KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema licha ya kushindwa kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini wamepata somo zuri wanalotaka kuanza kulitumia kesho Alhamisi dhidi ya Copco FC na mechi nyingine zijazo za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA).
Singida BS iliyokuwa Kundi C la michuano hiyo ikishiriki kwa mara ya kwanza ilimaliza mkiani ikiwa na pointi tano sawa na Stellenbosch ya Afrika Kusini, inarudi uwanjani kesho kwene Uwanja wa Airtel kukabiliana na Copco kutoka Mwanza katikaa mechi ya 64 Bora wa Kombe la Shirikisho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema haikuwa rahisi kwa Singida BS katika michuano hiyo ya CAF ikiandika rekodi ya kucheza kwa mara ya kwanza, lakini juhudi za kuipambania nendo ya klabu naa kujiamini uwanjani imefikisha walipo na sasa wameona mwanga na wanaamini wakirudi tena kutakuwa na malengo mengine makubwa.
“Nachukua nafasi hii kuupongeza uongozi, wachezaji na mashabiki kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha kuanzia mwanzo hadi hapa tulipofika, haikuwa rahisi bila wao tusingeweza. Wametupa nguvu tunaahidi kupambana zaidi katika Ligi na Kombe la CRDB ili tuweze kupata nafasi nyingine ya kurudi tena kimataifa msimu ujao,” alisema Ouma na kuongeza;
“Ili uweze kuwa bora ni kushiriki mara kwa mara na sisi tunataka kuwa bora tena kwa kuandika rekodi nzuri ambayo itabaki katika vitabu, hivyo Alhamisi (kesho) tutaanza kazi tukiwa uwanja wetu wa nyumbani kusaka tiketi ya uwakilishi.”
Ouma alisema anaamini mechi itakuwa nzuri na yenye ushindani, kwani hata wapinzani wao wana matarajio kama yao.
“Hatuwezi kuwa bora kama hatutamheshimu mpinzani tunaenda kukutana na nyota wengine 11 kutoka timu pinzani haitakuwa rahisi juhudi ya mchezaji mmoja mmoja na mipango sahihi ya mbinu kutoka kwetu itaisaidia timu kupata matokeo mazuri tukiwa uwanja wa nyumbani na mashabiki zetu kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo,” alisema Ouma aliyewahi kuinoa Coastal Union aliyeongeza;
“Wana Singida wanataka furaha na sisi tunataka kuuzindua uwanja kwa mechi za mashindano kwa ushindi, matarajio ni makubwa na maandalizi pia yatakuwa bora ili kuendana na tunachotamani kukipata baada ya dakika 90 za pambano la kwanza la msimu huu la Kombe la CRDB.”