NIKWAMBIE MAMA: Ufisadi hili ni zimwi linalotujua haswaa!!

Nakumbuka kisa cha panya mdogo aliyeingia kwa bahati kwenye kikao nyeti cha panya wazee. Kikao kilihusu namna ya kumdhibiti adui yao mkubwa, paka.

Kiliendeshwa kwa nidhamu kubwa, kila mmoja akipata nafasi ya kuchangia hoja. Mmoja alitoa wazo la kumfunga paka kengele. Hoja hii iliungwa mkono na wajumbe wote kikaoni.

Ilionekana kwamba akiwa na kengele, paka atajulikana kila mahala atakapokuwepo, hivyo hatapata nafasi ya kufanya shambulizi kabla panya hawajajiandaa.

Mtoa hoja alipongezwa kwa ubunifu wake kwenye nyanja za “kujihami”, na ilikuwa almanusura apewe uwaziri kwenye eneo hilo.

Lakini panya mdogo ambaye alimsindikiza babu yake kipofu pale mkutanoni, aliwaacha wenzake midomo wazi kwa swali lake fupi.

Alianza kwa kuunga mkono hoja, lakini akaendelea na swali: “Ni nani atakayekwenda kumfunga paka kengele?” Panya wote waliduwaa.

Hapo ndipo ninapoanza kuielewa kauli kwamba ufisadi ni mkubwa kuliko tunavyosikia. Wakati Mbunge aliposimama ndani ya Bunge la Tanzania na kusema ufisadi ni mkubwa kuliko tunavyokubali, watu wakasema, “Hilo si jipya bwana, ni kama kusema bahari inayokupwa na kujaa kila siku!” Lakini hoja hii ni kama ile hali ya mtu anayeficha tumbo kwa kuvuta pumzi ndani.

Katika historia yetu, tumewahi kusikia kauli kama: “Hili ni tatizo dogo tu, tutalimaliza ”, “Ni makosa ya kimfumo”, na “Tutaunda tume kulichunguza.”

Matokeo yake ni nini? Tume zinaundwa na kufanya kazi, ripoti zinachapishwa, wananchi wanafurahishwa na mapendekezo ya tume, wanapiga makofi… halafu maisha yanaendelea kuwa yaleyale. Ni kama sehemu ya pili ya tamthilia.

Ni kweli kuwa Watanzania wa leo sio wa jana na juzi. Zamani tulikuwa na uhakika kuwa cha ziada anachojua dereva wa bodaboda ni njia za mkato. Leo anajua bajeti imesomwa lini, anajua bei ya saruji imepanda kwa nini, anafahamu tofauti ya ahadi na utekelezaji. Ukimpa dakika tano anaweza kuichambua hotuba ya bajeti na kukuonesha mstari uliojaa hewa.

Zamani watu waliamini kila jambo. Leo watu wanasikiliza stori huku wanaangalia mitandaoni kile unachokisema. Ukitangaza “barabara imekamilika,” kesho picha ziko mitandaoni zikionesha mashimo kama mabwawa ya samaki.

Kutokana na kukosa kazi, vijana wamejikuta wakiwa wachunguzi wa kujitolea. Wana simu janja, wana muda, na wana hasira ya kizazi chenye matumaini makubwa.

Hii hoja ina ladha ya mzaha mzito. Mara nyingi tulishuhudia dagaa wakibebeshwa lawama za ulalamishi wakati papa aliyewala akiombwa radhi kwa usumbufu wa dagaa.

Sawa na hukumu ya gari ndogo iliyogongwa na treni, gari ndogo ndiye anaonekana mkosaji kwa “kutohakikisha usalama wake”. Katika enzi zile, msako wa mwizi wa kuku ulikuwa mkali kuliko wa mwizi wa mabilioni.

Tulishuhudia kesi za ufisadi zikianza kwa mbwembwe: kamera, hotuba, maneno mazito na ahadi za “hatutavumilia”. Baada ya muda, kimya kizito kinashuka.

Watu waliopata jeuri ya kuuliza mwenendo wa kesi sio hawa tunaoishi nao mtaani. Inafikia mahala tunawahurumia wabunge wetu wanaolaumiwa bila makosa; aidha na mamlaka au na wananchi waliowachagua.

Wakisema wanaonekana vimbelembele, wakikaa kimya tunawaita wazembe. Kauli za mbunge huyu si mpya sana katika historia ya siasa zetu. Tofauti ni kwamba sasa zinatamkwa wazi zaidi. Ucheshi wake uko hapa: kila awamu hufikiri imegundua tatizo jipya, kumbe ni sura mpya ya tatizo la zamani (nyani wapya kwenye msitu wa kale).

Tatizo lilikuwepo, lipo, na tusipolitokomeza litaendelea kuwepo katika historia ya nchi yetu. Ni kama urithi usioandikwa kwenye katiba bali kwenye mazoea.

Ufisadi ni zimwi linaloiteketeza nchi. Ni kama jini linalorithiwa kwa vizazi. Kuna wanaouhalalisha kama sehemu ya maisha waliyoumbiwa na Mwenyezi Mungu. Wanawachukulia wale wanaoukataa kuwa hawajui maisha.

Bahati mbaya zaidi hao wanaouhalalisha ndio wahisani wetu. Ndio tunaotegemea uwepo wao. Hapo ndipo jamii inapochanganyikiwa: je, umkatalie anayekupa mkono kwa sababu mkono huo umezoea kuchukua zaidi kuliko kutoa?

Wengine husema, “Bila hongo mambo hayaendi.” Kauli hii imekuwa kama msemo wa kale. Ukienda kuomba kazi bila ‘maji ya mkuu’, ni kama umeenda shereheni bila zawadi. Haki imegeuzwa kuwa hisani.

Hapo ndipo ufisadi unapokua kimya kimya; si lazima uwe wa mabilioni yanayotajwa kwenye vichwa vya habari, wakati mwingine ni elfu kadhaa zinazoharibu misingi ya maadili.

Ufisadi unatisha kwa sababu hauko tu kwenye ripoti; uko kwenye mazoea, kwenye kauli zetu za kila siku, kwenye vicheko vyetu vya kujifariji. Umekuwa kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku: tunaucheka, tunauzoea, na mwisho tunauhalalisha. Pengine siku moja atatokea “panya” jasiri wa kweli atakayemfunga paka kengele.

Lakini kama ilivyokuwa kwa panya wale, swali bado linasimama: ni nani atakayemfunga paka kengele? Je, ni yule aliye karibu naye na anayefaidika na mfumo? La hasha. Au ni yule anayehofia kupoteza hata kile kidogo alichonacho? Ole wake! Pengine paka adangaywe kuwa kengele ni urembo, aivae mwenyewe. Yote kwa yote, penye nia pana njia. Lisilowezekana kwa panya kwa Mungu linawezekana.