.
“Muheza ndiyo wilaya iliyonidisapointi (iliyonikatisha tamaa) sana kwa sababu huku kwingine nimekuta upungufu, bali kule Muheza ni uharibifu. Mheshimiwa Waziri, kesho rudi Muheza, nenda kachukue hatua. Shirikiana na waziri wa utumishi, mchukue hatua,” amesisitiza.
Dk Mwigulu amesema kuna baadhi ya vifaa vilinunuliwa lakini havikufika eneo la mradi. “Nondo zenye thamani ya Sh9.2 milioni zililipwa kwa mzabuni Saifi Store wa Tanga, lakini hazikufikishwa site, maana yake zimechepushwa.”
“Kuna marine boards vipande 192 vyenye thamani ya Sh7.8 milioni havikufika site. Wanaohusika ni Mhasibu, Rajab Mushi, na Mhandisi Abdalla Jaha, na ofisa anayehusika kupokea vifaa.”